Wednesday, April 24, 2013

KIGOMA WAISHUKURU NHIF KUPELEKA MADAKTARI BINGWA, WAGONJWA 750 WAPATIWA TIBA

2Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Issa Machibya akizungumza na timu ya madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Taasisi ya Mifupa (MOI) mara baada ya kumalizika kwa zoezi la kuhudumia mamia ya wagonjwa katika Hospitali ya Mkoa ya Maweni mkoani humo
3Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Ramadhan Maneno akitoa neno la shukrani kwa kazi kubwa iliyofanywa na madaktari hao mpango ambao unatekelezwa na NHIF (Kutoka kulia kwake ni Dk. Vence wa MOI, Dk. Kisenge na Dk. Makia wa Muhimbili.4 IMG_8674 
Wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Kigoma
BAADHI ya wagonjwa waliopata fursa ya kuhudumiwa na madakri bingwa katika Hospitali ya Mkoa ya Maweni mkoani Kigoma, wameushukuru Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa kuanzisha mpango huo kwa kuwa umesaidia kuokoa maisha yao.

Wamesema wamefarijika sana kutokana na ukweli kwamba ni vigumu kwao kumudu gharama za kuwafuata wataalam hao katika Hospitali za Rufaa Bugando, KCMC au Hospitali ya Taifa ya Muhimbili hivyo wameiomba Serikali kupitia Mfuko huo kukarisha mpango huo ambao unasaidia wananchi hasa wa kipato cha chini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mkoani humo baadhi ya wagonjwa walionufaika na huduma hiyo wamesema kuwa bado  wana mahitaji makubwa ya huduma ya madaktari bingwa kwa kuwa hazipatikani katika hospitali hiyo.

“Wananchi wengi wanahitaji huduma hii kutokana na urahisi wa kuwapata madaktari  hawa…ni ngumu sana kwetu kumudu gharama za kuwafuata huko waliko kutokana na hali za vipato lakini pia miundombinu ya mkoa wetu, hivyo mimi binafsi naushukuru sana Mfuko kwa kazi hii kubwa,” alisema Mkazi wa Mwanga mjini Kigoma,Zawadi Daudi.

Alisema kuwa alibahatika kupata huduma ya upasuaji kutoka kwa madaktari bingwa hao, kutokana na uvimbe wa tumbo, uliokua ukimsumbua kwa muda mrefu.

Mgonjwa mwingine Anna Sebastian alisema anamshukuru Mungu tatizo lake la tumbo, limepatiwa matibabu kwa kufanyiwa upasuaji na mabingwa hao.

Lakini, alisema ana ndugu zake wengi ambao walihitaji huduma za madaktari hao, lakini hawakuipata kutokana na muda waliokuwa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya alitoa shukrani kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kubuni mpango huo, ambao unatoa unafuu mkubwa kwa wananchi  kupata huduma za madaktari bingwa.

Alisema hayo alipozungumza na madaktari hao, ambao walifika ofisini kwake kutoa taarifa ya kuhitimisha awamu  ya kwanza ya mpango huo mkoani kwake.

Machibya alisema kumekuwa na upungufu mkubwa wa madaktari hao nchini na hasa kwa mkoa wa Kigoma hivyo kuja kwa madaktari hao,kumepunguza tatizo la wananchi kupata huduma za madaktari bingwa.

Akitoa takwimu hizo Mkurugenzi wa tiba na masuala ya kiufundi wa mfuko wa taifa wa bima ya afya(NHIF), Frank Lekey amesema  jumla ya watu 754 mkoani Kigoma, walionana na madaktari bingwa na kupata ushauri mbalimbali.

Alisema jumla ya wagonjwa 37 walifanyiwa upasuaji mkubwa,ikiwemo kufanyiwa upasuaji wa magojwa ya tumbo kwa akina mama ,magonjwa ya moyo na figo na magonjwa ya kawaida.
Alisema baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza, Mfuko utaendelea  kuratibu upatikanaji wa huduma ya madaktari bingwa kila baada ya miezi mitatu.

Alisema katika awamu hiyo ya kwanza wamebaini kuwa kuna mahitaji makubwa ya huduma hiyo ya madaktari bingwa kwa mikoa ya pembezoni mwa nchi.

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umekuwa ukiboresha huduma zake mara kwa mara na kwa sasa unatekeleza mpango wake wa kusogeza huduma karibu na wanachama wake lakini pia wananchi kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment