Saturday, December 21, 2013

Kamati ya Bunge yataka watendaji Maliasili wang’olewe


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli akiwasilisha taarifa kuhusu tathmini ya matatizo yaliyotokana na Operesheni Tokomeza Ujangili, bungeni Dodoma jana. Picha na Emmanuel Herman.

 Na Sharon Sauwa, Mwananchi Posted Decemba21 2013 saa 9:13 AM Kwa ufupi • Tathmini ya Kamati ilibaini kuwa maofisa wa Maliasili hawakutekeleza wajibu wa ipasavyo hali Dodoma.

 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imependekeza watendaji wakuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii akiwemo Mkurugenzi wa Wanyamapori, Profesa Alexanda Songorwa, kuwajibishwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa kuhujumu Operesheni Tokomeza Ujangili.

 Pia kamati hiyo imemtaka Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Dk David Mathayo kujipima na kuona iwapo bado anastahili kuendelea kuhodhi wadhifa alionao. 

Akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo ya kuhusu tathmini ya matatizo yaliyotokana na operesheni hiyo bungeni mjini Dodoma jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, James Lembeli, alisema kamati hiyo imebaini baadhi ya viongozi wa kisiasa na kiserikali waliingilia utekelezaji wa operesheni hiyo kwa manufaa yao binafsi.

 Lembeli aliliomba Bunge liazimie kwamba Serikali ihakikishe kuwa kuna uwajibikaji wa pamoja pale inapoamua kutekeleza jambo la kitaifa kama Operesheni Tokomeza.

 Alisema kamati hiyo imebaini kuwa taarifa kwa umma iliyotolewa kwa vyombo vya habari na mkurugenzi wa wanyamapori Oktoba 23, mwaka huu, haikuwa sahihi na pia ililenga kudanganya umma kwa kuficha mazingira na sababu za kifo cha Emiliana Gasper Maro. 

“Bunge liazimie kwamba Serikali ichukue hatua za kumwajibisha mkurugenzi huyo kwa kudanganya umma kwa kujaribu kuficha ukweli,” alisema.

 Kamati pia imebaini kumekuwepo na mchezo mchafu unaofanywa na baadhi ya maofisa wa wanyamapori na wa misitu, katika mapori ya akiba, misitu ya Serikali na katika baadhi ya hifadhi za taifa kwa kupokea rushwa, kutesa wananchi, kuwabambikia kesi na kujihusisha na ujangili.

 Aliomba Bunge liazimie Serikali ifanye tathmini nchi nzima, kwa lengo la kutambua kiwango cha vitendo vya rushwa, miongoni mwa watumishi wao na kuwachukulia hatua stahiki za kinidhamu wale watakaobainika kuhusika ikiwa ni pamoja na kuwawajibisha na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria. 

Alisema kamati hiyo imebaini kwamba pale Jeshi la Wananchi (JWTZ) linaposhirikishwa katika operesheni ufanisi mkubwa hupatikana, hivyo bado ipo haja ya kuendeleza operesheni hiyo kwa masilahi ya taifa. 

Lembeli alisema ushahidi wa mazingira unaonyesha kuwa JWTZ ilichukua uongozi wa operesheni baada ya kugundua washiriki kutoka vikosi vingine (Polisi, Tanapa, TSF na NCAA) kwa kushirikiana na wafugaji wenyewe ushawishi wa kifedha na wanasiasa, walihujumu operesheni hiyo kwa kutoa taarifa kwenye mitandao mikubwa ya kijangili.

 Alisema mtandao huo umejengeka kuanzia wizarani hadi kwenye maeneo ya hifadhi na kusaidia ‘majangili papa’ wasikamatwe.

 “Kamati inaliomba Bunge liazimie kwamba Serikali ichukue hatua za makusudi kuvunja mtandao huo na kuandaa operesheni nyingine ambayo itapangwa kutekelezwa na JWTZ na Idara ya Usalama wa Taifa,” alisema.

 Aidha, alisema kamati hiyo, imebaini migogoro wanayokumbana nayo wafugaji kutokana na kuingiza mifugo kwenye maeneo ya hifadhi pamoja na kero nyingine ni kutokana na kukosekana kwa miundombinu sahihi na endelevu kwa mifugo.

 Alisema licha ya kupitia nyaraka mbalimbali ikiwemo sheria na mpango kazi wa operesheni hiyo, kamati ilifanya mahojiano na watu mbalimbali, akiwemo Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki. 

Wengine waliofanyiwa mahojiano na kamati hiyo ni pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori na Mkurugenzi Msaidizi Kikosi Dhidi ya Ujangili.

 Viongozi wengine waliohojiwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Hifadhi za Misitu (TFS). 

Pia kamati hiyo ilifanya mahojiano na baadhi wabunge na kuzuru maeneo yaliyoainishwa katika Taarifa ya Wizara kuhusiana na utekelezaji operesheni hiyo.

 Pia alisema kamati ilitembelea maeneo yenye migogoro kati ya wakulima au wafugaji na wawekezaji katika maeneo ya hifadhi kwa lengo la kuhakiki (verify) masuala yaliyoainishwa kupitia uchambuzi uliofanywa na kamati. 

Kamati hiyo ilibaini vifo vilivyotokea wakati wa operesheni hiyo Kamati hiyo ilibaini mateso dhidi ya watuhumiwa yaliyosababisha maumivu, kupata ulemavu wa kudumu na hata wengine kupoteza maisha. 

Pia ilibaini matumizi mabaya ya silaha ambapo ilitoa mfano wa mzee wa miaka 70 kuuawa kwa kupigwa risasi tatu. “Nyumba za wananchi kuchomwa moto, mifugo kuuawa kikatili kwa kuchomwa moto na kupigwa risasi,” alisema. 

Mambo mengine ni kukosekana kwa mwongozo wa utoaji wa taarifa jambo lililosababisha viongozi husika wa Serikali kutopewa taarifa muhimu za utekelezaji wa operesheni. 

Alitoa mfano Waziri wa Maliasili na Utalii, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Waziri wa Ulinzi na Wakuu wa Mikoa na Wilaya. Pia askari waliotuhumiwa kukiuka taratibu kukataa kutoa ushirikiano wa kutosha pale walipohitajika kufanya hivyo.
  
 Na kutoshirikishwa kwa viongozi wa Mamlaka za Utawala katika ngazi za mikoa na wilaya. 
Spika wa Bunge, Anne Makinda, alitoa uamuzi wa kupeleka mgogoro kati ya wafugaji na wakulima, hifadhi na uwekezaji katika kamati hiyo kwenye Bunge la 13 mwaka huu.

 Uamuzi huo ulifuatia Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba, (CCM), aliomba mwongozo wa Spika wa Bunge. 
Kamati hiyo ilipewa kazi ya kutathmini na kuangalia jinsi Mpango wa Kupambana na Majangili ulivyopangwa na kutekelezwa na Serikali kupitia ‘Operesheni Tokomeza’.

 Kamati hiyo iliundwa na Lembeli, (Mwenyekiti wa Kamati hiyo), ilikuwa na wajumbe tisa ambao ni Abdulkarim Esmail Shah, (Mafia-CCM), Susan Kiwanga (Mbunge Viti Maalum-Chadema), Kaika Sanin’go Telele (Longido-CCM) na Dk. Henry Daffa Shekifu, (Lushoto-CCM). Wengine ni Amina Andrew Clement, (Koani-CCM), Haji Khatibu Kai (Micheweni-CUF), Muhammad Amour Chomboh, (Magomeni-CCM) na Dk. Mary Mwanjelwa (Viti Maalum-CCM).

No comments:

Post a Comment