Thursday, October 18, 2012

ASKARI POLISI AUAWA ZANZIBAR

Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi zanzibar
 
Askari Polisi mmoja wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Ziwani Mjini Zanzibar ameuawa kwa kukatwakatwa mapanga na watu wanasadikiwa kuwa ni wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho.
 
Kamishna wa Polisi Zanzibar CP mussa Ali Mussa, amemtaja askari aliyeuawa kuwa ni mwenye namba F.2501 CPL Saidi Abdrahamani Juma(41) ambaye aliuawa saa 6.30 usiku wa kuamkia leo wakati akiwa njiani kurejea nyumbani baada ya kumaliza zamu yake ya kazi.
 
Katika hatua nyingine Kamishna Mussa amesema watu kumi wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kufanya fujo na vurugu zilizopelekea uharibifu mkubwa wa barabara kwa kuchoma matairi na kuweka mawe barabarani.
 
Amesema na misako mbali mbali imeanzishwa kuwakamata wale wote waliofanya mauaji ya CPL Said Abdulrahman. Tuelewe kuwa aliyeuliwa ni askari Polisi, ni raia wa Tanzania na ni muumini wa dini ni lazima tuhakikishe waliofanya unyama huu wanakamatwa na kufikishwa Mahakamani kama Sheria za nchi zinavyotuelekeza.
 
Amesema kuuawa kwa askari huyo kunafuatia fujo na vurugu za wafuasi wa Jumuiya hiyo ya uamsho Sheikhe Faridi ambapo amesema hadi sasa watu kumi wamekamatwa kwa tuhuma za makosa mbali mbali yaliyotokana na vurugu hizo.
Kamishna Mussa amesema upelelezi wa kujua ukweli juu ya uvumi wa kutekwa kwa Sheikh Farid bado unaendelea.
 
Amesema kuwa jana majira ya saa 6:30 za mchana Sheikh Mselem alifika katika kituo cha Polisi Madema mkoa wa Mjini Magharibi na kutoa taarifa za kupotea kusikojulikana kwa Bw. Faridi.
 
Akimkariri mmoja wa Viongozi wa Uamsho, Kamishna Mussa amesema Bw. Faridi ambaye hadi sasa hajulikani aliko akipotea tangu tarehe 16,10,2012.
 
“Taarifa zilizoripotiwa polisi madema ni kuwa kuwa Kiongozi mwenzao wa Jumuiya ya UAMSHO Sheikh Farid ametekwa na hawamuoni tokea jioni ya tarehe 16.10.2012” Alisema kamishna Mussa.
 
Amesema baada ya taarifa hiyo Polisi walianza uchunguzi kwa kuwahoji watu mbalimbali walio karibu na Bw. Faridi ambapo amesema waliohojiwa ni pamoja na dereva wa Bw. Farid Bw. Said Omar Said.
 
Kamisna Mussa amesema kwa mujibu wa dereva wa gari ya Sheikh Farid, yeye alimuacha eneo la Mazizini baada ya kununua umeme na ni farid mwenyewe aliyemtuma dereva wake kupeleka umeme nyumbani wakati yeye Sheikh Farid akizungumza na watu wengine waliokuwemo kwenye gari moja aina ya NOAH ambayo namba zake hazikupatikana.
 
Amesema dereva huyo aliporudi tena katika eneo alipokuwa amemuacha Bw. Faridi hakumkuta na ndipo alipotoa taarifa kwa viongozi wengine wa Jumuiya hiyo.
 
Amesema wakati taarifa hizo zikipelekwa kuripotiwa Polisi wakati huo wafuasi wa Jumuiya ya UAMSHO walijikusanya katika msikiti wa Mbuyuni na kuanzisha fujo kwa kuanza kuchoma moto kwenye jaa la karibu na msikiti huo. Baadae fujo zilienea haraka katika maeneo mbali mbali ya mjini kwa kufanyika uharibifu mbali mbali wa mali za Serikali, Chama tawala na za wananchi kwa ujumla.
 
Mbali ya hofu kubwa kwa wananchi juu ya maisha na mali zao, fujo hizi zilileta hasira ya kuchoma na kuharibu miundo mbinu ya barabara, kuharibu maskani za Chama tawala CCM za Kisonge na muembeladu kwa kuzichoma moto. Gari moja ya Serikali ilivunjwa kioo kidogo cha pembeni, gari ya zimamoto kuvunjwa kioo cha mbele. Aidha walivunja duka la Pombe na kuiba mali iliyokuwemo ndani.
 
Kamisha wa Polisi Zanzibar ameendelea kuwaomba wananchi kudumisha amani na utulivu katika maeneo yao, kutupa taarifa za watu waliohusika na vurugu pamoja na mauaji ya askari wetu. Tuendelee kukumbushana kutii Sheria bila ya shuruti.

No comments:

Post a Comment