Monday, April 29, 2013

WADAU BUNDA WAOMBA KUANZISHA KITUO CHA UTALII


WADAU wa sekta ya utalii wilayani Bunda mkoani Mara,wameuomba uongozi wa wilaya hiyo kuanzisha kituo maalum cha utalii wilayani humo kitakachotumika kupokelea watalii watakaotembelea vivutio mbalimbali vilivyomo wilaya ya Bunda.

Wakichangia maoni yao kwenye kongamano maalum la kujadili jinsi gani wilaya hiyo inanufaika na utalii lililoandaliwa na chuo cha New Hope Utalii cha mjini Bunda,wadau hao wamesema kwa kufanya hivyo kutasaidia kukuza pato la ndani la wilaya hiyo inayoelezewa kuwa ya kwanza kwa umasikini nchini.

Wamesema utafiti wao unaonesha kuwa mapato mengi ya utalii unaotokana na hifadhi ya taifa ya Serengeti huwanufaisha zaidi watu wa nje na wilaya hiyo kutokana na wilaya ya Bunda kutokuweka miundombinu mizuri ya kuwavutia watalii ikiwa ni pamoja na kituo maalum cha
kuwapokelea na kuwatembeza.

Wametaja baadhi ya vivutio vya utalii vilivyomo ndani ya wilaya hiyo na ambavyo haivitumii kuwa ni Ziwa Victoria na maajabu yake zikiwamo fukwe na mawe ya ajabu, maajabu ya mlima Chamriho,hifadhi ya taifa ya Serengeti,mila na desturi ya baadhi ya makabila na kazi mbalimbali za sanaa.

Akihitimisha maoni ya wadau hao mkurugenzi wa taasisi binafsi ya
Giraffe ya mjini Musoma inayojishughulisha na Uhifadhi wa Mistu na Maendeleo ya jamii Bw Donny Shule,amesema ni wajibu wa Serikali ya wilaya hiyo kujenga miundombinu mizuri ya kitalii itakayowezesha kupata mapato na kuwaomba watendaji wa wilaya hiyo kuwa wabunifu.

No comments:

Post a Comment