Thursday, April 24, 2014

Udhaifu wa usimamizi waua elimu ya watu wazima

Elimu ya watu wazima ni elimu ambayo hutolewa kwa watu wenye umri mkubwa, lengo la Elimu ya watu wazima ni pamoja ya kujifunza jambo lolote lenye shabaha ya kumwendeleza mwanadamu ili aweze kuyamudu mazingira yake.

Pamoja na hayo nia kubwa ya elimu hii ni kumwendeleza mtu ambaye  hakubahatika kupata elimu ya Msingi.

Kwa Tanzania inaelezwa kuwa mkakati huu ulianza mara baada ya nchi kupata uhuru Mwaka 1961 ambapo suala hili lilipewa kipaumbele lengo likiwa ni kupambana na ujinga, Maradhi na Umaskini.
Taarifa zinaeleza kuwa mpango huu ulifanikiwa kwa asilimia kubwa kupunguza idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika wakati wa Serikali ya awamu ya Kwanza lakini kwasasa inaonekana idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika imeongezeka kwa kasi.

Wakati wa Serikali ya awamu ya kwanza chini ya hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere idadi ya walimu katika Shule za Msingi na Sekondari ilitosheleza ambapo ilipelekea walimu hao kuweza kufundisha Elimu ya watu wazima.

Kutokana na hali ngumu ya Uchumi kwa sasa na ongezeko la uandikishaji  wanafunzi wa Shule za Msingi kuwa mkubwa kumekuwepo na upungufu mkubwa wa walimu na hivyo kushindwa kufundisha katika madarasa ya elimu ya watu wazima na hivyo madarasa mengi ya elimu ya watu wazima kukosa wawezeshaji.

Kaimu Afisa elimu ya watu wazima katika halmashauri ya manispaa ya Musoma mkoani Mara Mwalimu Fibe Okelo alisema kwasasa elimu ya watu wazima ni kama vile imepuuzwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Alisema mwaka 1964 katika mpango wa miaka 5, 10 hadi 20 msisitizo ulikuwa elimu kwa wote na Mwaka 1970 Msisitizo wa elimu ya watu wazima ulitangazwa na Mwalimu Nyerere kuwa suala la kuelimisha watu wazima lilikuwa ni jukumu la kila Mtanzania aliyekuwa anajua kusoma na kuandika tofauti na ilivyosasa.

"Nyakati za Mwalimu kulikuwa na msisitizo mkubwa sana katika suala la elimu ya watu wazima jambo ambalo kila mtanzania aliliona kama linamhusu tofauti na leo kila mtu na mambo yake" alisema Afisa huyo.

Mwalimu Okelo anaendelea kuelezea kuwa juhudi hizo wakati wa mwalimu ziliweza kupunguza idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika kuwa asilimia 6.7 Mwaka 1967 huku Mwaka 1980 idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika ilianza kuongezeka kutokana na vita ya Kagera ambapo idadi iliongezeka hadi kufikia asilimia 9.6 huku kwa sasa idadi hiyo ikiwa imeongezeka hadi kufikia asilimia 31.

Kwa sasa hali ngumu ya Maisha na kiuchumi  imeweza kuzalisha kundi lingine la vijana la wasiojua kusoma na kuandika kutokana na kukosa nafasi ya kuandikishwa darasa la kwanza.

Aidha afisa elimu huyo watu wazima alieleza kuwa kwasasa takwimu za watu wasiojua kusoma na kuandika katika wilaya ya Butiama ni pamoja ana ME 89,396 huku KE 103,501 huku idadi ya watu wasiojua kusoma,kuandika na kuhesabu ikiwa ni asilimia 82 na idadi ya wanakisomo ikiwa ni 3,575.

Akielezea kuhusu sera ya elimu ya watu wazima,Mwalimu Okelo alisema kuwa Sera ya Kisomo chenye Manufaa (KCM) haiwezi kufanikiwa kutokana na viongozi kutotoa kipaumbele katika elimu hiyo bali kwa sasa limebaki jina la kuwepo kwa elimu ya watu wazima (EWW).
Alisema kutokuwepo kwa bajeti ya kutosha katika kuendesha Madarasa na idara hiyo ni tatizo katika mustakabali wa elimu hiyo kwani viongozi wetu hawaoni kama kuna umuhimu katika elimu hiyo.

"Itakuwa kazi sana kufanikiwa katika Elimu ya watu wazima na hii ni kutokana na viongozi kutotekeleza sera ya Elimu ya watu wazima,tunapanga bajeti lakini bajeti hailetwi sasa hapo sisi tutafanya nini" alisema Mwalimu Okelo.

Alisema EWW si mfumo rasmi kama ulivyo mfumo wa elimu wa Moja kwa moja hapa kuna madarasa ambayo wahusika huzalisha na hiyo ndiyo tafsiri sahihi ya EWW kuwa ni kisomo chenye Manufaa.

Mbali na kutokuwepo kwa bajeti lakini pia hakuna vitabu ambavyo vinaendana na sera yenyewe katika kutoa elimu ya watu wazima.Madarasa rasmi na hivyo kusababisha kutoa elimu hiyo katika mfumo usio sahihi.

Katika hatua nyingine imeonekana kuwepo kwa uzembe wa viongozi katika kusimamia na kuhimiza sera ya elimu ya watu wazima kutekelezwa kutokana na kutokuwepo kwa hamasa kwao,mfano katika wilaya Mwenyekiti wa kuhamasisha elimu ya watu wazima ni Mkuu wa wilaya akisaidia na Mkurugenzi lakini viongozi hao pamoja na kuwepo kwa jukumu kubwa katika kufanikisha suala hilo hakuna msumo wowote wanaoutoa katika Jamii au vikao vya Madiwani.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma Bw Musiranga Muhabi  alisema tatizo kubwa ambalo linasababisha kutofanikiwa katika utekelezaji wa elimu ya watu wazima ni ukosefu wa Bajeti ambao umekuwa tatizo kubwa katika halmashauri.

Alisema mara nyingi bajeti ya elimu ya watu wazima inaunganishwa katika idara ya elimu hivyo fedha zinapokuja huunganishwa katika mfumo wa elimu ulio rasmi kutokana na mahitaji yake hivyo nadhani ingekuwa bora kama serikali ingetenga idara ya elimu ya watu wazima ambayo inajitegemea.

"Kufanikiwa bado nji tatizo kutona na bajeti kuwa ndogo mimi nadhani kama kweli tunataka kufanikiwa katika suala hili ni bora kitengo hiki kingejitegemea ili kuleta ufanisi mkubwa" alisema kaimu Mkurugenzi huyo.

Baadhi ya watu waliosoma elimu ya watu wazima nyakati za serikali ya awamu ya kwanza walisema kwa sasa elimu ya watu wazima ipo kwa sababu isije kuonekana imekufa mikononi mwa watu lakini hakuna ambaye anajali eneo hilo.

Mzee Nyanjofu Majaaliwa alisema kuwa kama sio kisomo hicho leo hasingejua kusoma na kuandika lakini kulingana na sera nzuri iliyokuwepo waliweza kufanikiwa hadi kufikia kufanya kazi kwenye Makampuni wakati huo.

Naye Mwalimu Mstaafu Juma Nyasoro ambaye aliwahi kufundisha madarasa ya Elimu ya watu wazima alisema kuwa wakati wa Serikali ya awamu ya kwanza hayati walimu Nyerere aligundua watanzania hawajui kusoma wala kuandika hivyo hatua za haraka zilihitajika.

Alisema kuwa hata walimu waliokuwa wanajitolea kufundisha Madarasa hayo walikuwa na moyo tofauti na leo walimu wengi wametanguliza Masilahi mbele bila kuangalia athari ambazo jamii inazipata.

"Sisi tulikuwa na moyo wa kujitolea katika kuhakikisha watanzania wanaondokana na tatizo la kutojua kusoma na kuandika tofauti na leo kila mwali mu anatnguliza pesa kwanza" alisema Mwalim huyo Mstaafu.

Katika hatua hiyo Mwalimu huyo Mstaafu alisema kuwa bila kuwepo na msukumo kutoka idara huska elimu ya watu wazima itabaki jina huku akieleza kuwa hajui kama madarasa hayo bado yapo.

Nao baadhi ya wananchi mbalimbali walipata nafasi ya kuhojiwa na mwandishi wa Makala hii walisema kuwa itakuwa kazi kukuza eneo hilo kutokana na Serikali kutoiona kama ina manufaa katika jamii,mmoja wa mwananchi aliyejitambulisha kwa jina la Ally Ramadhani Mkazi wa manispaa ya Musoma alisema kuwa si rahisi kufanikiwa katika eneo hilo kwasasa kutokana na hali ya uchumi ilivyo lakini viongozi kutotoa msukumo katika elimu hiyo.

Alisema kuwa Mamlaka huska zinapaswa kuweka bajeti ambazo zitasaidia katika kukuza na kuendeleza elimu ya watu wazima ili kionekana kuwa na Manufaa tofauti na sasa ambapo idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika inaongezeka na hasa kundi la vijana.

source: http://www.jambotanzania.com

No comments:

Post a Comment