Friday, April 27, 2012

                                    CHADEMA YASHINDA CHATO KWA KISHINDO

katika Mkoa mpya wa Geita, CHADEMA kimepata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mdogo wa wenyeviti wa serikali za vijiji baada ya kuibwaga CCM kwa kupata vijiji vinane kati ya 11 vilivyokuwa vikishindaniwa.

Uchaguzi huo mdogo wa kuziba nafasi zilizoachwa wazi na baadhi ya viongozi waliokuwepo awali jimboni humo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vifo  ambao ulifanyika hivi karibuni uliwafanya baadhi ya Wana CCM kujiunga na CHADEMA mara baada ya matokoeo kutangazwa akiwamo aliyekuwa mgombea wa CCM wa Kijiji cha Minkoto.

Nafasi zilizogombewa zilikuwa zikishikiliwa na viongozi wa CCM kabla ya baadhi yao kujiuzulu, kuhamia vyama pinzani na wengine kuhama makazi yao na kwenda maeneo mengine.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari,  msimamizi msaidizi wa uchaguzi huo, Sodio Nyuga alisema CHADEMA kimefanikiwa kutwaa nafasi 8 za vijiji dhidi ya tatu zilizonyakuliwa na CCM .

Hata hivyo, CCM ilijifariji kwa kutwaa uenyekiti katika vitongoji 28 na CHADEMA kikipata nafasi 10, wakati wajumbe wa serikali za mitaa CCM kilijipatia wajumbe 92 na CHADEMA 46.

Katibu wa CHADEMA wa Wilaya ya Chato, Mange Sai, alisema ushindi uliopatikana ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa wilaya hiyo kwa kuwa baadhi ya vitongoji CHADEMA ilipitisha wagombe pasipo kuwa na upinzani wa chama tawala jambo ambalo linaonyesha wazi kukubalika kwa chama hicho kwa wananchi.

Alisema kuwa CHADEMA kilitegemea kuibuka kidedea katika uchaguzi huo mdogo kutokana na wapiga kura kuchoshwa na ahadi mbalimbali za serikali ya CCM ambazo zimekuwa hazina utekelezaji na badala yake baadhi ya viongozi wamekuwa wakijinufaisha kwa maslahi yao binafsi huku wakiwaacha wananchi wakitaabika.

No comments:

Post a Comment