Thursday, May 24, 2012

Na Mohammed Mhina, Handeni
HANDENI, ALHAMISI MEI 24, 2012. WANANCHI wa Kata ya Misima wilaya ya Handeni mkoani Tanga, wamewalalamikia viongozi wa vijiji vya Kibaya na Misima kwa kujihusisha na uuzaji wa ardhi ya yakiwemo maeneo ya mashamba ya umma yanayomilikiwa na vijiji na umoja wa vijana pasipo ridhaa ya wananchi wa vijiji husika.
Wakizungumza na Mwandishi wa Habari hizi kijijini hapo, Bw. Rashidi Changoma na Bw. Yahaya Lubwililili, wamesema kuwa kutokana na kuuzwa kwa maeneo ya vijiji katika kata ya Misima wilayani humo, kuna hatari ya vizazi vijavyo vikawa watumwa wa wahamiaji kutoka mikoa mingine.
Bw. Changoma amesema viongozi wa vijiji vya Kibaya na Misima wamethubutu kuuza mpaka mashamba ya ujamaa nay a vijana yanayomilikiwa kwa pamoja na vijiji vya Misima na Kibaya katika kata hiyo.
Amesema mashamba yaliyouzwa ni ya Lengomi lenye zaidi ya ekari 80 na lile lililopo kati ya Misiama na Mzeri na lile la vijana linalopakana na Mzee Saasha Mbega Komgambo hayo hivi sasa yanamilikiwa na wahamiaji wafugaji kutoka mkoa wa Arusha kinyume na malengo ya mstumizi ya ardhi hiyo yenye jumla ya ekari zaidi ya 72.
Na kwa upande wake Bw. Lubwilili amesema kuwa maeneo yaliyouzwa ni pamoja na yale yanayotumiwa na Jeshi la Kujenga Taifa katika kufanyia mazoezi ya kijeshi ya mbuga iliyopo kati ya vijiji vya Mbagwi na Mzeri.
Wananchi hao wamemuomba Mkuu mpya wa wilaya ya Handeni Bw. Muhingo Rweyemamu, kuwa mara atakapoanza kazi wilayani humo ashughulikie masuala ya ardhi ili kuepusha migogoro inayoweza kuzuka katika siku za usoni baina ya wakulima na wafugaji ama vijana kukosa maeneo ya kujiajili.
Kwa upande wake vingozi wa vijiji vya Misima na Kibaya wilayani humo, wamesema kuwa baadhi ya wahamiaji hao wameuziwa maeneo na wenyeji lakini baadhi yao wamejipachika wenyewe katika maeneo tengefu wakidai wameuziwa na serikali ya kijiji cha Misima na Kibaya.
Afisa Mtendaji wa kijiji cha Misima Bw. Omari Athumani Waziri na Bw. Khalidi Machokolo wa kijiji cha Kibaya katika kata hiyo ya Misima, wamesema wao kama viongozi wamepanga kufanya mkutano wa pamoja ili kujadili masuala ya uuzaji holela wa ardhi katika kata hiyo.
Pamoja na vijiji vya Misima na Kibaya, maeneo mengine yanayokabiliwa na migogoro ya ardhi siku za usoni ni katika vijiji vya Mzeri,Mbagwi vya kata ya Misima na kitongoji cha Bwawani kilichopo katika kijiji cha Sindeni wilayani Handeni.
Mwisho

No comments:

Post a Comment