Thursday, September 2, 2010

JESHI LA POLISI TARIME LATOA ONYO

JESHI la polisi katika kanda maalum ya Tarime na Rorya limeviagiza vyama vya siasa na wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 31 mwaka huu ndani ya mkoa huo wa kipolisi kuepuka vitendo vyovyote ambavyo vinaweza kuhatarisha kukosekana kwa hali ya amani na utulivu.

Agizo hilo limetolewa juzi mjini Tarime na kamanda wa mkoa huo wa kipolisi wa Tarime na Rorya, kamishina msaidizi Constantine Massawe, wakati akielezea namna ya jeshi lake lilivyojipanga kukabiliana na vitendo hivyo wakati huu wa kampeni za uchaguzi mkuu na siku ya upigaji wa kura.

Alisema wilaya ya Tarime imekuwa na historia ya ya kuwa na matukio mbalimbali ya kutisha wakati wa chaguzi na hivyo jeshi hilo limejipanga kikamilifu katika kukabiliana na vitendo hivyo.

Alisema miongoni mwa mikakati ambayo itachukuliwa na jeshi la polisi ni pamoja na kuweka ulinzi wa kutosha wakati wote wa zoezi hilo ili kuwapa fursa wananchi na wagombea kushiriki katika mchakato huo wa uchaguzi mkuu bila ya kubugudhiwa.

"Tunategemea viongozi wa vyama vya siasa na wagombea wa nafasi mbalimbali wawe chachu ya amani na utulivu kwenye mchakato huu,na watumie mikutano ya kampeni kuwaelimisha wapiga kura umuhimu wa kutunza amani iliyopo"alisema Kamanda Massawe.

Kamanda Massawe,alisema jeshi la polisi halitasita kuchukua hatuo kwa mtu ama chama chochote kitakachobainika kutumia wafuasi wake kuzomea,kutoa lugha za mtusi,kuvaa sare ama kubeba bendera ya chama kingine cha siasa katika eneo la kampeni za chama kingine.

"Tutahakikisha kwamba wale wote watakao vunja sheria zinazohusu suala la uchaguzi pamoja na zile za nchi kwa ujumla wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria bila upendeleo wowote"alisisitiza
Kiongozi huyo wa jeshi la polisi,ametumia nafasi hiyo pia kuwaonya waandishi wa habari kufanya kazi yao kwa kuzingatia maadili ya uandishi wa habari,kwa kuepuka kuandika habari za uongo ama kuongeza chumvi kwa lengo la kupendeleoa ndugu ama ukoo atokao jambo ambalo alisema linaweza kusababisha uvunjivu wa amani.

Kauli ya kamanda Masawe,imeitoa kufuatia kuwepo madai kuwa baadhi ya waandishi wilayani Tarime kuandika habari za ushabiki wa koo watakazo jambo ambalo limesababisha mgawanyiko miongoni wao.

Mwisho

No comments:

Post a Comment