Saturday, August 6, 2011

DAWA ZA KULEVYA ZAKAMATWA ZANZIBAR

Na Mwandishi wa Jeshi la Polisi -Zanzibar


Makachero wa Jeshi la Polisi Zanzibar kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama vilivyopo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar, wamefanikiwa kumtia nguvuni mkazi mmoja wa Sinza Jijini Dar es Salaam akiwa na kiasi kikubwa cha dawa za kulevya aina ya Cocaine.


Afisa Uhusiano wa Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina, amesema kuwa mtuhumiwa huyo Honest Kyara Abraham(30), amekamatwa juzi kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa zanzibar akitokea Sao Paulo nchini Brazil kwa ndege ya shirika la Oman.

Akizungumzia tulio hilo, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Kamishna Msaidizi wa Polisi Muhudi Mshihiri, amesema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa na jumla ya pipi 93 za dawa hizo tumboni mwake.

Amesema kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kunatokana na uhakika wa taarifa za kiitelijensia zilizokuwa zikifanywa na Makachero wa Jeshi la Polisi hapa nchini ambao walikuwa wakifuatilia nyendo za mtuhumiwa huyo tangu alipoondoka hapa nchini Julai 3, mwaka huu na hadi kurudi.

Mtuhumiwa huyo aliondokea kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwl Nyerere Jijini Dar es Salaa, akitumia hati ya kusafiria yenye namba AB 349553 iliyotolewa Septemba 23, 2009 Jijini Dar es Salaam.

Kamanda Mshihiiri amesema kuwa, mara baada ya kuwasili kwa ndege hiyo na kumkamata mtuhumiwa Abdaham ambaye ni mkazi wa Sinza Jijini Dar es Salaam, alihojiwa na ndipo alipofikishwa kwenye Hospitali Kuu ya Mnazimmoja Zanzibar kufanyiwa uchunguzi na kubainika kuwepo kwa vitu visivyo vya kawaida tumboni mwake.

Amesema pamoja na kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa miongoni mwa kundi kubwa la abiria, waliosafiri pamoja katika ndege hiyo, lakini aligundulika kutokana na kukua kwa mtandao wa Polisi katika upashanaji wa habari za wahalifu katika nchi mbalimbali.

Amesema alipohojiwa mtuhumiwa huyo alionyesha ushirikiano na kukiri kumeza dawa hizo tumboni mwake na hivyo kuwekwa chini ya ulinzi na ndipo alipoanza kuzitoa dawa hizo kwa njia ya haja kubwa dawa ambazo zilifungwa kwa mfumo wa pipi.

Huyo ni Mtazania wa tatu kukamatwa na Polisi kwa kupatikana na dawa za kulevya aina ya Cocaine kwenye Uwanja huo huo wa zanzibar akitokea Sao Paulo nchini Brazil ambapo watu wengine wawili walikamatwa kwa nyakati tofauti mwanzoni na katikati mwa mwezi Jualai mwaka huu wakiwa na dawa za kulevya pia aina ya Cocaine.

Watuhumiwa wengine ni Kasim Abdallah Ali(44), mkazi wa Magomeni Mapipa Jijini Dar es Salaam ambaye alikamatwa Julai 5, mwaka huu akiwa amemeza pipi 96 za dawa hizo na Bathoromeo Tutubet Nditi(33) naye mkazi wa magomeni Mapipa Jijini Dar es Salaam aliyekamatwa Julai 12, mwaka huu.

Kamanda Mshihiri amesema kuwa watuhumiwa wote hao walikuwa wakisafiri kwa ndege ya Shiirika la Oman ziliyokuwa ikizotokea Sao Paulo nchini Brazil.

Amesema kuwa kutokana na utafiti uliofanywa na Jeshi la Polisi, umebaini kuwa watuhumiwa wengi wa dawa za kulevya wanapanga kushukia kwenye uwanja wa ndege wa Zanzibar kwa kuthani kuwa wangeweza kufanikiwa kuvuka ili kusafiri kwa boti hadi Dar es Salaam.

Kamanda Mshihiri amesema kuwa hivi sasa hali ya uwanja wa ngege wa Zanzibar umeimarishwa kwa kushirikiana na vyombo vyote vya ulinzi na usalama vilivyopo uwanjani hapo.

Amesema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani Jumanne kujibu tuhuma zinazomkabil

No comments:

Post a Comment