JOHN MNYIKA ATEMA CHECHE KWA PINDA.
Katibu
Mwenezi wa Chama cha Demakrasia na Maendeleo Mh. John Mnyika amesema
leo mjini Dodoma kuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda anapaswa kuagiza timu
ya wataalamu aliyoiunda kufuatia mkutano wake wadau wa viwanda vya nguo
kufanya uchunguzi maalum kuhusu kiwanda cha nguo cha Urafiki.
Mnyika
amesema kuwa ukaguzi huo wa Timu ya Wataalamu kwa maagizo ya Waziri
Mkuu Pinda utachangia katika kunusuru Kiwanda cha Nguo cha Urafiki dhidi
ya udhaifu wa kiutendaji, ufisadi dhidi ya mali za kampuni, kulinda
maslahi ya wafanyakazi na kushughulikia kasoro katika mchakato wa
ubinafsishaji.
Katika hotuba yake ya kuahirisha bunge tarehe 23 Aprili 2012 Waziri
Mkuu Pinda alieleza taifa kuwa kufuatia mkutano wake na wadau wa tarehe
23 Machi 2012 ameunda kamati ya wataalamu ya kuangalia changamoto
zinazokabili viwanda vya nguo nchini ili kuviwezesha kuchangia kwenye
mapato ya nchi na katika kuongeza ajira.
Hatahivyo Mnyika amesema ni muhimu Waziri Mkuu Pinda na timu ya
wataalamu hao wakazingatia kuwa matatizo ya kiwanda cha urafiki ni zaidi
ya changamoto za kawaida kwa kuwa ni matokeo ya kasoro katika mchakato
mzima wa ubinafsishaji, udhaifu wa kiutendaji wa miaka mingi pamoja na
ufisadi uliokithiri unaohitaji uchunguzi maalum.
Kutokana na hali hiyo Mnyika ametoa wito kwa Serikali kuingilia kati
kupitia Wizara ya Fedha hususani Ofisi ya Msajili wa Hazina na Shirika
Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) na Wizara ya Viwanda na
Biashara kuchukua hatua zinazostahili juu ya kiwanda cha Urafiki.
Aidha,
kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara kuchukua hatua za
kuisimamia serikali ili kuharakisha hatua za kunusuru kiwanda hiki ili
kuonyesha pia mfano wa hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuhusu viwanda
vingine. Hata hivyo mpaka sasa hakuna hatua kamili zilizochukuliwa na
Wizara na Mamlaka husika hivyo Waziri Mkuu Pinda anapaswa kuingilia kati
kusukuma hatua kuchukuliwa baadala ya kutoa kauli za ujumla kwamba
serikali inalinda viwanda vya ndani.
No comments:
Post a Comment