Thursday, April 19, 2012

POLISI KUSAIDIA KUWAVUSHA BARABARA WATOTO NA VIKONGWE KUEPUSHA AJALI
Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi-Zanzibar
ZANZIBAR ALHAMISI APRILI 19, 2012. Jeshi la Polisi Zanzibar limesema kuwa limekuwa likiwatumia Askari Polisi waliopangwa kufanya kazi kwa wananchi kama Polisi Shehia katika mpango wa uvushaji wa wanafunzi barabarani wanapokwenda na kutoka shuleni ili kuwaepusha na ajali za barabarani.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar ACP Aziz Juma Mohammed, amesema kuwa, Askari Polisi hao pia wamekuwa wakitoa msaada kama huo kwa vikongwe wasio na uwezo wa kuvuka wenyewe barabara.
Amesema kabla ya kuanzishwa kwa utaratibu huo, kumekuwapo na matukio mengi ya ajali za barabarani ambazo nyingi zilikuwa zikisababisha vifo na vilema vya kudumu kwa watumiaji wa barabara wakiwemo wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Kamanda Aziz amesema sambamba na mpango huo, lakini pia Askari Polisi wa Usalama Barabarani wameendelea na mpango wake wa kutoa elimu ya matumizi salama ya barabarani kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ikiwa ni sehemu ya mpango wake wa usalama kwanza ili kupunguza ajali.
Amesema kwa kufahamu kuwa wanafunzi wa leo ndio wazazi na walezi wa kesho, Jeshi la Polisi mkoani huo limeamua kutilia mkazi katika kutoa elimu kwa wanafunzi hao ili kuwajengea uwezo wa kuzifahamu sheria mbalimbali zikiwemo za matumizi salama ya barabara.
Kamanda Aziz amesema kuwa mpango wa utoaji wa elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari unafanywa na askari wa Kikosi cha Usalama barabarani wakiwemo maafisa  wa kikosi hicho kama sehemu ya uwajibikaji.
Amesema mara nyingi Askari hao wamekuwa wakienda katika shule mbalimbali kutoa elimu hiyo ili kuwawezesha wanafunzi sio kuelewa tu matumizi samala ya barabara lakini pia madhara yatokanayo na ajali za barabarani.
Amesema ajali za barabarani zimekuwa zikipoteza maisha ya watu wengi na wengine kwa mamia wakibaki na vilema vya kudumu na wengine hata kushindwa kufanya kazi za uzalishaji mali na kumudu jitunza wao wenyewe pamoja na kuzitunza familia zao na hivyo kupunguza pato la taifa.
Kamanda Aziz alikuwa akizungumza na mwandishi wa Habari hizi aliyetaka kujua mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa utaratibu huo katika mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar.

No comments:

Post a Comment