Wahariri 25 kutoka vyombo mbali mbali vya habari vikiwamo
magazeti, redio, televisheni na hata mitandao ya kijaamii Tanzania Bara na
Visiwani (Zanzibar) wamenufaika na mafunzo ya usalama kutoka kwa Mtandao wa
Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC).
Mafunzo hayo ya siku tatu yaani tarehe 13 hadi 15 Juni,
yalitolewa na wakufunzi wa ndani ya taasisi Bw. Onesmo Olengurumwa ambaye ni
mratibu wa THRDC na Bw. Elias Mhegera ambaye ni afisa habari katika mtandao
huu. Wengine waliotoa mada ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitengo cha
habari Dk. Ayub Rioba, na mshauri mwelekezi, ambaye pia ni mhariri mkongwe Bw.
Rweyemamu kutoka New Habari 2006 Ltd.
Miongoni mwa wahariri walitoka mikoani kama vile Mbeya,
Arusha, Kigoma, Zanzibar n.k. usawa wa kijinsia ulizangatiwa katika utoaji wa
mafunzo hayo. Mada zilizofundishwa ni pamoja na namna ya kuchukua tahadhari
katika utekelezaji wa kazi za uandishi, namna ya kung’amua na kutathmini tishio
la kiusalama, namna ya kutunza taarifa katika njia salama na maadili ya
kitaaluma katika fani ya habari.
Aidha Dk. Rioba alizungumzia hatari zinazowakabili waandishi
wa habari za uchunguzi na namna ya kukabiliana nazo. Mafunzo hayo yalitumika
pia katika kujadili changamoto mbali mbali wanazokutana nazo wahariri na hata
falsafa mbali mbali zinazoleta mikinzano katika utendaji wao wa kazi. Hii ni
pamoja na mitazamo ya kiitikadi, sheria zinazobana uhuru wa habari na hata
maslahi kinzani ya wamiliki wa vyombo vya habari.
No comments:
Post a Comment