Daniel Mjema, Dodoma na Editha Majura, Dar
KITENDO cha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kushindwa kuzungumzia shinikizo la baadhi ya wabunge kutaka mawaziri wanane wajiuzulu, kimeonekana kuwakera wawakilishi hao ambao sasa wameamua kuibana Serikali huku wakiapa kukwamisha bajeti za mawaziri hao katika Bunge lijalo la Bajeti.
Jana
walianza kuonyesha makali baada ya kukataa mapendekezo ya Mfumo wa
Mpango wa Mabadiliko wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2012/2013 wakisema
hauna jipya na umetayarishwa kwa mfumo uleule kwa miaka 15 mfululizo.
Juzi, Pinda aliahirisha Bunge bila kugusia shinikizo la wabunge hao kutaka Serikali iwawajibishe Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo; Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja; Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu; Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami; Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe; Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), George Mkuchika.
Wakizungumza
na kwa nyakati tofauti jana, wabunge hao, wengi wao wakiwa ni wa CCM,
walisema silaha pekee waliyobaki nayo ni kukwamisha Bajeti ya Serikali
kwa mwaka 2012/2013 katika kikao kijacho cha Bunge.
Wabunge
hao pia wameonya kwamba kutojiuzulu kwa mawaziri hao kutaiweka CCM njia
panda katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwani hoja ya ufisadi ndiyo
iliyowafanya wenzao wengi wasirudi bungeni.
“Silaha
kubwa tuliyobaki nayo sasa ni kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu
na nakuambia kama ile karatasi ingerudi upya leo idadi ya wabunge wa CCM
ambao wangetia saini ingetikisa nchi,” alisema James Lembeli wa Kahama
(CCM).
Lembeli
alisema anashangaa kuona mawaziri waliotakiwa kujipima wenyewe na
kuandika barua za kujiuzulu wakigoma kufanya hivyo na Serikali kupuuza
hoja hiyo akisema, hatashangaa kuona Watanzania wakiingia mitaani.
“Kitendo
cha Waziri Mkuu kutosema chochote kuhusu kujiuzulu kwa mawaziri hao
wakati akihitimisha Bunge ni kuiingiza nchi kwenye mgogoro mkubwa.
Serikali ifahamu kuwa, ipo madarakani kwa ridhaa ya wananchi,” alisema.
Lembeli
alisema wananchi walipokea kwa shangwe taarifa ya mawaziri hao kutakiwa
kujiuzulu lakini, kitendo cha Waziri Mkuu kuwaacha na kuikwepa hoja
hiyo alipokuwa akiahirisha Mkutano wa Bunge juzi, kitaongeza chuki ya
wananchi dhidi ya Serikali yao kwa kuwa wataamini inawakumbatia
mafisadi.
“Inakuwaje
hawa mawaziri wanane tu watake kuitumbukiza nchi kwenye machafuko?
Uwaziri ni dhamana aangalie huko kwenye vijiwe na mitaani watu
walivyoshangilia kusikia wametakiwa kujiuzulu leo wanagoma, unamgomea
nani?” alihoji Lembeli.
Lembeli
alisema anaamini Rais atafanya uamuzi mgumu na wa haraka kabla ya Bunge
la Bajeti vinginevyo Waziri Mkulo na mawaziri wengine watakuwa na
wakati mgumu ambao haujawahi kuonekana katika kupitisha bajeti za wizara
zao.
Mbunge mmoja wa Viti Maalumu kwa tiketi ya CCM kutoka Kanda ya Ziwa, alisema ukimya wa Rais Kikwete na kiburi cha mawaziri wake wenye tuhuma za kweli kugoma kujiuzulu, kumezidi kukifanya chama hicho tawala kuporomoka umaarufu.
Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), alisema Rais Kikwete anapaswa kuheshimu maoni na maelekezo ya wabunge na kusema hata kutaka mawaziri wajiuzulu ni utaratibu tu wa kistaarabu.
Mbunge mmoja wa Viti Maalumu kwa tiketi ya CCM kutoka Kanda ya Ziwa, alisema ukimya wa Rais Kikwete na kiburi cha mawaziri wake wenye tuhuma za kweli kugoma kujiuzulu, kumezidi kukifanya chama hicho tawala kuporomoka umaarufu.
Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), alisema Rais Kikwete anapaswa kuheshimu maoni na maelekezo ya wabunge na kusema hata kutaka mawaziri wajiuzulu ni utaratibu tu wa kistaarabu.
“Sisi Wabunge 76 tuliosaini hoja ya kutaka Waziri Mkuu ang’oke tumejitoa sadaka kwa maslahi ya nchi lakini naamini wakati wa kumpigia kura Waziri Mkuu, wengi zaidi watatuunga mkono kwa jinsi walivyokerwa na jambo hili,” alisema.
“Bunge
safari hii limeisha kimyakimya, Spika alipowahoji wanaoafiki hoja ya
Waziri Mkuu ya kuliahirisha Bunge waliosema siyo ndiyo waliokuwa wengi
na kama ulifuatilia Bunge lilikuwa kimya si kawaida… Rais anatakiwa
alione hilo,” alisema.
Mbunge
wa Kinondoni, Iddi Azzan (CCM), alisema amesikitishwa na hatua ya
mawaziri hao kugoma kujiuzulu na kwamba kwa hali ilivyo, busara ya
kawaida inataka mawaziri hao wajiuzulu.
“Kwa
busara ya kawaida wote wanaotuhumiwa kwa wizara zao kufanya madudu
wangeacha uroho wa madaraka na kujiuzulu ili kuitikia kilio cha wabunge
na Watanzania kwa sababu upepo huko nje sio mzuri hata kidogo,” alisema
Azzan.
Mbunge
wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM) alisema taifa limeghafilika kwa sababu
wananchi wengi nchi nzima walikaa kwenye luninga na kusikiliza redio
juzi jioni wakitarajia Waziri Mkuu angetamka moja kwa moja kuwang’oa
mawaziri hao.
Nape, Mukama
Baadhi ya wabunge wa CCM waliosaini barua ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu wamedai kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho Wilson Mukama amewatisha.
Kanji Lugola wa Mwibara alidai jana kwamba usiku wa kuamkia Jumapili, siku moja baada ya kusaini hati hiyo alipokea simu kutoka kwa Mukama akimtolea maneno makali kutokana na hatua yake hiyo.
“Alizungumza maneno mengi ya vitisho kwa mfululizo bila hata kunipa nafasi ya kujieleza, akasema, ‘nakuja huko wewe na huyo mwenzako mliosaini mtanitambua,’ kuona hivyo tukaondoka Dodoma usiku huohuo,” Lugola alieleza.
Alisema walisafiri hadi Dar es Salaam na kwamba walihudhuria kikao cha Bunge cha Jumatatu iliyopita wakitokea mafichoni.Alipotakiwa kuthibitisha madai hayo Mukama alisema: “Siwezi kutoa habari kwa simu.”
Alipopigiwa tena na kuombwa afuatwe ofisini alisema, “Kwa leo haitawezekana maana niko njiani natokea Dodoma sasa hivi nimefika Gairo, kama unaweza njoo kesho.”
Lugola alidai wakati akipokea vitisho hivyo kutoka kwa Mukama waliokuwa wamesaini kwa upande wa CCM walikuwa yeye na Filikunjombe, baadaye alifuatia na Nimrod Mkono.
No comments:
Post a Comment