Taasisi ya Trade Mark East Africa (TMEA) imezindua mfuko wa
thamani ya dola za Kimarekani milioni 7.5 kufadhili miradi ya ubunifu katika
nchi tano wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inayolenga kuondoa
vikwazo vya biashara katika kanda hiyo.
TMEA ni taasisi inayofadhiliwa na mashirika mbalimbali ili
kuunga mkono juhudi za kusukuma mbele masuala ya mtangamano hususan ni katika
biashara na uchumi katika kuimarisha mkataba wa mtangamano wa EAC.
Mradi huo unaojulikana kama ‘’Mfuko wa Changamoto wa
Taasisi ya Trade Mark East Africa ‘’ uliziduliwa rasmi katikati mjini Kigali, Rwanda
na Mkurugenzi wa Afrika Mashariki wa taasisi hiyo, Mark Priestly.
Mfuko huo utakaoendeshwa kwa kipindi cha miaka mitatu
unalenga sekta binafsi na vyama vya kiraia, Shirika Huru la Habari la Afrika
Mashariki (EANA) limeripoti.
Priestly alibainisha kuwa changamoto kama vile kuwepo kwa vikwazo visivyo vya ushuru na
mchanganyiko wa vuzuizi vya usambazaji, ni masuala ambayo bado yanazuia
mtiririko mzuri wa uendeshaji wa biashara katika kanda.
“Sisi hasa tunatafuta ubunifu na mawazo mapya ya
kuchangamsha biashara katika Jumuiya EAC na kukabiliana na changamoto ambazo
inakumbana nazo,” aliongezea.
Uwekezaji mkubwa katika ubunifu wa miradi ulianza na sekta
binafsi na vyama vya kiraia ambavyo vinaweza kukuza biashara katika kanda ndani
ya EAC.
Mfuko huo umeshaanzishwa nchini Kenya
na Tanzania na muda si mrefu
utazinduliwa pia katika nchi za Burundi
na Uganda.
Waziri wa Viwanda na Biashara wa Rwanda, Francois Kanimba, alisema
mfuko huo ni mpango mwafaka ambao utakuza juhudi za nchi yake kubadilisha
uchumi na kuwa mhimili wa kutoa huduma kupitia usafirishaji bidhaa kwa wingi
nje ya nchi.
Alisema Mfuko huo unatoa nafasi kwa Wanyarwanda
kushindana kikanda kwa kuutumia ili kuendeleza biashara zao.
Na Nchi wananchama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)
zitaendelea kufanya mashauriano zaidi juu ya maombi ya nchi mbili za Sudani
Kusini na Somalia
kutaka kujiunga na jumuiya hiyo yenye wanachama watano.
Uamuzi huo ulifikiwa mwishoni mwa mkutano wa Baraza la
Mawaziri la EAC, ambalo ni chombo cha Sera cha Jumuiya hiyo, mjini Bujumbura nchini Burundi.
Vyanzo kadhaa kutoka katika mkutano huo vililiambia Shirika
Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) kuwa Baraza lilikuwa na maoni kwamba
maombi ya nchi hizo mbili ambayo yaliwasilishwa mwaka jana na mapema mwaka huu
yanahitaji muda zaidi ili yaweze kufikiriwa na jumuiya hiyo ya nchi za Kenya, Uganda,
Tanzania, Rwanda na Burundi.
“Baadhi ya nchi wanachama zinahitaji muda zaidi kujadiliana
na wadau wote kuhusu taarifa za kamati za uhakiki juu ya maombi ya Sudani
Kusini,” vyanzo hivyo vimesema.
Ilikubaliwa kuwa taarifa ya timu ya wahakiki iliyotumwa
Juba mwezi Julai kutathmini matayarisho ya Sudani Kusini kujiunga na EAC
itawasilishwa katika kikao kijacho cha Baraza la Mawaziri mjini Nairobi,Kenya,
Novemba mwaka huu.
Kuhusu maombi ya Somalia,
mawaziri hao walibainisha kuwa jambo hilo
linahitaji majadiliano ya ziada na wadau zaidi wa kimataifa wanaojihusisha na
juhudi za kuleta amani nchini Somalia.
Hata hivyo, Baraza lilimwelekeza Katibu Mkuu wa EAC
kuwasilisha maombi ya Mogadishu
katika kikao kijacho cha wakuu wa nchi wanachama.
No comments:
Post a Comment