DC HANDENI APIGA KAMBI MSITUNI KUNUSURU MITI YA UWOTO WA ASLI
Na Mohammed Mhina, Handeni
HANDENI JUMATANO JULAI 11, 2012. Mkuu wa wilaya ya Handeni mkoani
Tanga Bw. Muhingo Rweyemamu, amepiga kambi kwenye mwambao wa misitu ya
Kang'ata wilayani humo kukagua na kuona athari za uvamizi na ukataji
miti ya uoto wa asili unaofanywa na wananchi kwa kisingizio cha
kusafisha mashamba kwa ajili ya kilimo.
Akiwa katika msitu huo, Mkuu huyo wa wilaya ya Handeni ameshuhudia
uharibifu mkubwa uliotokana na uvamizi na ukataji wa miti ya asili
katika misitu tengefu ya Kang'ata msitu ambayo ilikuwa ikihifadhi idadi
kubwa ya makundi ya nyuki na kuvuta kiasi kikubwa cha mvua.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu akizungumza kwa mara ya kwanza na baadhi ya wakuu wa Idara ya Wilaya hiyo.
Kutokana na uharibifu huo mkubwa wa ukataji wa miti katika misitu
hiyo, Bw. Muhingo amepiga marufuku utoaji wa vibali vya uvunaji wa miti
ya mkaa na mbao hadi hapo kamati maalumu itakapoweka utaratimu mpya wa
utoaji wa vibali vya uvunaji wa miti wilayani humo.
Akizungumzia uvamizi na uhalibifu huo wa uoto wa asili, Bw. Muhingo
amesema kuanzia sasa mtu yeyote atakayeomba kibali cha kuvuna miti kwa
ajili ya kupasua mbao ama mkaa ni lazima akaonyeshe shamba lake la miti
kabla ya kufikiriwa kupata kibali.
Amesema hata baada ya kupata kibali hicho, mwombaji ambaye ni
mwenyeshamba ni lazima ukaguzi ufanywe katika shamba la mhusika ili
kujiridhisha kama kibali alichopewa amekitumia kwa kuvuna miti iliyopo
katika shamba husika na ndipo apatiwe kibali kingine kwa ajili ya
kusafirisha mazao hayo kutoka msituni hadi katika eneo la soko.
Bw. Muhingo amesema wilaya ya Handeni ambayo ina maeneo mengi ya
misitu ya uwoto wa asili, hivi sasa iko hatarini kugeuka jangwa kama
juhudi za makusudi za kukabiliana sasa na wavamizi wa misitu hiyo na
kuikata hazitachukuliwa mapemba.
Amewataka viongozi wa Serikali za Vijiji na wananchi wenye maeneo
makubwa ya ardhi, kuacha kuyauza maeneo hayo kwa wageni wanaodai
wanataka maeneo kwa ajili ya kilimo kwani hata baada ya kupatiwa maeneo
hayo wageni hao hukata mikaa na mbao akijifanya wanasafisha maeneo kwa
ajili ya kilimo.
Akiwa katika harakazi za kuinusuru misitu wilayani handeni, Mkuu
huyo wa wilaya, hivi karibuni alimkamata mmoja wa watumishi wa Idara ya
Misitu akisafirisha kiasi kikubwa cha magogo yaliyovunwa bila ya kibali
jambo lililopelekea kusimamishwa kazi kwa afisa huyo wilayani handeni.
Aidha Bw. Muhingo amewataka watumishi wote wa Idara ya Maliasili na
Misitu wilayani humo kuwa waaminifu na waadilifu na kwamba kazi
waliyonayo ni dhamana ya Watanzania wote na kwamba wao hawana mamlaka wa
kutumia rasilimali hizo kwa kujinufaisha wenyewe na familia zao.
No comments:
Post a Comment