Miaka 32 ya uhuru wa Zimbabwe
Zimbabwe inasherehekea miaka 32 tangu kupata uhuru kutoka kwa watawala wa kikoloni. Lakini licha ya kuwa huru kwa muda mrefu, Zimbabwe inayoongozwa na Rais Robert Mugabe, bado inakumbwa na matizo mengi.
Chipukizi wa chama tawala, jeshi la vijana, wapiganaji wa zamani pamoja
na wafuasi wa chama tawala kutoka pande zote za Zimbabwe leo
watasherehekea uhuru wa nchi yao. Tarehe 18. Aprili mwaka 1980 ilikuwa
siku iliyojawa na matumaini kwa watu wa Zimbabwe. "Umeshika lulu
mikononi mwako na hivyo itunze." Hayo ndiyo maneno ambayo Samora Machel,
aliyekuwa rais wa Msumbiji na Julius Kambarage Nyerere, rais wa kwanza
wa Tanzania, walimwambia Robert Mugabe siku ambapo Zimbabwe ilipata
uhuru.
Leo, miaka 32 baadaye, nchi hiyo imegubikwa na umaskini. Utawala
uliopo sasa haufanyi tena kazi ipasavyo. Andreas Sibanda ni mkimbizi
kutoka Zimbabwe. Yeye anamlaumu rais Mugabe kwa kushindwa kuipatia nchi
yake uhuru wa kweli. Kwa mtazamo wake, raia wa Zimbabwe sasa wanateseka
zaidi kuliko hata ilivyokuwa wakati wa utawala wa kikoloni.
Washington Chiula, ambaye pia ni raia wa Zimbabwe, anaupinga utawala wa
Mugabe. Anajiuliza inakuwaje Zimbabwe inajiona kuwa nchi huru wakati
asilimia 90 ya raia hawana ajira, wapinzani wa kisiasa wanagandamizwa na
watu wanakamtwa na polisi bila hatia. "Kila siku wapo watu wanaokamatwa
bila kuwa na hatia. Hakuna demokrasia. Hatuwezi kusema kwamba tuko huru
wakati hakuna demokrasia."
Chiula anaeleza kwamba asilimia 30 ya raia wa Zimbabwe, ambao ni watu
wapatao millioni 5, wamefukuzwa kutoka nchini mwao katika miaka 11
iliyopita. Mmoja wao ni Noel Mguti. Yeye alitekwa nyara na kuteswa.
Nyumba yake ilichomwa moto na kuteketea kabisa. Mke wake alipotea na
hadi leo haifahamiki mahali alipo.
Kwa sasa Mguti anaishi uhamishoni Afrika ya Kusini akiwa na msononeko
mkubwa. "Nitawezaje kusherehekea uhuru wakati akili yangu haiko huru?"
Anauliza Mguti. "Wala siko huru katika nchi niliyokimbilia. Kwa kweli
Zimbabwe haikuwa na uhuru. Watu waligandamizwa na rais wao mwenyewe.
Mugabe ndiye anayepaswa kulaumiwa kwa sababu hakuwapatia Wazimbabwe
uhuru."
Karibu kila raia wa Zimbabwe anayeishi uhamishoni ana mawazo kama
aliyonayo Mguti. Mugabe hatazamwi tena kama kiongozi aliyeiletea nchi
yake uhuru bali kama mtawala anayewafanya raia wake wateseke.
No comments:
Post a Comment