Thursday, April 23, 2015

Wananchi Butiama watoa ya Moyoni,wamuomba Prof Muhongo kugombea urais wa Tanzania
Baadhi ya Wananchi katika wilaya ya Butiama mkoani Mara wametoa ya moyoni kwa kumuomba aliyekuwa waziri wa nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo kugombea nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha Mapinduzi CCM .

Wakiongea kwa nyakati tofauti katika kijiji cha Kiriba kata ya Bwai halmashauri ya Musoma Vijiji,wananchi hao walisema kuwa wamefika hatua hiyo ya kumuomba Profesa Muhongo baada ya kuridhishwa na utendaji wake wa kazi wakati akiwa katika wizara ya nishati na Madini na hasa kwa kitendo chake  cha kuwakumbuka watu wanaoishi vijijini.

“Mwaka huu lazima nipige kura kwa Chama cha CCM pale watakapomsimamisha Prof Muhongo kuwa mgombea wa chama hicho,sikuwahi kufiria katika miaka niliyobakiza hapa duniani ningeuona umeme maana toka uhuru huku hata nguzo hatukuziona ila muhongo kafanya jambo la kishujaa sana”alisema Bw Joseph Magoti mkazi wa Bwai Kwitululu.

Mbali na Bwana Joseph kuelezea kile ambacho alisema kina msukumu kumshaiwishi Prof Muhongo kugombea nafasi hiyo lakini pia baadhi ya akina mama walipata nafasi ya kutoa maoni yao kuhusu hatua hiyo walidai kuwa kupelekwa kwa umeme katika vijiji mbalimbali hapa nchini imesaidia kupunguza umaskini kwa wananchi walio wengi.

Bi Sophia Matiku aliyesema kwasasa amebadili maisha yake kufuatia kuwepo kwa nishati ya umeme katika kijiji hicho alisema haoni sababu ya Prof Muhongo kutogombea nafasi hiyo kwani wale wote waliotajwa katika kinyang’anyiro hicho bado wanapwaya kutokana na utendaji wao katika nafasi walizoweza kushika.

“Wanasema mnyonge mnyongeni haki yake mpeni,huyu Profesa kiukweli kwa muda mfupi aliokaa kwenye ile wizara ya umeme (Nishati na Madini) alifanya kazi kubwa sana na kama angekuwepo tangu Rais Kikwete anaingia madarakani leo vijiji vyote vingewaka umeme,kwa kweli katika hilo mimi naomba agombee nafasi ya urais ili na sisi wanyonge tusaidiwe”alisema Bi Sophia Matiku.

Hata hivyo mbali na wananchi hao kuta sifa hizo kwa aliyekuwa waziri wa nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo,Bw Juma Wambura alisema muda umefika kwa watanzania kuamua kwa pamoja kumchagua kiongozi ambaye atafanya maamuzi ambayo yatanufaisha watanzania wote ni kikundi cha watu.

Alisema msimamo aliounyesha Profesa Muhongo wakati akiwa katika nafasi ya uwaziri wa nishati na Madini ni mfano tosha kwa kiongozi ambaye anastahili kuiongoza Tanzania kwasasa.

‘Nchi yetu leo ina tatizo la viongozi kuwa na maamuzi ambayo atayatoa na kuyasimamia bila kuogopa mtu lakini kiukweli Profesa anastahili kuwa Rais maana msimamo aliokuwa nao ndiyo unatakiwa leo hapa nchini.alisema Bw Juma Wambura.

Pamoja na kuwepo kwa kauli mbalimbali juu ya kumshawishi Profesa Muhongo kugombea nafasi ya Urais ndani ya Chama cha Mapinduzi,Bw Musa Hassan mkazi wa Mgango ambaye amewahi kuwa mtumishi katika serikali ya awamu ya pili alisema kuwa angependa Profesa Muhongo kuwa rais wa awamu ya Tano wa Tanzania ili kusaidia uchumi wa Tanzania ukue tofauti na sasa.

Alisema pamoja na kuamini Profesa Muhongo anaweza kukuza uchumi wa Tanzania zaidi ya hapa lakini pia ukusanyaji wa kodi utaongezea mara dufu kwani kwasasa ukusanyaji wa kodi si mzuri kutokana na mifumo iliyopo  ya kukusanya kodi kwa Maskini na kuwaacha matajiri.

 “Kiukweli bado sijaona mtu ambaye anaweza kuitoa Tanzania hapa ilipo kwani hao wote wanajitangaza hawana uwezo wa kukuza uchumi wa Tanzania na wakasimamia vyema ukusanyaji wa kodi,nampenda Profesa sababu hana urafiki na matajiri sasa ukiona mtu wa hivyo hataona haya kumwambia mtu alipe kodi´alisema Bw Musa Hassan

Kwa nyakati tofauti baadhi ya makundi mbalimbali yamekuwa yakijitokeza na kumuomba aliyekuwa Waziri wa nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kugombea nafasi ya urais katika chama cha Mapinduzi lakini mpaka sasa Profesa Muhongo hajasema chochote.

No comments:

Post a Comment