Tuesday, December 14, 2010

NYERERE AANZA KAZI KWA VITENDO JIMBO LA MUSOMA MJINI


MUSOMA

MBUNGE wa Jimbo la Musoma Mjini mkoani Mara, Vincent Nyerere (Chadema), ametoa msaada wa madishi mawili ya Televisheni pamoja na ving'amuzi vyake, kwa wafungwa na watuhumiwa waliopo katika Gereza la Musoma mkoani Mara  ikiwa ni zawadi yake wakati huu wa kuelekea kwenye Sikukuu ya Chrismas na mwaka mpya wa 2011

Vifaa hivyo vina uwezo wa kuonesha channeli 120 kutoka nchi mbali mbali na kuwa  msaada huo umelenga kuwawezesha wafungwa na watuhumiwa waliopo katika Gereza hilo kujifunza mambo mbali mbali yakiwemo ya Kilimo Kwanza, kumcha Mungu, Ufundi na shughuli za kujipatia mali kwa njia halali na wafungwa hao wanayo haki ya kuthaminiwa na kutambuliwa kama ilivyo kwa binadamu wengine.

Mbunge huyo wa jimbo laMusoma Mjini alikabidhi msaada kwa uongozi wa Gereza hilo akiwemo Mnadhimu wake hafla ambayo ilifanyika kwenye Bwaro la Magereza mjini Musoma hapa

Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo, Nyerere alisema msaada huo wa madishi ya Televisheni na ving'amuzi vyake ameutoa kama mchango wake wa upendo kwa watuhumiwa na wafungwa hao kwani watu hao wanayo haki ya kuthaminiwa ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kujifunza mambo mbali mbali ya uzalishaji mali na kumcha Mungu kwa kipindi chote walicho nacho Gerezani humo.

"Unapokuwa mfungwa si kwamba umepoteza haki zako zote hapana katika maisha yako  nchi yetu inahimiza masuala mengi yakiwemo ya Kilimo kwanza hivyo nimuhimu kupata vitu kama hivi ili mwende na dunia ya sasa” alisema mbunge huyo

Aidha kwa mujibu wa mbunge huyo wa jimbo la Musoma mjini msaada huo utawawezesha pia wafungwa na watuhumiwa wa gereza hilo la Musoma kusherehekea Sikukuu ya Krismasi inayosherehekewa kote duniani Desemba 25 kila mwaka, huku wakiwa wanapata elimu kupitia televisheni hivyo, ambavyo aliahidi kuweka kwa kila chumba cha gereza hilo pamoja na eneo la mahabusu.

Alisema yupo mbioni kuanzisha utaratibu wa kuwasomesha wafungwa wote wasiojua kusoma na kuandika katika gereza hilo la Musoma lengo ni kuwasaidia kielimu na hatimaye kujikwamua na lindi la umasikini miongoni mwao.
Musoma.

Mbali na kutoa madishi na ving’amuzi kwa wafungwa wa gereza la Musoma mbunge huyo ambaye hivi karibuni alileta kontena zima la vitabu jimboni humo alitangaza pia kutumia fedha za mshahara na posho zake kuwasomesha watoto 180 waliochaguliwa kujiunga na masomo ya Sekondari jimboni humo ambao wazazi wao hawana uwezo.

Nyerere  ambaye pia ni diwani wa Kata ya Mkendo, alisema kazi kubwa iliyopo mbele yake ni kuwatumikia wananchi wake wenye uwezo na masikini, na kwamba shabaha yake halisi ni kuona wananchi wa jimbo lake hilo wanaondokana na kero nyingi zilizokuwa zikiwatatiza kwa muda mrefu, na kuboresha sekta zote za elimu, afya, maji, barabara, viwanda na uchumi.

Kauli ya kuwasomesha watoto hao wanaotoka kwenye familia masikini aliitoa wakati akizungumza na wenyeviti wa mitaa na vitongoji wa jimbo hilo na kusema atatumia fedha zote za posho ya udiwani kuwasomesha wanafunzi hao 180 ikiwa ni pamoja na kuwalipia ada ya shule, michango na mambo mengine.

Mbunge huyo anayetoka katika ukoo wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alisema haoni sababu ya kushindwa kuwasomesha wanafunzi hao ambao wameshinda kwenda Sekondari lakini wazazi ama walezi wao hawana uwezo wa kuwagharimikia masomo hayo.

Katika mazungumzo hayo Nyerere aliwataka wenyeviti hao wa mitaa na vitongoji kubeba jukumu la kuwabaini watoto wa maeneo yao ambao wameshinda kwenda Sekondari mwaka huu lakini wazazi wao hawana uwezo na kwamba kazi hiyo ni vema ikatekelezwa na kila mwenyekiti ili kuwasaidia watoto hao kupata elimu na baadaye kulisaidia taifa.

Hata hivyo, mbunge huyo wa Musoma mjini, alitumia nafasi hiyo kulaani vikali kitendo cha uongozi wa CCM wilaya hiyo ambapo alidai kimewazuia wenyeviti wa mitaa na vitongoji wa chama hicho tawala kushirikiana na yeye (mbunge) katika suala zima la kimaendeleo jimboni humo.

Alisema uongozi wa CCM wilaya ya Musoma mjini, umewaagiza viongozi hao wa ngazi ya mitaa na vitongoji jimbo zima hilo wanaotokana na chama hicho cha CCM, kutompa ushirikiano katika utekelezaji wake wa majukumu ya maendeleo, ikiwa ni lengo la kutaka kumwangusha kisiasa jambo ambalo limepingwa vikali na jamii ya rika na kada zote mkoani Mara.

Katika hatua nyingine, mbunge huyo wa Musoma mjini aliwataka madiwani wa kata zote jimboni humo bila kujali itikadi za vyama kuhakikisha wanawajibika kikamilifu katika suala zima la usimamiaji na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo katika kata zao kwani kufanya hivyo itasaidia kuwaondolea kero nyingi wananchi.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment