Friday, October 29, 2010

NAHITAJI TANZANIA YA AMANI SI VITA

MUSOMA

MGOMBEA ubunge kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) Vincent Nyerere amesema kuwa haitaji kuwa mbunge katika jimbo ambalo limemwaga damu kwani ataopata wakati mgumu katika kuwatibu watu hao badala ya kutafuta maendeleo ya wananchi hao.

Kauli hiyo Vincent aliitoa hivi karibuni katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika mtaa wa Kibini kata Kigera manispaa ya Musoma mkoani Mara.

Alisema kuwa Tanzania ambayo Mwalimu Nyerere ameiacha ni ya amani na si vita kwani kwa kufanya hivyo itakuwa ni dhambi ambayo kamwe haitasameheka kwa mwasisi wa Taifa hili.
Nyerere alisema kuwa Tanzania itaendelea kuwepo hata baada ya uchaguzi mkuu kwani mambo ya kisiasa ni ya muda lakini maisha bado yanaendelea,aliongeza kuwa amani iliyopo Tanzania ni ya watanzania wote na si mtu Fulani.
  “Ndugu zangu Tanzania tunayohitaji ni Tanzania ya amani kwani sihitaji kuwa kiongozi katika Taifa ambalo limemwaga damu” alisema mgombea huyo

Katika  hatua hii ya mwisho ya kampeni mgombea huyo aliwaasa watanzania kuwa watulivu na kuhakikisha wanachagua viongozi ambao watawasaidia katika miaka mitano ijayo.

Nyerere aliongeza kuwa ingawa kuna watu kwa sasa ambao wamekuwa wakipita majimbani usiku kuwashawishi kwa fedha ili wawajachugue alisema kuwa hiyo ni dalili ya kushindwa hivyo wawapuuze kwani kiongozi anayepatikana kwa njia ya rushwa siku zote hafanyi kazi kwa maslahi ya jamii bali maslahi ya wafadhili wake.

Akiwa katika kata ya Nayakato hapo jana mgombea huyo alisema kuwa suala la barabara mbovu katika jimbo hilo si la kuuliza kwani hiyo ni ishara kuwa mbunge aliyemaliza muda wake hakuwathamini wananchi.

Alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano atakachokuwa mbunge wa jimbo la Musoma atajitahidi kufanikisha masuala nyeti ambayo yanaisumbua jamii   kwani kwa kufanya hivyo anaamini atakuwa  ameikomboa jamii ya Musoma.

   “Barabara zetu ni mbovu sana ingawa watu wanjisifu eti wamejenga barababara katika mji huu kitu ambacho sikweli,nahitaji kuona kila mwananchi wa Musoma anakuwa katika hali nzuri ya kimaisha na mazingira”alisema mgombea huyo

Mgombea huyo ambaye ni mmoja wa familia ya watoto wa  Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitano haitaji kuweka mabango ambayo yatakuwa yanamuonyesha kuwa yeye ni mgombea wa chama Fulani bali maendeleo atakayokuwa ameyafanya kwa miaka mitano katika jimbo la Musoma mjini ndio yawe kielelezo chake.


No comments:

Post a Comment