Wednesday, May 28, 2014

Wanachama Simba waandamana wakitaka Wambura arudishwe katika Uchaguzi wa June 29

Mamia ya wapenzi na washabiki wa klabu kongwe ya mpira wa miguu hapa nchini Simba SC  leo (May 28,2014)  mchana wamejikusanya kwa wingi katika makao makuu ya klabu yao hiyo,kupinga Michael Wambura kuondolewa kwenye orodha ya wagombea kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Juni 29,2014.

Wanachama hao ambao walizunguka jengo hilo na kutaka wapewe sababu za msingi kwanini Wambura ameondolewa huku wakitaka kufanya vurugu lakini vyombo vya usalama waliwahi kufika eneo la tukio na kuweza kuwatuliza wanachama Hao.

Polisi wakiwa wamefika eneo la klabu ya simba ili kuimarisha ulinzi na kuwataka wanachama wa simba kutulia ili wapate majibu kwa kamati ya uchaguzi.

Wanachama wa simba wakiwa wamelizunguka Jengo la klabu yao mchana huu kupinga kuondolewa kwa wambura kwenye uchaguzi wa klabu hiyo.Picha na Sek David
Michael Richard Wambura aliyekuwa anawania nafasi ya uenyekiti katika klabu ya Simba kupitia uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Juni 29, jijini Dar es Salaam, amechujwa katika mbio hizo kwa kutokuwa mwanachama.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Damas Ndumbaro, amesema Wambura ameenguliwa kwa kutokidhi matakwa ya kanuni zinazotumika katika mchakato huo kutokana na dosari katika uanachama wake.
Ndumbaro alisema kutokana na Wambura kuvuliwa uanachama wake mwaka 2010 kwa kosa la kuishitaki Simba mahakamani, jambo hilo lilipaswa kupelekwa kwenye mkutano mkuu wa wanachama kwa uamuzi wa mwisho kwa mujibu wa ibara ya 55 ya katiba ya klabu hiyo.
Alisema kamati yake ilipokea barua tatu kutoka kwa Wambura, ikiwemo ya Desemba 12, mwaka 2012 kwenda kwa Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage akiomba kuelezwa hatma ya uhalali wa uanachama wake na akajibiwa kuwa ingefanyiwa kazi.
Ndumbaro ambaye ni mwanasheria kitaaluma, alisema kwa mazingira hayo, kamati yake ilibaini kuwepo kwa mchanganyiko wa barua hizo na kudai kusema Ibara ya 12 ya Simba, mwanachama aliyesimamishwa uanachama anakosa haki ya msingi ya kushiriki uchaguzi, iwe kuchaguliwa au kuchagua.
Kati ya wagombea waliokuwa wakipingwa, Wambura alikuwa akiongoza kwa kupingwa na wanachama watano; Said Lubea, Ustadh Masoud, Jackson Chacha, Varentino Nyaru na Swalehe Madjaba, lakini baadhi ya pingamizi zilitupwa kwa kukosa nguvu ya hoja.
Mbali ya Wambura, wagombea wengine waliokuwa wamepingwa ni Geofrey Nyange ‘Kaburu’, Swedy Nkwabi na Joseph Itang’are ‘Kinesi’ kwa nafasi ya makamu pamoja na Aveva anayewania nafasi ya rais.
Wengine waliokuwa wakipingwa ni Ibrahim Masoud ‘Maestro’, Said Pamba, Chano Almas na Daniel Manembe wanaowania nafasi ya ujumbe, ambao wote wamepenya kutokana na kufanikiwa kupangua pingamizi dhidi yao.
Akizungumzia kuenguliwa kwake, Wambura alisema ni kitu ambacho alikitarajia kutokana na dalili kujitokeza mapema katika mchakato huo kwa lengo la kumkwamisha, lakini atapambana kwa kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo kwani ni mwanachama halali wa klabu hiyo.
Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Juni 29, kuhitimisha zama za Alhaji Ismail Aden Rage aliyeingia madarakani Mei 9, 2010.

No comments:

Post a Comment