Saturday, June 15, 2013

MTAZAMO WANGU

Wakati mwingine ndugu zangu wadau hakuna ambaye hafurahii kukua kwa teknolijia hasa ya upashanaji habari kwa njia mbalimbali ambazo zitamsaidia mtu kufahamu matukio mbalimbali ambayo kimsingi yatamtoa hapo alipo na kuhabarika zaidi



Lakini hali hii ya kukua kwa kasi imekumbwa na maudhi ambayo nina uhakika si mimi peke yangu nimeyaona ila wapo waliotangulia na wakasema, lakini pia imefika zamu yangu kusema na nina imani kuwa hata wenzangu wanakumbana nayo ipo siku nao watasema

Ongezeko la mitandao tando (blogs) hakuna asiyejua kuwa ni msaada mkubwa wa kuwafikishia watu habari kama utatimiza malengo yako kwa kuwa ulipokuwa na mpango wa kufungua hiyo blog yako lazima ulikuwa na malengo ambayo bila shaka ulikaa chini na kuona kuwa utayamudu

Nichukulie mfano kwa nchi yetu ambayo ni kubwa, si kila habari unaweza kuipata kwa kufika eneo la tukio na ukaichukua kutoka kwenye vyanzo husika, labda uwe na waandishi wa habari katika mikoa ama wilaya zote za Tanzania, lakini kwa kuwa wamiliki wengi wa mitandao tando(blogs) hawana uwezo huo, inawalazimu kuchukua habari ambazo tayari zimewekwa kwenye mitandao ya mwanalibeneke mwenzako na kuziingiza kwenye blogs zao, kwa maana nyingine tunategemeana
Hili si tatizo bali nachoona mimi kuwa ni tatizo ni kuwa baadhi ya wanalibeneke(bloggers) wengi wanakosea hata “kucopy” na “kupaste” jambo ambalo limekuwa likiboa wasomaji wa blog zetu kwa kuwa unaweza kukuta habari moja imekosewa kwenye zaidi ya blog 50 ambazo zimeweka habari hiyo hiyo, jambo linaloshiria kuwa mtu ana copy habari na kuipaste kwake bila hata yeye mwenyewe kuisoma, sasa kama wewe huisomi na kuihariri je unataka nani aisome na kuirekebisha?

Na si hilo tu, pia si kila habari iliyopo kwenye blog ya mwenzako inatakiwa iwepo kwenye blog yako kwa kuwa kama ndiyo hivyo je ni kwa nini kusiwe na blog moja itakayokuwa na habari zote, kwa kuwa unakuta habari zilizoko kwenye blog moja ndiyo hizo hizo zipo katika blog zaidi ya 20 sasa unajiuliza tofauti za blog zetu kwa sasa ni majina ama ni nini? Ninaposema si kila habari lazima iwe kwenye blog yako namaanisha zipo habari ambazo mmiliki wa mtandao kazitafuta angalau kutofautisha blog yake na nyingine, mfano kakuta mifugo inazurura mitaani akaipiga picha na kuziweka kwenye blog yake, unakuta wamezinakili na kuziweka kwao, tena wakati mwingine bila hatimiliki ya mwenye picha ama ulipoinakili, sasa unajuuliza hivi wamiliki hawa hawajui kutofautisha habari za “kucopy” na za kuacha?

Huu si muda wa kuwaudhi wasomaji kwa kukuona kuwa huna ubunifu na namna ya kuelewa ni jinsi gani ya kunakili habari na habari ipi uiache, mfano rais akiwa na ziara sehemu fulani mathalani hapa nchini, lile ni tukio ambalo linatazamwa na nchi nzima kufahamu kinachoendelea na wanahabari wanaokuwa naye ndiyo tunaowategemea kwa habari za ziara hiyo, ambapo hata ukizinakili zinaleta mantiki, lakini usisahau kutoa hati miliki ya mwenye habari
Hebu tubadilike na tuone huu ni muda wa kutumia vizuri libeneke zetu ili zizidi kuwavutia watu, na kama unaona huwezi, hebu jifunze kwa wanaoweza wakuelekeze halafu uje kuendelea na kitu chenye ubora na mvuto kwa wasomaji

Ni hayo tu wadau

Edwin Moshi
EDDY BLOG

No comments:

Post a Comment