Tuesday, April 17, 2012

              APIGWA HADI KUFA KWA WIZI WA KUKU KIGOMA

Na Pardon Bwate na Felister Elias , wa Jeshi la Polisi Kigoma

KIGOMA JUMANNE APRILI 17, 2012. Mkazi mmoja wa Kijiji cha Kagongwa mkoani Kigoma Patroba Christopher(25), ameuawa kwa kupigwa mawe na marungu na kundi la watu wenye hasira baada ya kukurupushwa akiiba kuku kijijini hapo.

Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma Kamishna Msaidi Frasser Kashai, amesema kuwa juzi majira ya saa 9.00 usiku, marehemu alienda nyumbani kwa Bi. Hawa Ahmed na kuingia kwenye banda la kufugia kuku ambapo aliiba kuku watano wenye thamani ya shilingi 50,000.

Kamanda Kashai amesema kuwa, wakati marehemu akitoka kutoka kwenye banda hilo Bi. Hawa alisikia kuku wakilia na kishindo cha mtu anayekimbia ambao kuku waliendelea kusikika wakilia akitokomea nao na ndipo alipopiga kelele za mwizi na watu walijitokeza kwa wingi na kuanza kumfukuza marehemu huku wakimshambulia kwa mawe na marungu hadi kufariki dunia.

Katika tukio lingine wakazi wawili wa kijiji cha Kibande wilaya ya Kasulu mkoani humo, Zegeli Shumba (60) na mkewe Bi. Helena Zengeli(58), waliuawa na kundi la watu wenye hasira kwa kupigwa mawe na miili yao kuchomwa moto kutokana na imani za kishirikina.

Kamanda Kashai amesema siku ya tukio hilo juzi majira ya saa 2.00 usiku kundi la wananchi wa kijiji hicho waliwavamia marehemu hao kwa kuwashambulia hadi kuwaua baada ya kutuhumiwa kuwa walikuwa wakijihusisha na vitendo vya kichawi.

Amesema kuwa hivi karibuni kulikua na binti mmoja kijiji hapo (hakumtaja jina) ambaye alipotea kwa njia za kutatanisha na marehemu hao walidai kuwa wangefanya maarifa ya kiganga kumrejesha lakini hadi wanauawa walikuwa hawajamrejesha jambo lililoibua hasira kwa wakazi hao.

Amesema watu saba wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za mauaji hayo na uchunguzi wa tukio hilo umeanza.

Na huko wilayani Kibondo mmiliki mmoja wa kilinge cha pombe haramu ya gongo anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kumuua mteja wake ambaye alikuwa mlinzi wa Soko la halmashauri ya mji wa kibondo Bw. Hamisi Jambigwa (56).

Kamanda Kashai amesema kuwa siku ya tuki marehemu Jambigwa ambaye alikua na fedha zake za mshahara alitoroka lindoni majira ya saa 3.30 usiku na kwenda nyumbani kwa mtuhumiwa Johnson Godfrey (37), ili kujipatia kinywaji hicho haramu kinyemela.

Amesema akiwa kilabuni hapo marehemu alitoa bulingutu la fedha na kuchomoa noti moja kulipia kilaji hicho na ndipo mtuhumiwa alipoanza ugonvi wa kutaka kumnyang’anya marehemu fedha zake lakini alishindwa na ndipo marehemu alipoondoka kurejea kazini kwake kuendelea na ulindi sokoni hapo.

Lakini ilipofika nyakati za usiku mtuhumiwa alikwenda kazi kwa marehemu na kumvamia kisha kumkata shingo hadi kufa na baadaye kuuburuza mwili wake hadi kwenye pagale la nyumba na kuutelekeza hapo baada ya kuchukua fedha alizokuwa nazo marehemu.

Kamanda Kashai amesema baada ya taarifa za mauaji hayo kufika Polisi, Makachero walianza uchunguzi na ndipo walipofika nyumbani kwa mtuhumiwa kwa kumtilia shaka kuhusika na mauaji hayo.

Amesema makachero hao walipoanza upekuzi chumbani kwa mtuhumiwa  waliona panga na kisu vikiwa vimetapakaa damu hali hakukua na mnyama yetote aliyechinjwa hapo nyumbani kwa mtuhumiwa.

Kamanda huyo amesema hadi sasa jumla ya watu wanane wanashikiliwa na Polisi kuhusiana na tuhuma za mauaji ya watu hao.

Imehaririwa na kusambazwa kwenu na Insp. Mohammed Mhina, Afisa Habari Mkuu wa Jeshi la Polisi Zanzibar .

No comments:

Post a Comment