Tuesday, December 3, 2013

'Ni ukandamizaji':Wanahabari wa Kenya


Mamia ya wanahabari nchini Kenya wameandamana nchini humo kupinga sheria mpya ya vyombo vya habari iliyopendekezwa na wabunge na kufanyiwa mageuzi na Rais Uhuru Kenyatta.
 
 
Wanahabari hao waliokisiwa kuwa 300 baadhi wakiwa wameziba midomo yao kwa karatasi ya gundi (masking tape) kama ishara ya kukandamizwa, waliwasilisha malalamiko yao kwa bunge la taifa.
Sheria hiyo ambayo bado ni rasimu, itajadiliwa bungeni baada ya Rais kuikataa ilivyoandikwa akiwataka wabunge kuifanyia mabadiliko kabla ya kuifanya sheria.


Wakosoaji wanasema sheria hiyo ikiwa itapitishwa itabana uhuru wa vyombo vya habari licha ya mageuzi yaliyopendekezwa na Rais mwenyewe.


Wanadai kuwa mapendekezo hayo mapya ni makali zaidi kwa uhuru wa vyombo vya habari hata kuliko mapendekezo ya hapo awali yaliyoidhinishwa na bunge kabla ya bwana Kenyatta kukataa kutia saini.


Naibu wa chama cha wahariri nchini kenya David Ohito alisema kuwa waandisihi wanataka mswaada huo unaojadiliwa bungeni kufanyiwa mabadiliko.


Aliongeza kuwa ikiwa itapitishwa sheria hiyo, inatoa fursa ya kuundwa kwa jopo la serikali litakalowachunguza waandishi wa habari na kuwatoza dola 5,500 kama faini huku makampuni yakitozwa dola 230,000 ikiwa watapatikana na hatia ya kukiuka sheria za uandishi ambazo zinasisitiza umuhimu wa uhakika wa taarifa zinazopeperushwa.

Chanzo BBCSwahili

No comments:

Post a Comment