Bastola ya Kanumba yasakwa,baada ya Wiki mbili ya kifo
Bastola ambayo inadaiwa ilikuwa ikitumiwa kihalali na staa wa filamu barani Afrika, Steven Charles Kanumba, inasakwa na Jeshi la Polisi Tanzania.Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi, Kinondoni, Dar es Salaam, ACP Charles Kenyela amesema kuwa anafuatilia kumbukumbu za silaha hiyo, kwani haijarejeshwa kwenye jeshi lake.
Kenyela alisema juzi kuwa anafuatilia juu ya umiliki huo na baada ya hapo, jeshi la polisi litawahoji ndugu wa msanii huyo kuhusu kurejesha bastola hiyo jeshini.
“Bastola ni mali ya serikali. Kuna hatua ambazo hufuata mpaka mtu aruhusiwe kumiliki bastola,” alisema Kenyela na kuongeza:“Endapo mmiliki halali wa silaha hiyo atafariki dunia, ndugu zake lazima waikabidhi kwa jeshi la polisi na baada ya hapo, kama kuna ndugu anataka aimiliki tena, inabidi afanye maombi upya na atakapokidhi vigezo ndiyo ataruhusiwa.
“Kutokana na hali hiyo, bastola ya Kanumba lazima irudi kwetu haraka na kama kuna ndugu yake yeyote anataka kuimiliki, itabidi awasilishe maombi.”
Kenyela aliongeza kuwa hivi sasa anafuatilia kumbukumbu za jeshi la polisi ili awe na uhakika kama kweli msanii huyo alikuwa anamiliki silaha hiyo.
“Tukithibitisha tutawahoji ndugu zake pamoja na wengine wanaohusika ili tuwe na taarifa za hiyo silaha. Ila kwa sasa tunafanyia kazi taarifa hizi kwa kupitia kumbukumbu za jeshi,” alisema.
Kenyela alitoa ufafanuzi huo baada ya kuulizwa na mwandishi wetu kama jeshi lake limeshapokea bastola ambayo alikuwa anaitumia Kanumba enzi za uhai wake.
NDUGU WANASEMAJE?
Mama mzazi wa Kanumba, Flora Mtegoa, alipoulizwa na paparazi wetu kuhusu bastola inayodaiwa kutumiwa na mwanaye alipokuwa hai, alikuwa na haya ya kujibu:
“Sijaiona hiyo bastola humu ndani tangu nimefika hapa. Sijui ipo wapi na sijui kama kweli Kanumba alikuwa anamiliki hiyo silaha.
“Najua sheria za silaha hiyo, kwa hiyo ingekuwepo ningeiwasilisha polisi haraka. Baba yangu alikuwa na silaha hiyo, alipofariki dunia tuliikabidhi kwa jeshi la polisi.”
NANI ANAJUA ILIPO?
Taarifa zinaonesha kuwa mdogo wa Kanumba, Seth Bosco alikuwa karibu zaidi na marehemu lakini kwa sababu umiliki wa silaha hiyo ni siri, siyo rahisi kujua ilipo.
Mtu mwingine ambaye alikuwa karibu na marehemu mpaka nyakati za mwisho za uhai wake, kama ripoti zinavyoonesha ni muigizaji Elizabeth Michael ‘Lulu’ (pichani), ingawa naye inawezekana hajui kutokana na unyeti wa silaha yenyewe.
BASTOLA NA KANUMBA
Akiwa hai, Kanumba aliwahi kuripotiwa mara kadhaa kumiliki silaha hiyo, japo haikufafanuliwa kama ni kihalali au batili.
Kanumba aliripotiwa kwa mara ya kwanza kumiliki bastola miaka minne iliyopita, akidaiwa kuichomoa baada ya kuvamiwa na kundi la watu aliohisi wanataka kumteka.
Licha ya stori hiyo kuandikwa gazetini na nyingine ambazo zilimhusisha na umiliki wa bastola, bado Kanumba hakuwahi kufafanua chochote kuhusu silaha hiyo.
IPO WAPI?
Je, aliiacha sehemu ambayo hakuna mtu anayeweza kupafikia?
Aliirejesha kabla mauti hayajamkuta ndiyo maana haionekani?
Je, Kuna mtu aliiwahi baada ya kifo chake kwa kuona ni dili?
Kanumba alifariki dunia Aprili 7 na kuzikwa Aprili 10, 2012 kwenye Makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment