Friday, February 4, 2011

SAKATA LA DOWANS SASA WANACCM RORYA WATISHIA KURUDISHA KADI

Rorya
 
Sakata la kampuni ya kufua umeme ya Dowans Tanzania Limeted kuhitaji serikali ya Tanzania kuIlipa kiasi cha shilingi bilioni 94 limeingia sura mpya baada ya wanachama wa chama cha mapinduzi wilaya ya Rorya kutishia kurudisha kadi kwa nia ya kukiama chama hicho endapo serikali itakubali kulipa fedha hizo.
Katibu wa Itikadidi na Uenezi wa chama cha mapinduzi wilaya ya Rorya Gerald Samwel,aliiambia Nipashe juzi katika kijiji cha Bwiri kuwa baada ya serikali ya CCM kutoa kauli za kukubali kulipa fedha hizo kwa kampuni hiyo,wanachama na viongozi mbali mbali ngazi ya kata na matawi wamekuwa wakimiminika katika makao makuu ya ofisi wilaya na kusema hawatakuwa tayari kuendelea kuwa ndani ya chama hicho endapo fedha hizo zitalipwa.
Alisema sakata hilo la Dowans limekiweka chama hicho katika hali tete kuendelea kuwapo wilayani rorya ambapo alitahadharisha serikali ya ccm kutumia kila uwezo kuhakikisha deni hilo halilipwi ikiwa ni njia moja wapo ya kukinusuru chama chao na kutowawebebesha mzigo wananchi.
Samwel alisema hayo wakati ziara ya mbunge wa jimbo la rorya Lameck Airo ya kukagua ujenzi wa vyumba viliwili vya madarasa na ofisi moja ya walimu katika shule ya msingi ya Bwiri ambavyo vinajengwa kwa shilingi milioni 30 zilizotolewa na mbunge huyo.
Alisema tangu kuibuka kwa sakata hilo la malipo ya dowans idadi kubwa ya wananchi wilayani rorya wamekuwa wakikataa kuchangia miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao kwa maelezo haiwezekani serikali kulipa fedha hizo kwa kampuni hewa huku wananchi wakinyonywa kuchangia huduma hizo za jamii.
“KIla kiongozi wa ccm hapa wilayani  hasa wanachama wa kawaida wamekuwa wakifika ofisini na kusema uamuzi wa serikali kuilipa dowans ndio mwisho wa ccm wilaya ya rorya na kwamba wanakusudia kurudisha kadi za uanachama sasa sisi kama viongozi tunaitahadharisha serikali hii ya chama chetu ijaribu kusikiliza kilio cha waliyoiweka madarakani …hawa wakubwa wakicheza tu watavuna walichokipanda”alisema Samwel.
Hata hivyo kiongozi huyo wa ccm wilaya ya rorya alisema inasikitisha kuona badhi ya viongozi wakikwepa kutoa uamuzi kuhusu malipo hayo ya dowans kwa kisingizio kuwa ni suala la kisheria huku akidai kuwa viongozi hao hao wamekuwa wakivunja sheria na katiba hapa nchini katika mambo mbalimbali ya maendeleo.
“Lakini mimi siamini hata kama ni jambo la kusheria kuilipa dowans je tunashindwaje kuwataja wamiliki wa kampuni hiyo kwa vile sheria za nchi yetu zinasema wazi mtu wan je hawezi kuwekeza nchini bila kuwa na mwenyeji sasa wao hawaoni kwa hilo tu wanavunja sheria iweje washindwe kuingilia jambo hili linalohusu maisha ya wananchi”alisema
Alisema kilio kikubwa cha wananchi ni kwamba wakati serikali ikisisitiza kulipa fedha hizo kampuni hiyo ya kufua umeme ya dowans huku idadi kubwa ya watanzania maeneo ya vijijini hawajawahi kuina nishati hiyo ya umeme katika kipindi chote cha miaka 50 bya uhuru huku serikali hiyo hiyo ikiruhusu mfumuko mkubwa wa bei za bidhaa muhimu nchini.
“Kwa mfano sukari wakati tukiomba kura kwa wananchi mwishoni mwa mwaka jana ilikuwa ikiuzwa kwa shilingi 1,400 hadi 1,600 kwa kilo lakini hivi sasa kilo moja inauzwa 2,000 na zaidi huku mche wa sabuni ukiuzwa 1,200 hadi 1,400 kutoka shilingi 700 mwishoni mwa mwaka jana wakati soda ikiuzwa kwa shilingi 600  hivyo hivyo bidhaa nyingine muhimu je hapa serikali yetu haioni inatengeza bomu katika siku za usoni kwa chama chetu”alisisitiza.
Akizungumza katika kijiji hicho mbunge Lameck aliwataka wananchi kuendelea kuchangia miradi mbalimbali ya maendeleo na kwamba atazidi kutoa msaada wa kuwezesha kukamika kwa miradi hiyo baada ya wananchi kuchangia michango yao.
“Nimetoa milioni 30 kwa ujenzi wa vyomba hivi vya madarasa na pia nimeahidi kutengeneza barabara ya kuja eneo hili kwani tayari nimenunua greda kwa kutumia mkopo wa hela za gari la mbunge ili kuhakisha barabara zote zinapitika lakini yote haya yatawezekana tu tukishiriki nasi kuchangia nguvu zetu katika miradi”alisema Airo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri hiyo ya rorya Charles Ochere,aliwataka viongozi wa vijiji na kata kusoma mapato na matumizi kwa wananchi kwa kuwaeleza mchango unaotolewa na serikali kupitia halmashauri ili kuwawezesha wananchi kutambua kiasi cha fedha kinachotolewa katika miradi yao.
“Pia nawataka walimu wakuu na kamati za shule kutangaza kila fedha mnazopokea kwani mwaka jana tu kila shule ya msingi katika halmashauri yetu ambazo zinazofikia 117 ilipoteza milioni nane zilizoliwa kifisadi na mmoja wa maafisa wetu kwa kuzidanganya kamati na walimu wakuu lakini tunashangaa afisa huyo baada ya kufanya ufisadi huo mbaya na kukwamisha utekelezaji wa miradi ameamishiwa mkoa wa shinyanga na anaendelea na kazi”alisema Ochere.
Hata hivyo katibu wa ccm wa wilaya ya rorya Abubakary Ghati,alisema baada ya uchaguzi mkuu kumalizika ni vema wananchi wakajenga umoja kwa kuacha kubaguana kiitikadi,kikabila na kidini ili kuwezesha kushirikiana na kuharakisha maendeleo katika maeneo yao.

No comments:

Post a Comment