Tuesday, July 19, 2011

MFICHUAJI WA KASHFA YA MAWASILIANO AFARIKI DUNIA

Mwandishi wa habari wa zamani wa gazeti la News of the World aliyefichua kashfa ya udukizi amepatikana akiwa amefariki.
Sean Hoare

Sean Hoare aliliambia gazeti la New York times kuwa waandishi wa gazeti News of the World walikuwa wanafanya udukizi kwa kiwango kikubwa hata kabla polisi waanze kufanya uchunguzi dhidi ya gazeti hilo.
Msemaji wa polisi ameelezea kuwa kifo cha mwandishi huyo hakieleweki lakini kufikia sasa hakuna sababu za wazi zinazoonyesha kuwa kuna hila yoyote.
Habari hizo zimetokea wakati mmiliki wa gazeti hilo Rupert Murdoch, mwanae James na aliyekuwa msimamizi wa kampuni ya News International Rebecca Brooks wanafika mbele ya kamati ya bunge kujibu tuhuma hizo za udukizi wa simu.
Naye waziri mkuu David Cameron amelazimika kukatiza safari yake barani Afrika ili awepo bungeni leo wakati wa mjadala maalum kuhusu kashfa hiyo.
Kamishna wa Polisi Sir Paul Stephenson naibu wake John Yates nao wamelazimika kujiuzulu kutoka nyadhifa zao kufuatia sakata hiyo. Wote wanatuhumiwa kuwa na uhusiano wa karibu na kampuni ya Rupert Murdoch.
Na tovuti ya gazeti The Sun nchini Uingereza, linalomilikiwa na Bw Murdoch imevamiwa na wasomaji wake kuelekezwa kwenye taarifa ya kubuni kuwa mfanyibiashara huyo maarufu amepatikana akiwa ameuawa.
Kundi moja maarufu kwa uvamizi wa tovuti za serikali ya marekani na mashirika mengine, Lulz security limedai kuhusika na uvamizi huo kupitia ujume kwenye twitter.
Shirika la News International limekiri kuwa tovuti ya gazeti lake imevamiwa lakini haijatoa taarifa zaidi kuhusu tukio hilo.

No comments:

Post a Comment