Saturday, November 24, 2012

KCB BENKI YATOA ELIMU KWA WAJASILIAMALI WA KATI NA WADOGO ( SMEs) VISIWANI ZANZIBAR

 
Na Mohammed Mhina, Zanzibar

ZANZIBAR IJUMAA NOVEMBA 23, 2012. Benki ya KCB nchini imeanza kutoa mafunzo kwa wajasiliamali wadogo na wa kati ili kuwawezesha kukuza miradi na mitaji yao ya kiuchumi.

Wakati wa mafunzo hayo, pamoja na mambo mengine wakufunzi wa Benki hiyo wamesema nia ni kuongezea uwelewa wa namna ya kuanzisha miradi kuendesha biashara ndogondogo na utunzaji wa fedha benki kwa wajasiliamali hao.

Wakati wa mafunzo hayo, pamoja na kuelimishwa masuala mbalimbali juu ya kukuza mitajio na uansishaji wa biashara mpya, Wakufunzi Bw. Fredrick Lyimo na Bw. Francis Mandala, wamesema benki hiyo inaendelea na mpango wake wa kuboresha huduma kwa wateja.

Wamesema kuwa pamoja na kutoa elimu hiyo kwa wajasiliamali, KCB Bank ambayo ina matawi katika nchi zote tano za Afrika ya Mashariki, pia hutoa misaada mbalimbali ikiwemo ya Vifaa vya Afya, Elimu na huduma nyingine za kijamii.

Washiriki hao wameelimishwa jinsi ya kuweza kuomba na kupatiwa mikopo pamoja na kufundishwa jinsi ya kuitumia mikopo wanayoipata.

Akitoa elimu juu ya biashara na namna ya kukuza mitaji, mmoja wa wakufunzi Bw. Peace Lumelezi, amesema kuna haja ya kila mfanyabiashara kutofautisha biashara yake naya mwingine ili kupata faida.

Amesema kuwa hata kama biashara ya mfanyabiashara mmoja inafanana naya mwingine katika eneo moja, lakini ni lazima kufanyabiashara makini atofautishe biashara yake hata kwa lugha kwani wateja wanahitaji huduma bora.

Amewashauri pia wafanyabiashara kutokwepa kodi za Serikali na kujiwekea bima ili kuepuka ajali na hasara za majanga ya moto ama wizi.

Amewakumbusha wajasiliamali hao mfanya biashara zao kwa kufuata taratibu na masharti ya leseni zao na kuepuka kukwepa kodi mambo yanayoweza kupelekea kufilisiwa ama kushitakiwa na Mamlaka ya Kodi za mapato yaani TRA kwa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ZRB kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, wameelezea changamoto mbalimbali zinazowakuta na kusema baadhi ya waomba mikopo wamekuwa wakitoa taarifa za uongo katika mabenki ili mradi waweze kupatiwa mikopo jambo ambalo halijengi uaminifu kwa taasisi za fedha.

Pamoja na kuelezea kunufaika na mafunzo hayo, washiriki hao pia wameiomba benki ya KCB hapa nchi kuangalia uwezekano wa kuongeza matawi zaidi ya kenki hiyo pamoja na kuongeza idadi za mashine za kutolea fedha yaani ATM karibu na maeneo yenye wananchi wengi.

Wamesema kwa ulimwengu wa sasa hakuna mtu anayependa kutembea na fedha nyingi mfukoni kwa kutoka eneo moja hadi jingine kwa kuhofia kuporwa ama kuibwa kwa fedha zake.

Wamesema kama kutakuwa na matawi mengi ya benki ni rahisi kwa wajasiliamali kufanya biashara zao na kuweka fedha zao benki lakini wakazichukua hata kwa kupitia katika mashine za ATM pale wanapozihitaji kwa matumizi ya kawaida ama ya kibiashara.

Hata hivyo wamepongeza juhudi zinazochukuliwa na Benki hiyo katika kuwaelimisha wajasiliamali bila kujali kama ni wateja wa benki hiyo ama vinginevyo.

Wamesema elimu hiyo imewasaidia kwa kiasi kikubwa kujitambua na jinsi ya kukuza mitaji na kuboresha biashara zao.

No comments:

Post a Comment