POLISI ZANZIBAR WAMTIA MBARONI MWIZI WA KICHANGA
Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi Zanzibar
ZANZIBAR
JUMATATU APRILI 16, 2012. Jeshi la Polisi Zanzibar linamshikilia
mwanamke mmoja mkazi wa Tomondo mjini Zanzibar kwa tuhuma za kuiba mtoto
mchanga mwenye umri wa miezi mitano kutoka katika Hospitali Kuu ya
Mnazimmoja mjini Zanzibar .
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar Kamishna Msaidizi Aziz Juma
Mohammed, amemtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Fatma Abdallah Mohammed(26),
ambaye alikamatiwa Bandarini akisafiri na mtoto huyo kwenda Pemba .
Kamanda
Aziz amesema kuwa mtoto huyo aitwaye Aisha Nassor Ali, aliibwa Aprili
10, mwaka huu majira ya saa tano asubuhi wakati mama wa mtoto huyo Bi. Rahma Hassan Ali, alipompeleka mtoto wake kupata matibabu katika Hospitali ya Kuu ya Mnazimmoja mjini Zanzibar .
Amesema
wakati mama wa mtoto huyo akiwa katika foleni ndefu ya kutaka kupata
kadi ya kumuona daktari, alitokea mwanamke mwingine ambaye sasa ni
mtuhumiwa, akijifanya kuwa ni mwandishi wa Habari na alikuwa akifuatilia
kezo za tiba katika Hospitali hiyo, lakini pia alikuwa akifahamiana na
mmoja wa madaktari na hivyo kumtaka ampe msaada ili mtoto huyo aweze
kupatiwa tiba kwa haraka.
Amesema
mtuhumiwa huyo aliongea na simu na kujifanya kuwa alikuwa akionge na
daktari na bwamba amemtaka apelekwe mtoto huyo kwake kwa matibabu na
ndipo mtuhumiwa huyo alipomwambia mama wa mtoto kuwa ampatie mtoto ili
atangulie naye kwa daktari na kumtaka mama wa mtoto akatafute daftari la
kuandikia matibabu ya mtoto wake.
Kamanda
Aziz amesema mtuhumiwa huyo alimchukua mtoto huyo na kupanda ghorofani
kwa daktari lakini baada ya mama wa mtoto huyo alipopata daftari na
kumfuatilia mtuhumiwa huyo hakuweza kumpata na ndipo alipotoa taarifa
Kituo cha Polisi Malindi na juhudi za kipolisi za kumtafuta mtuhumiwa
pamoja na mtoto zilianza.
Amesema
hadi kufikia jana asubuhi Polisi wa kike Konstebo Jaala Juma Makame ,
wa Kikosi cha Polisi Wanamaji na Bandari Zanzibar , alimtia nguvuni
mtuhumiwa huyo akiwa pamoja na kichanga hicho na baada ya kuwasiliana na
viongozi wake Bandarini hapo, Wazazi wa kichanga hicho waliitwa na
walipofika walimtambua mtoto wao.
Aidha
mama wa mtoto pia alimtambua mtuhumiwa kuwa ndiye aliyejifanya kuwa ni
mwandishi wa Habari na kumkabidhi mtoto wake siku ya tukio ili amsaidie
kwenda kwa daktari kupatatiwa matibabu.
Kufuatia
kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta
Jenerali Saidi Mwema, ametoa cheti cha sifa na tuzo ya shilingi 200,000
kwa Konstebo Jaala Juma Makame, kutokana na juhudi na utambuzi wake wa haraka wa kumpata mtuhumiwa ingawa siku hiyo kulikuwa na wanawake wengi waliokuwa wakisafiri na watoto wenye umri tofauti.
Akikabidhi
cheti hicho cha heshma na tuzo ya fedha kwa Konstebo Jaala, kwa niaba
ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Mussa
Ali Mussa, alisema kuwa Jeshi la Polisi hap nchini litaendelea
kuwazawadia askari wote watakaofanya kazi zao kwa ubunifu na kufuata
misingi ya sheria na haki, lakini pia kuwaadhibu na hata kuwafukuza kazi
wengine watakaobainika kwenda kinyume na maadili ya Jeshi hilo.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mh. Abdallah Mwinyi, amempatia Askari
huyo mwanamke shilingi 50,000 kama motisha kwa juhudi alizofanya hadi
kufanikisha kumkamata mtuhumiwa huyo akiwa pamoja na mtoto.
Mwisho
No comments:
Post a Comment