Tuesday, July 19, 2011

KIKWETE KUWAKOMBOA WATANZANIA HAWA

Musoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe:Jakaya Kikwete ametakiwa kutoa uamuzi wa mwisho juu ya hatma ya wafanyakazi wa zamani wa kiwanda cha nguo cha Musoma(Mutex) wanaodai mafao yao serikalini yanayofikia sh. bilioni nne kwa takribani miaka 17 bila mafanikio yoyote.
 
Uamuzi huo umefikiwa mjini Musoma jana katika kikao cha pamoja cha wafanyakazi hao waliokutana pamoja na mambo mengine kutaka kujua hatma ya mafao yao baada ya kuachishwa kazi kufuatia kufilisika kwa kiwanda hicho mwaka 1994.
 
Mwenyekiti wa wafanyakazi hao bw. Joseph Pundo amesema wafanyakazi hao wa zamani wa kiwanda hicho cha MUTEX wapatao 950 wamechoka na hatua ya viongozi mbalimbali wa serikali toka awamu ya tatu ya uongozi wa serikali ya Rais mstaafu Benjamini Mkapa jinsi gani wanavyolitafutia ufumbuzi suala hilo huku wakionekana kushindwa kulipatia jawabu sahihi.
 
Bw. Pundo amesema matokeo yake serikali ya awamu ya tatu kupitia kwa mfilisi wake LART, iliwahadaa wafanyakazi hao kwa kutaka kuwalipa kiasi cha kati ya sh. elfu sita na elfu hamsini tu za kitanzania kama mafao yao licha ya kukitumikia kiwanda hicho kama watumishi kwa zaidi ya miaka kumi,ushawishi uliokubaliwa na baadhi ya wafanyakazi wachache kutokana na ugumu wa hali ya maisha unaowakabili.
 
Hivyo amesema kiongozi pekee aliyebaki serikalini ambaye hajasikiliza na kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu hatma ya mafao yao ni Rais Jakaya Mrisho Kikwete pekee ambaye wafanyakazi hao wanaamini ndo mweye suluhisho litakalopelekea kupatikana kwa hatma ya mafao yao waliyoyasotea kwa miaka mingi huku baadhi yao wakiwa wameshafariki dunia na kuziacha haki zao.
 
Kiwanda cha nguo cha Mutex kilichojengwa na serikali ya Tanzania kwa msaada wa serikali ya Ufaransa kilianza uzalishaji wake mwaka 1979 kikiwa chini ya shirika la viwanda vya nguo nchini (TEXCO) hadi mwaka 1994 kilipofilisika na kushindwa kuendelea na uzalishaji huku waliokuwa wafanyakazi wake wakibaki kupigwa danadana wasijue nani wa kuwalipa kinua mgongo chao.

No comments:

Post a Comment