Wednesday, September 1, 2010

SERIKALI YASHAURIWA KUFUTA MABARAZA YA ARDHI

Bunda

Baadhi ya wakazi wilayani hapa wameishauri serikali kuyafuta mabaraza ya ardhi ya kata kwa vile yanaendesha kazi zake katika misingi ya rushwa badala ya kutenda haki kulingana na sheria.
 
Wakiongea na mwandishi wa habari hizi jana (Jumatatu) wakazi hao walisema mabaraza hayo yaliyoundwa na serikali miaka mitatu iliyopita kwa lengo la kuamua mashauri ya ardhi katika misingi ya haki kwa sasa yamegeuka kuwa mahala pa kujichumia pato miongoni mwa wajumbe wake kutokana na kutawaliwa na rushwa.
 
Mmoja wa wakazi hao Festus Makoye aliyepata kulalamika katika moja ya baraza alisema kinachofanyika ndani ya mabaraza hayo ni kinyume cha misingi ya utawala wa haki na sheria unaohubiriwa na serikali ya awamu ya nne kwa nguvu zote kwani wajumbe wake kabla ya kutoa hukumu hukuuliza kama una chochote mkononi mwako ili wakupendelee.
 
 “Hamna haki mle;kuna rushwa tu. Mwandishi kabla ya kuhukumiwa unaulizwa kama una chochote kwa ajili ya wazee ili upewe haki yako.Hii hufanywa siri kwani anakuja mjumbe wao maalum kukuletea hoja hiyo,ukiikataa umeumia;ukiikubali ndo hivyo umeukata,”alisema Festus.
 
Festus aliyeeleza kuwakatalia wajumbe hao hoja yao hiyo hali iliyomnyima haki katika baraza hilo ameishauri serikali kuangalia uwezekano ama wa kuyafuta mabaraza hayo au kubadilisha muundo wake wa utendaji ili uendane na misingi ya utawala wa sheria ili yawatendee haki wananchi kama yalivyokusudiwa.
 
Habari zinasema kuwa wajumbe wa mabaraza hayo wamekuwa wakiomba rushwa wanayoiita’chakula cha wazee’kwa kisingizio kuwa hawapewi posho na serikali ingawa hata hivyo halmashauri ya wilaya hii ilishaanza kuwalipa posho kutoakana na faini wanazotoza katika mashauri wanayoamulia.
 
Hata hivyo mwanasheria wa wilaya hiyo Phillip Shoni amemweleza mwandishi wa habari hizi kuwa pamoja na kulipwa posho mabaraza hayo yamekuwa mstari wa mbele katika kuendekeza rushwa hali iliyoifanya serikali kuazimia kuyafuta mwezi ujao (Septemba) na kuyaunda upya na kutumia fursa hiyo kuwaomba wakazi hao kuvuta subira wakati mchakato wa kuyafuta ukiendelea.
                  

No comments:

Post a Comment