HOTUBA YA MKUU WA MKOA WA MARA BWANA JOHN TUPPA WAKATI
WA KUFUNGUA MKUTANO WA WADAU WA MFUKO WA TAIFA WA BIMA YA AFYA (NHIF)
ULIOFANYIKA MKOANI MARA TAREHE 13 APRILI 2012
·
Katibu Tawala wa Mkoa
wa Mara
·
Wakuu wa Wilaya zote
za Mara
·
Wajumbe wa Bodi ya Mfuko
wa Taifa wa Bima ya Afya
·
Mstahiki Meya wa Manispaa
ya Musoma
·
Mkurugenzi wa Manispaa
na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri
·
Waheshimiwa Wabunge
·
Mwakilishi toka Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii
·
Mwakilishi wa
Mkurugenzi Mkuu Bohari ya Dawa
·
Mganga Mkuu wa Mkoa
wa Mara
·
Waheshimiwa Madiwani
·
Wakurugenzi, Mameneja
na Maofisa wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
·
Wenyeviti wa Bodi za
Afya za Halmashauri
·
Waratibu Mfuko wa
Mfuko wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya na Mfuko wa Afya ya Jamii
·
Ndugu zangu Waandishi
wa Habari
·
Wageni waalikwa
(itifaki imezingatiwa)
Mabibi na Mabwana, Asalamu Aleikum, Bwana Asifiwe.
1.
SHUKRANI
Waheshimiwa Viongozi na washiriki wa mkutano huu, Awali ya yote napenda niwashukuru
viongozi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa kunialika kuwa mgeni rasmi katika
mkutano huu muhimu. Kama mwenyeji wa mkoa huu napenda kuwakaribisha sana Mkoani Mara.
Pia napenda kuupongeza Mfuko wa Taifa
wa Bima ya Afya kwa kuadhimisha miaka 10 tangu ulipoanzishwa. Tuliona kupitia
vyombo vya habari namna Waziri Mkuu Mizengo Pinda alivyosisitiza umuhimu wa
huduma kwa wanachama na usimamizi wa Fedha zitokanazo na NHIF na Mfuko wa Afya
wa Jamii (CHF) ili zilingane na ubora wa huduma inayotolewa hivyo nasi ni
lazima tulitekeleze hilo.
2.
LENGO LA MKUTANO
Ndugu Washiriki wa Mkutano, imedokezwa katika utangulizi kuhusu lengo la mkutano
huu, mimi napenda niwasisitize kuwa mkutano huu ni muhimu kwa mustakabali wa
sekta ya afya hapa mkoani na nchini kwa
ujumla. Hii ni kwa sababu sekta ya afya inakabiliwa na changamoto mbalimbali
ambazo nyingine ziko ndani ya uwezo wenu. Kama nchi tulishapitisha sera kwamba
huduma zetu ni za kuchangia na yale makundi maalum yana utaratibu wao. Kwa kuwa
wadau wote wa Mfuko huu mpo hapa ni matarajio yangu kuwa mtatumia nafasi hii
kujadiliana kwa uwazi na kwa kina ili mwishoni mwa mkutano kila pande uwe na
maazimio yatakayosaidia kuboresha mifuko hii. Lengo letu liwe ni kujadiliana
ili kuboresha huduma siyo kutupiana lawama na kutafuta mchawi. Katika suala la
kuboresha huduma za afya, kila mmoja wetu anawajibika kwa namna moja au
nyingine.
Kwa maana hiyo basi katika mkutano huu
natamani washiriki mpate nafasi ya kufanya yafuatayo:
·
Mpate taarifa kuhusu
mambo yaliyofanywa na Mfuko ndani ya miaka 10, mafanikio na changamoto ambazo
bado zipo lakini pia maagizo mbalimbali ya Serikali na mikakati mbalimbali
ambayo Serikali imeweka kwa ajili ya kufikia
lengo la Afya Bora kwa wote.
·
Jadilianeni kuhusu
mambo mbalimbali yanayohusu uboreshaji wa Huduma Vijijini na Afya kwa wote
ambayo Mfuko wameweka kipaumbele katika hilo hasa kipindi hiki ambacho wanaanza
safari nyingine ya miaka 10 ijayo.
·
Jadiliane kwa kina
umuhimu wa CHF kwa Watanzania huku tukichukua mifano ya halmashauri kadhaa
ambazo hivi karibuni zimetunukiwa tuzo ya usimamizi wa fedha na uboreshaji wa
huduma kwani hiyo itasaidia sana kuwavuta wananchi kujiunga na CHF na hatimaye
kupata huduma za matibabu kwa njia ya kadi.
·
Ni vema pia uongozi
wa NHIF ukatueleza ni maeneo gani ambayo mshiriki mmoja mmoja anaweza kuchangia
ili kuboresha huduma za afya.
·
Hakikisheni mnatumia
uzoefu wenu kutoa ushauri katika maeneo mbalimbali ili Mfuko huu uendelee
kuimarika na kutoa huduma stahili kwa wanachama wake.
3.
UMUHIMU WA WANANCHI KUWA NA BIMA ZA AFYA
Ndugu zangu Waratibu wa NHIF na CHF mliopo hapa, ninyi ni wataalam zaidi katika suala hili la huduma za matibabu kupitia
Mifuko ya Afya ambayo mnakutana na wanachama wa Mifuko hii kila siku. Tambueni
kuwa shughuli zenu katika kuelimisha umma kuhusu Mifuko hii zina umuhimu mkubwa
katika kufanikisha dhamira ya Serikali ya Watanzania kuwa kwenye utaratibu wa
Bima za Afya.
Ni ukweli ulio wazi kuwa gharama za
matibabu zinapanda kila uchao, hivyo njia pekee ya kumkomboa Mtanzania ni kumpa
uhakika wa kutibiwa yeye na familia yake kupitia mfumo wa Mfuko wa Afya ya
Jamii ambao NHIF uko chini yao.
Nawaomba fanyeni kazi zenu kwa moyo
mmoja mkijua kuwa mafanikio ya CHF ni ndoto ya kila kiongozi katika ngazi zote
za serikali. Tumieni wakati wenu kuelimisha wananchi kuwa, raslimali ndogo
walizo nazo za mifugo au mazao wanayozalisha zinaweza kuboresha afya zao kwani
hakuna uzalishaji bila uwepo wa Afya bora.
4.
HALI YA UCHANGIAJI CHF MKOANI MARA:
Mkoa wa Mara ni miongoni mwa mikoa
ambayo wananchi wake wanachangamkia sana fursa za maendeleo kila zinapojitokeza. Lakini kwa bahati mbaya hatujaonyesha
mwamko wowote katika kuchangamkia fursa ya utaratibu rahisi wa kuchangia
matibabu kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF). Takwimu zinaonyesha kuwa hadi
mwezi Disemba mwaka jana, kati ya kaya 237,071 zilizopo katika mkoa wa Mara ,
ni kaya 1,460 tu ya kaya zilizojiunga na CHF ( hiyo ni sawa na asilimia 0.6) ya
kaya zote. Tunajiuliza tatizo ni nini?
Ni kweli wananchi wa mkoa wa Mara hawana uwezo wa kuchangia Shilingi elfu Kumi (
10,000/=) kwa kaya kwa mwaka? .
Majibu ya maswali haya mnayo ninyi
washiriki wa mkutano huu. Tutumie nafasi hii kujadiliana na kupata majibu
yatakayotusaidia kuondoa kabisa hapa tulipo.
Kutokana na hayo, kwa mujibu wa takwimu
zilizopo hapa, hali ya uchangiaji wa Mfuko wa Afya ya Jamii katika Mkoa huu
hairidhishi hivyo kila kiongozi kwa nafasi yake anatakiwa atafakarina kuweza
kushauri ni mkakati gani unaweza kutumiwaa ili kuhakikisha hali hii inabadilika
na wananchi wanajiunga na Mfuko huu ambao ndio mkombozi wa afya za wananchi.
5.AFYA NA SHUGHULI ZA KIUCHUMI;
Ndugu zangu washiriki wa mkutano huu
wa wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya
Afya, mkoa wa Mara umebarikiwa kuwa na hali nzuri ya hewa ambapo mazao
mbalimbali yanastawi vizuri lakini pia tunalo ziwa ambalo linasaidia shughuli
za uvuvi kuendelea na kuongeza pato kwa wananchi wa Mkoa huu, kwa maana hiyo
wananchi wa mkoa huu wakati wote wako katika shughuli za uzalishaji kwa njia ya
kilimo, uvuvi, ufugaji shughuli ambazo zinawezekana tu endapo afya za wananchi
hawa ni njema.
Familia yenye maradhi kila wakati
inakosa muda mzuri wa kuzalisha mali, ili familia iwe katika hali bora ya afya
ni lazima iwe na uhakika kuwa mmoja wao anapougua ana uwezo wa kwenda kwenye
kituo cha matibabu na kutibiwa hata kama hana fedha mfukoni. Uhakika huu wa
matibabu utapatikana tu iwapo wananchi wengi watajiunga na CHF na
wakishirikishwa katika usimamizi wa huduma kupitia Bodi za Afya.
Naomba katika mkutano huu tujadiliane
ni namna gani tutawahamasisha wananchi wa mkoa wa Mwanza kujiunga na CHF na
kuhakikisha kuwa wanapokwenda katika vituo vya wanapata huduma zinazostahili.
5.
HITIMISHO
Ndugu washiriki kabla ya kumaliza Hotuba yangu
naomba mhakikishe yafuatayo yanatekelezwa:-
· Kuhusu huduma za
matibabu: Watoa huduma mhakikishe mnawapa
huduma za heshima wanachama wa mifuko hii kwani huduma mnayowapa tayari
imelipiwa, watibiwe mapema ili wakawahudumie wananchi wengine.
· Wanachama muwe walinzi wa huduma zenu na hasa mnapokutana na Dawa
zinazotolewa na Serikali zinauzwa katika maduka ya watu binafsi, toeni taarifa
kwa wahusika ili hatua stahili zichuliwe.
· Watoa huduma fanyeni kazi zenu kwa uadilifu na kuwabaini wote wanaotumia au
kufanya udanganyifu katika vitambulisho vya matibabu kwa lengo la kuusaidia
Mfuko kuondokana na gharama zisizokuwa zake.
· Waajiri hakikisheni mnawaandaa watumishi wanaokalibia kustaafu ili waweze
kurejesha vitambulisho vya Mfuko na kufuata utaratibu uliowekwa katika kupata
kitambulisho kipya.
· Pia himizeni waajiriwa wapya kujaza fumo za uandikishaji ili wapate vitambulisho kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya
Afya kwa lengo la kuondoa malalamiko yasiyo na tija.
· Dawa zitumike vizuri na kuratibiwa katika ngazi mbambali. Jadilianeni kwa
kina kuhusu suala hili na mtoke na mkakati wa pamoja kwani bila uwepo wa dawa,
wanachama watapunguza imani na huduma hizi.
· Malengo ya
uandikishaji Kaya: Kila Halmashauri iwe na lengo
la uandikishaji wa kaya kujiunga na CHF na taarifa hizi nizipate kwa ajili ya
ufuatiliaji zaidi.
· Kwa Halmashauri ambazo ziko nyuma na mpango huu, viongozi husika nendeni
mkajipange na mliweke suala hili katika vipaumbele vyenu na mimi kama Mkuu wa
Mkoa naahidi kulifuatilia kwa ukaribu zaidi ili kuona utekelezaji wake.
· Kwa Mfuko wa Taifa wa
Bima ya Afya: Hakikisheni huduma ya Tiba kwa Kadi
Mijini zinaimarishwa na mpango wenu wa elimu uelekee zaidi vijijini ili
wananchi wengi wahamasike na huduma zenu.
· Taarifa za mapato na
matumizi ya fedha za CHF: Waheshimiwa wabunge
na madiwani ombeni taarifa za Fedha zitokanazo na Mfuko huu ili muweze
kufuatilia matumizi yake.
· Suala la CHF
lifanyeni kuwa agenda ya kudumu katika vikao vyenu na angalieni namna ya
kutunga sheria ndogo ndani ya Halmashauri ambazo zitawataka wananchi kujiunga
na Mfuko huu.
· Kama Mkuu wa Mkoa, naahidi ushirikiano mkubwa kwenu kama NHIF na mlango
wangu uko wazi wakati wowote.
AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA
No comments:
Post a Comment