Friday, December 7, 2012

POLISI MARA YAKANUSHA UVUMI WA WATU 15 MKOANI HUMO KUCHINJWA.

Jeshi la Polisi Mkoani Mara limekanusha uvumi wa kutishia wananchi toka kwa baadhi ya watu wenye nia mbaya kuwa ndani ya mwezi mmoja watu 15 wameuwawa kwa kuchinjwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kaimu kamanda wa Jeshi la Polisi Mara, Musoma Japhet Lusingu imedai kwamba hivi karibuni kumekua na uvumi kuwa katika Mkoa wa Mara wananchi wamekuwa wakichinjwa na tayari watu 15 wameuwawa kwa kuchinjwa kitu ambacho ni uongo.

Kaimu kamanda huyo amesema kutokana na uvumi huo wamekua wakipokea simu toka kwa wananchi na viongozi ndani ya manspaa ya Musoma katika kata ya nyakato kwamba kuna kuna mwanafunzi ameonekana ameuwawa kwa kukatwa kichwa katika makaburi ya Musoma bus na jeshi la polisi likifuatilia wanakuta ni taarifa za uongo na za kuwatisha wananchi.
Amesema kuna matukio mawili wanawake kuuwawa vichakani katika vijiji vya Mmahare kata ya Etaro ambapo Blandina Peru (28) aliuwawa 2.12.2012 kwa kukatwa koromeo na kubakwa na wauaji kabla ya kumuua wakati akiwa porini akikata kuni na watuhumiwa wa tukio hilo bado hawajakamatwa.
Tukio la pili lilitokea Kabegi kata ya Nyakatende wilayani butiama ambapo Sabina Mkireri (44) mkazi wa kijiji cha kiemba aliwawa kwa kuchinjwa shingo na kichwa chake kuchukuliwa na watu wasiojulikana katika kijiji cha kabegi na watu sita wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano.
Kutokana na uvumi huo amewatoa hofu wananchi  juu ya mauaji hayo na kuwatahadharisha akina mama hasa maeneo ya vijijini wanapokua katika shughuli zao za kilimo na utafutaji wa kuni wawe waangalifu na watoe taarifa mapema wanaposhuku jambo lolote lisilo lakawaida.
Ameongeza kuwa kwa sasa wanaendelea na msako maeneo mbalimbali ya manispaa ya Musoma na wilaya ya butiama ambapo kuna watu watano wanashikiliwa na jeshi hilo kwa kwa makosa yakupatikana na pombe haramu ya gongo na wengine wanashikiliwa kwa kupatikana na bangi na wote watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Katika hatua nyingine amewataka wananchi wenye taarifa za uhalifu na wahalifu wasisite kulijulisha jeshi la polisi kupitia kwa viongozi wa maeneo yao.

No comments:

Post a Comment