Wednesday, September 12, 2012

AJALI YAUA 13 NA KUJERUHI 14 MUSOMA


         
  Musoma,

AJALI  ya gari iliyotokea jana  jioni katika Kijiji cha Mkiringo Wilaya ya Butiama Mkoani Mara ikiwa safarini kutoka Musoma Kuelekea Nyamswa wilaya ya Butiama Mkoani Mara
imeuwa Watu 13  na  14 kujeruhiwa.

Wakiongea  na Tanzania daima  mashuhuda wa ajali hiyo iliyohusisha gari aina ya Toyota Hiace lenye namba T123 CAE iliyokuwa ikiendeshwa na dereva aliyefahamika kwa jina la Emmanuel Joseph maarufu kama Diouf ilikuwa katika mwendo kasi huku ikiwa imebeba abiria kupita kiasi waliokuwa katika safari hiyo.

Mashuhuda walisema  gari hilo likiwa katika mwendo  kasi lilipasuka tairi la nyuma upande wa kulia na kupinduka mara tatu na kupelekea vifo pamoja na majeruhi hao waliolazwa na kuhifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mara.

Kwa mujibu wa maelezo ya Mganga mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Mara Dk. Samson Wenani alisema kuwa  amepokea majeruhi pamoja na maiti waliohifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali hiyo.

Dk. Wenani aliwataja  waliofariki  ni watu 12 ambao walitambuliwa na ndugu zao huku mmoja akiwa bado hajatambuliwa kuwa ni dereva wa gari hilo Emmanuel Joseph,Pendo John (39) pamoja na mtoto wake Joseph Richard (5) wakazi wa Bisarye,Razak Shaabani,Hamis Kanyoro,Nyamazore John,Innocent Fares Kweka na Jiadhari Saidi Dogori wakazi wa Nyamswa.

Wengine waliotajwa kufariki katika ajali hiyo ni Makuli Maguri,Aizaki Hassan, pamoja na watu wengine wawili waliotambulika kwa jina moja moja la Masoke na Richard ambao ni wakazi wa Wilayani Butiama.

Aliwataja  majeruhi katika ajali hiyo wanaoendelea kupata  matibabu  huku hali zao zikiendelea kuimarika kuwa ni Nyamakunguru Fanuel,Nyamazege Warioba,Gosbert Waryoba,Hamisi Wisaka,Hamisi Gibombi na Hamis Nyaga.

Alisema  wengine waliojeruhiwa katika ajali hiyo na kulazwa katika Hospitali hiyo ni pamoja na Mganda Nyamajege,Efrancia Kiamanzi pamoja na Beatrice Siriwa ambao ni wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Chief Ihunyo waliokuwa wakitokea Jijini Dar es salaam kuelekea shuleni.

Majeruhi wengine ni pamoja na Mwalimu wa shule ya msingi Butiama  Betreace Komba ambaye amevunjika sehemu ya juu ya mguu wake wa kulia,Bunuli Madube pamoja na mtoto wa miaka nane Matha Makuli ambaye baba yake waliyekuwa naye katika ajali hiyo alifariki Dunia.

No comments:

Post a Comment