Sunday, April 21, 2013

LOWASA AWAASA WATANZANIA

 Waziri mstaafu Edward Lowasa akiwa katika ukumbi wa St. Dominic kabla ya kuanza kwa harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa la Overcomes na kituo cha radio.

Mkuu wa mkoa wa Iringa Dr. Christine Ishengoma, kiwa na waziri mstaafu Lowasa, wakipata maombi kutoka kwa mchungaji Boazi Sollo wa kanisa la Overcomes kabla ya kuanza kwa aharambee ya ujenzi wa kanisa la Overcomes na kituo cha redio.
 Waumini wakisikiliza jambo, katika harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa na kituo cha redio ya Overcomes mjini Iringa katika ukumbi wa St. Dominic.
 Mchungji Boazi Sollo akisoma risala ya ujenzi wa kanisa, mbele ya mgeni rasmi waziri mstaafu Edward Lowasa
 Waziri Mstafu Edward Lowasa akionyesha Tuzo aliyopewa na mchungaji Boazi Sollo, wa kanisa la Overcomes la mjini Iringa.

 Mbunge Kangi Lugola wa jimbo la Mwibala (kushoto)  wakiteta jambo na mbunge wa Ludewa Deo Filikunjombe.
 Mbunge wa viti maalumu CCM Iringa mjini Ritha Kabati akiwa na mbunge Mendrad Kigola, katika harambee hiyo.

 Mbunge wa Mufindi Kasakazini (Iringa) Mendrad Kigola, akisema neno katika harambee hiyo.
 Mbunge Kangi Lugola wa jimbo la Mwibala, akisema neno katika harambee hiyo.
 (Kulia) Mbunge wa Ludewa Deo Filikunjombe, kimsikiliza kwa makini waziri mstaafu Edward Lowasa wakati wa harambee ya ujenzi wa kanisa na kituo cha redio. 
Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowasa amesema kuwa Watanzania tunatakiwa kuwa makini na swala la kuzuka kwa udini pamoja na ukabila kutokana na kuwa athari za kuwepo kwa mambo hayo kumeleta matokeo mabaya kwa baadhi ya nchi jirani ambazo zinaizunguka Tanzania ambapo amewataka wananchi kuungana na kuuendeleza umoja, amani na mshikamano ambao waasisi wa taifa hili waliuweka.
Akizungumza katika ukumbi wa St. Dominic uliopo mjini Iringa wakati akiendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa na kituo cha Redio ya Overcomers kilichopo katika eneo la Frelimo B, Waziri Mstaafu Edward Lowasa amesema kuwa Watanzania wanatakiwa kujifunza kutoka kwa nchi jirani ambazo zinaizunguka ambazo ziliingiza udini, ukabila, ukanda na hatimaye kuingia katika wimbi kubwa la vita za wenyewe kwa wenyewe.
“Nchi zinazoizunguka Tanzania zikiwemo Kenya, Burundi, Rwanda, Uganda pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameingia katika migogoro ya udini, ukabila, malumbano makubwa na migogoro mingi hali ambayo ilisababisha waanze vita baina yao mimi ninawaasa ndugu zangu tuilinde amani iliyopo, ili taifa liweze kuendelea kuwa kisiwa cha amani”, alisisitiza Lowasa.
Akimnukuu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Lowasa alisema kuwa aliwahi kusema kuwa kama watanzania wataulizwa na kuhojiwa na watu wa mataifa mengine duniani kitu wanachojivunia ndani ya taifa lao kuwa alisema kuwa wanatakiwa kusema ni amani iliyopo ndani ya nchi ambapo alisema kuwa amani hii ilitokana na viongozi waasisi wa taifa letu kuondoa mizizi ya udini, ukabila, ukanda na kuwafanya watanzania kuwa kitu kimoja.
Aliongeza kuwa Vyombo vya habari vinayo nafasi kubwa ya kuhakikisha vinaijenga Tanzania yenye watu wamoja ambao hawagawanyiki kwa misingi ya udini na ukabila na kusema kuwa vita vya udini na ukabila huwa havina mshindi ambapo amewataka waandishi wa habari nchini kuacha kuimomonyoa amani iliyopo badala yake kila chombo cha habari kihakikishe kinawaunganisha watanzania kuwa kitu kimoja.
“Tukianza kutengana sisi kwa sisi ndani ya nchi moja kwa matabaka ya dini, makabila, ukanda tutaitoa amani iliyopo na kuingia kwenye vita kubwa itakayoleta balaa kubwa nchini kwa wananchi wa sasa na vizazi vijavyo, Watanzania wote tujisahihishe pale tulipokosea, turudi katika kundi moja lenye jina moja la Tanzania na siyo kugawanyika kimakundi”, alisema Waziri Mstaafu Edward Lowasa.
Askofu Boazi Sollo wa kanisa la Overecomers amesema kuwa ujenzi wa kituo hicho tayari umetumia milioni 60 ambapo ujenzi uliobakia unahitaji jumla ya shilingi milioni 150 ili kufanikisha kujenga kanisa, kituo cha redio cha Overcomers FM pamoja na kituo cha Wahitaji ambacho kinasimamiwa na kanisa hilo.
Askofu Boaz Sollo amesema kuwa hadi sasa kituo chake hakina nyumba maalumu ambayo wanaweza kutumia katika kuendeshea shughuli zao ambapo alisema kuwa eneo Frelimo B ambalo wanalitumia kwa sasa katika  kutangaza neon la Mungu, kutoa huduma mbalimbali kwa jamii halitoshi ambapo wamenunua eneo jipya Zizilang’ombe ili kuhakikisha wanafanya huduma zao kwa weledi mkubwa kwa jamii ya watanzania wote.

Aidha amesema jumla ya shilingi Milioni 250 zinahitajika katika kukamilisha ujenzi huo, huku zaidi ya shilingi Milioni  72 zikikusanywa katika harambee hiyo iliyoendeshwa na waziri mstaafu Lowasa,  kati ya michango hiyo- fedha taslimu ikipatikana shilingi milioni  32.


“Kufanikiwa kwa mambo mengi mazuri kunatokana na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na waasisi wenzake ambao walipanda mbegu ya amani mioyoni mwa watu ambayo hadi leo tunaendelea kudumu nayo, kufanikiwa kwa mambo mengi mazuri kunatokana na juhudi zao, amani tunayoiona leo na kuishi nayo tangia tupate uhuru kuna watu waliumia kuipanda, waliteseka kuipanda sasa sisi tunaivuna kwa furaha, tunatakiwa pia tuilinde”, alisema Askofu Boaz Sollo.
Mbunge wa Ludewa Deo Filikunjombe akizungumza katika hafla hiyo alisema kuwa watanzania wanatakiwa walinde amani iliyopo, wasiingie kwenye migogoro ambayo itawatenganisha na kuwaingiza katika vita za wenyewe kwa wenyewe ambapo amewataka wakatae kwa nguvu zote mambo ya udini, ukabila, ukanda na kuwataka watanzania wajisikie ni wamoja.
“Watanzania ndani ya nchi yetu tunatakiwa kuendelea kupanda mbegu njema ili tuweze kuendelea kuvuna mambo mema zaidi yakiwemo upendo kati yetu, amani kati yetu utulivu na uaminifu, tukiacha kuifuata misingi ya waasisi wetu tutaingia kwenye migogoro ambayo matokeo yake yataliangamiza taifa letu lililodumu kwa nusu karne pila vita”, alisema Deo Filikunjombe mbunge wa Ludewa.
Waziri Mkuu Mstaafu Lowasa ambaye alitokea Dodoma Bungeni, aliongozana na wambunge mbalimbali wakiwemo  Deo Filikunjombe jimbo la Ludewa, Kangi Lugola wa jimbo la Mwibala, Mendrad Kigola Mufindi Kusini na Ritha Kabati Viti Maalum mkoa wa Iringa ambapo wabunge hao wakati wakizungumza walisisitiza watanzania kuachana na kutengana kwa makundi ya udini na kuwa badala yake wanatakiwa waungane kuwa kitu kimoja na kuendeleza kulinda amani.

No comments:

Post a Comment