Wananchi wakifuatilia Mada ya Katiba
Na Mwandishi wa
Thehabari.com Morogoro
TAASISI ya Jukwaa
la Katiba Tanzania imelazimika kugawa nakala ya Katiba ya Tanzania kwa
washiriki wa Mkutano wa Jinsia Ngazi ya Wilaya uliofanyika nje kidogo ya Mkoa
wa Morogoro kabla ya kuanza kuelezea umuhimu wa Tanzania kuingia katika
mchakato wa kuundwa kwa Katiba Mpya unaoendelea hivi sasa.
Tukio hilo
lilitokea juzi Kijijini Mkambarani ulipokuwa ukifanyika Mkutano wa Jinsia ngazi
ya Wilaya ulioandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), ambapo Jukwaa la
Katiba lilialikwa kutoa mada juu ya umuhimu wa wananchi kushiriki kikamilifu
katika mchakato wa Katiba mpya.
Idadi kubwa ya
wananchi kutoka vijiji mbalimbali walisema hawajawahi iona Katiba hivyo, hivyo
Mratibu wa Jukwaa la Katiba, Bi. Diana Kidala kulazimika kutoa nakala ya Katiba
kwa wananchi wote kabla ya kuanza mada yake.
Bi. Kidala
aliwataka wananchi hao kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni juu ya uundwaji
Katiba Mpya ili katiba itakayopatikana iweze kuleta mabadiliko kwa kila
mwananchi pasipo na ubaguzi wa aina yoyote.
“Tushiriki kwa
namna yoyote tutoe maoni yetu ili yaingizwe kwenye Katiba mpya. Katiba ndiyo
msingi wa sheria zote...Katiba iliyopo sasa inamapungufu mengi, tunamshukuru
Rais Jakaya Kikwete kwa kuona dosari hizo na kuridhia kuanza kwa mchakato wa
uundwaji Katiba Mpya,” alisema kiongozi huyo.
Hata hivyo
wakichangia wananchi hao katika mkutano huo walioneshwa kushangazwa zoezi la
ukusanyaji maoni mkoani kwao (Morogoro) kupita huku wengi wakiwa hawajui
chochote wala kushiriki kutoa maoni, jambo ambalo Bi. Kidala alitoa maelekezo
kuwa bado wananafasi kushiriki katika zoezi hilo kwa nafasi nyingine.
“Kwa sasa bado
mnanafasi ya kutoa maoni kwa kuandika barua kwenye vikundi kwenda Tume ya
Katiba, kushiriki katika upendekezaji wawakilishi kwenye mabaraza ya katiba ili
wawakilishe maoni yenu, na pia kupendekeza wajumbe na wabunge wa Bunge la
Katiba...tuelimishe, tuelimishane na tusichoke kutoa maoni kwani hakuna
mtaalamu wala mbumbumbu katika suala hili,” alisema Kidala.
Kwa upande wake
TGNP iliwataka wananchi kuunganisha nguvu katika utoaji maoni ili sauti zao
ziweze kusikika ipasavyo katika uwasilishaji wa maoni yao kwenye mchakato mzima
wa uundaji Katiba mpya.
*Habari hii imeandaliwa
na www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment