Wednesday, August 25, 2010

WATU 70 WANAHOFIWA KUFA MGODINI

Mwanza.

ZAIDI ya watu 70 ambao ni wachimbaji wadogo wa madini katika mgodi wa dhahabu wa Nyakagwe Wilayani Geita mkoani Mwanza, wanahofiwa kufa kwa kufukiwa na vifusi cha udongo vya maduara mgodini hapo, na tukio hilo linadaiwa kufichwa na viongozi.

Imeelezwa kuwa, maafa ya Watanzania hao yametokea Agosti 23 mwaka huu saa 3 usiku, baada ya kuibuka ugomvi mkubwa baina yao, wakati wakigombea kuchimba dhahabu kwenye mashimo 30 ya urefu wa mita 100 kwenda chini ya ardhi mgodini hapo.
 
Taarifa kutoka eneo la tukio zinasema kuwa, mbali na watu hao kufukiwa na maduara hayo, taarifa zaidi ya watu 20 walinusurika katika tukio hilo, baada ya kujiokoa wenyewe wakiwa hai kutoka chini ya mashimo hayo.

Mkuu wa wilaya hiyo ya Geita, Philemon Shelutete (DC), ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya hiyo, ameithibitishia Tanzania Daima kutitia kwa machimbo hayo ya dhahabu yaliyopo Kata ya Butobela wilayani humo.

"Ni kweli nami nimesikia, lakini mimi nimeambiwa kuna fujo tu na nimeshatuma maofisa wa Madini pamoja na polisi wapo huko", alisema Mkuu huyo wa wilaya ya Geita, Shelutete.
 
Kwa mujibu wa habari hizo kutoka kwa mashuhuda, zinasema kwamba, wachimbaji hao walipogundua kwamba maduara hayo yanatoa dhahabu kwa wingi waliingia wengi katika kila shimo, na ndipo ulipozuka ugomvi na kusababisha nguzo za maduara hizo kumeguka kisha kutitia.
 
“Mgodi huu umetitia Agosti 23 mwaka huu mida ya saa 3 hivi usiku, kulikuwa na zaidi ya wachimbaji 50 ambao hadi sasa hawajatoka ndani...lakini wengine 20 walijiokoa wenyewe kutoka chini", kilisema chanzo cha habari kutoka mgodini hapo.

Taarifa za uhakika zinasema, tayari Jeshi la polisi mkoani Mwanza, limetuma kikosi maalumu kwa ajili ya kwenda katika tukio hilo, na kwamba iwapo kuna ghasia kikosi hicho kiweze kutuliza mara moja.
 
Akizungumza  mmoja wa viongozi wa wachimbaji hao ambaye alikataa kutajwa jina lake, alisema ameshindwa kutoa taarifa kwenye vyombo vya dola kwa kuhofia usalama wao kutokana na shinikizo la baadhi ya viongozi wa Kiserikali wa eneo hilo, ambao unasadikiwa hautaki tukio hilo lifahamike.

“Siyo uongo ndugu yangu mwandishi, kuna wenzetu wengi wamefukiwa na tunahofua pengine wamekufa, ila tumeonywa tusitoe siri hii ili Serikali isiyafunge machimbo haya! Naomba sana usinitaje nitashughulikiwa", alisema mmoja wa viongozi wa wachimbaji hao.
 
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Charles Kazungu alipoulizwa kwa njia ya simu juu ya tukio hilo, alikiri maduara hayo kuporomoka, lakini akakanusha kuwa hakukuwa na mtu ndani yake.

Hata hivyo Ofisa Madini Mkazi wa wilaya ya Geita, Donard Mremi aliiambia Tanzania Daima jana jioni kwamba, yupo njiani anakwenda kwenye tukio hilo kwani kuna fujo imetokea.
 
“Ninapoongea nawe hivi nipo njiani nakwenda huko Nyakagwe, ni tukio tu la fujo ambalo tunakwenda kulitatua", alisema kwa mkato Ofisa huyo wa Madini.

Tukio hili ni mfululizo wa matukio ya namna hiyo ya kufukiwa wachimbaji katika maeneo ya migodi ya wachimbaji wadogo, ambapo mwaka jana wachimbaji 7 walifukiwa na kufa katika mgodi wa dhahabu wa Nyarugusu wilayani Geita.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment