TARIME
MKUTANO mkuu wa kijiji cha Nyangoto katika wilaya ya Tarime mkoani Mara,umepitisha azimio la kumfukuza ndani ya kijiji hicho mkazi mmoja Bw Wegesa Wangubo kwa madai ya kuupeleka uongozi wa kijiji hicho mahakamani akidai kurejeshea ardhi ambayo imetumika kujenga majengo ya kituo cha afya na jengo la kuhifadhia mahiti pamoja na fidia ya shilingi milioni 45.
Azimio hilo la kihistori limetolewa na wananchi hao, katika mkutano huo mkuu wa kijiji chini ya viongozi wa kijiji,kata na wale wa mila maarufu kama Ritongo,ambapo wamesema wakati kesi hiyo ikiendelea hawaoni sababu ya kuendelea kuishi na mkazi huyo kwa madai kuwa hatua yake hiyo inarudisha nyuma maendeleo ya kijiji chao.
Kwa sababu hiyo,wamewaagiza viongozi wa jadi kumtaka mwananchi huyo kuhama kijiji hapo kwa hiari kabla ya kutumia sungu sungu wa kijiji hicho kumwamisha kwa nguvu kwa maelezo wananchi wa kijiji hicho hawapo tayari kutoa ushirikiano wowote kwa mkazi huyo.
Hata hivyo afisa mtendaji wa kijiji hicho Bw Samwel Mwita na diwani wa kata ya Matongo Bartholomeo Machage,wamesema wamelazimika kuitisha mkutano huo wa kijiji kwaajili ya kujulisha wananchi kuhusu kesi hiyo inayokikabili kijiji chao ambayo pia inahusisha meneja mkuu wa mgodi wa North Mara ambaye amekuwa mfadhili wa ujenzi na ukarabati wa kituo hicho cha afya.
Kwa upande wake Bw Wegesa Wangubo,akizungumza katika mkutano huo,amesema yeye hajawahi kukishitaki kijiji hicho bali amemshitaki meneja mkuu wa mgodi huo kama sehemu ya kutafuta haki yake kwa madai baadhi ya watu waliopisha katika eneo hilo walilipwa fidia na uongozi wa mgodi huo.
Hata hivyo wakati Bw Wegesa Wangubo akidai hajawahi kukishitaki kijiji hicho,lakini hati ya mashitaka katika kesi No 79 mwaka 2011 inaonyesha kuwa mtuhumiwa wa kwanza katika kesi hiyo ni serikali ya kijiji cha Nyangoto.
,,,,,,,,,,,,,,,//,,,,,,,,,,,,,,,,,,//,,,,,,,,,,,,,,,,,,,//,,,,,,
No comments:
Post a Comment