Wednesday, October 23, 2013

Tukiamua, tunaweza. CHAGUA JAMAL MALINZI

Salamu kwa wapenzi, wachezaji na wadau wa michezo mliopo Tanzania na popote pale duniani.
Kwa muda mrefu nimekuwa mstari wa mbele katika michezo ambapo kati ya mwaka 1995 na 2001, DJB Promotions Ltd tuliweka historia ya ngumi za kulipwa nchini kwa kudhamini mabondia walionyakua mataji ya dunia akiwemo Rashid Matumla. 
Kati ya 1999 na 2005, nilishika nyadhifa mbalimbali Yanga zikiwemo seneta, mkurugenzi wa kuchaguliwa, kaimu katibu mtendaji na katibu mkuu. 

Nimekuwa mwenyekiti wa mashindano ya mpira wa miguu mkoa wa Pwani (2009 - 2011) na mjumbe wa Baraza la Michezo la Mkoa wa Dar es Salaam (2009-2012). 

Toka 2011 hadi sasa ni mjumbe kwenye Kamati ya Utendaji ya Chama cha Mpira wa Miguu wilaya ya Misenyi, pia mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Kagera.

Kwa sasa mimi Jamal Malinzi ni mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kagera, wadhifa nilioupata mwaka 2012 na tunaendela na utekelezaji wa programu ya vijana ya miaka mitatu 2013-16.
Raha ya mpira ni kelele na hoi hoi za mashabiki. 
Ziko wapi Ushirika Moshi, Bandari Mtwara, Kariakoo Lindi, Mirambo Tabora, Reli Morogoro, Lipuli FC Iringa, Tukuyu Stars Mbeya, Ujenzi Rukwa, Ndovu Arusha, Pamba Mwanza na nyinginezo?
Naomba tushikamane, tushirikiane, tujadiliane na ikibidi tusahihishane. Na nia yetu iwe moja tu, maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu humu nchini na kimataifa.

Panapo majaliwa, Oktoba 27, 2013 ni siku ya kihistoria ambapo Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) utafanyika jijini Dar es Salaam.

Watanzania wenzangu, mimi Jamal Malinzi, mgombea wa nafasi ya Urais wa TFF naomba baraka zenu ili tuwe na timu madhubuti ya kuipandisha Tanzania katika ulimwengu wa soka. 
Ndugu wanamichezo, wadau wa michezo na wale wote wenye kuitakia mema Tanzania - Tukiamua, tunaweza.
Jamal E. Malinzi
Oktoba 23, 2013

No comments:

Post a Comment