Tarime
CHAMA cha Mapinduzi mkoani Mara,kimewaonya viongozi wake kuacha kukihujumu chama chao kwa kutumia viongozi wa mila kupiga kura za koo katika jimbo la Tarime.
Chama hicho pia kimesema hakitasita kuwafukuza ndani ya chama viongozi wake watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo.
Katibu wa CCM mkoani Mara Bw Ndekubali Ndeng'aso,alisema hayo mjini Tarime wakati akizungumza na wagombea wa udiwani na ubunge wa chama hicho wa majimbo ya Rorya na Tarime.
Alisema kuna taarifa ya kuwepo baadhi ya viongozi wa CCM katika ngazi ya wilaya,mkoa na baadhi ya wagombea walioshindwa katika kura za maoni kuwatumia wazee hao wa jadi kukihujumu chama hicho jambo ambalo alisema kamwe halitavumiliwa ndani ya chama.
"Tumesikia kuna viongozi wenzetu wameanza vikao na viongozi wa mila kukihujuma chama chetu..nawaonya viongozi na wagombea wanatajwa kuhusika na vitendo hivyo sisi tumetuma watu wetu kupeleleza na kutukibaini kuhusika kwao hatutaweza kumvulia mtu wa namna hiyo hata kama akiwa kiongozi mwenye cheo kikubwa"alisema Ndeng'aso.
Alisema CCM inaheshimu sana viongozi wa mila katika kuongoza jamii kulingana na taratibu na si jambo jema viongozi hao wa mila wakatumia heshima hiyo kujiingiza kutafutia wananchi viongozi.
Katibu huyo wa CCM mkoani Mara,aliwakumbusha viongozi wanaodaiwa kufanya vitendo hivyo kukumbuka kuwa Tanzania ni nchi yenye makabila mengi na dini mbalimbali na si jambo la busara kuwagawa wananchi kwa kutumia koo kwani alisema kufanya hivyo pia ni kinyume cha katiba ya nchi.
"Kauli yetu ndani ya CCM ni mafiga matatu yaani diwani wa CCM,mbunge wa CCM na kura kwa mgombea urais wa CCM na tukifanya hivyo tutakuwa tumeweka msingi mzuri wa kuharakisha maendeleo yetu kwa kuwa na sauti ya pamoja..hapa tarime CCM inawanachama wengi kuliko chama chochote cha siasa jambo la msingi ni kuhakikisha kipindi hiki tunashinda kwa kishindo katika kurejesha heshima yetu"alisema.
Alisema mbali na jimbo hilo kuongozwa na upinzani kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita lakini Serikali ya CCM chini ya rais Jakaya Kikwete haikuweza kulibagua kimaendeleo katika nyanja zote na kwamba endapo CCM itaiibuka na ushindi katika uchaguzi wa Oktoba 31 kasi ya maendeleo hayo itaongozwa mara dufu kuliko ilivyo hivi sasa ili wana tarime pia waweze kunufaika na keki ya taifa.
Wagombea wa ubunge jimbo la Tarime kupitia CCM ni Nyambari Nyangwine na jimbo la Rorya ni Lameck Airo.
Wakati huo huo chama cha mapinduzi mkoani Mara tayari kimepata ushindi wa madiwani 22 waliopita bila kupingwa jimbo la Musoma vijijini likiongoza kwa kupata madiwani 15,Buna wawili,Serengeti wanne na Rorya diwani mmoja.
Mwisho
No comments:
Post a Comment