Bendi ya Jeshi la Polisi Tanzania ikiwajibika katika mahafali hayo
Baadhi ya wafanyakazi wa TGNP wakiwa katika mahafali
Bendi ya Polisi ikiwajibika
Maandamano mgeni rasmi na viongozi wa GTI na TGNP
Maandamano ya mgeni rasmi na viongozi wa GTI na TGNP
Mgeni rasmi, John Mnyika akizungumza
Mmoja wa wahitimu wakitunukiwa cheti cha mafunzo ya GTI na mgeni rasmi, John Mnyika
Mwenyekiti wa Bodi ya GTI,Marry Rusimbi akihutubia
Na Joachim Mushi
MBUNGE
wa Jimbo la Ubungo kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), John Mnyika ameahidi kumsomesha mwanafunzi bora wa Chuo cha
Jinsia (GTI) kupitia sehemu ya mshahara wake wa ubunge.
Mbunge huyo alitoa ahadi hiyo jana jijini Dar es Salaam katika
sherehe za Mahafali ya Kwanza ya Chuo cha Jinsia, GTI alipokuwa mgeni
rasmi. Alisema anatambua mchango wa chuo hicho katika kuiandaa jamii
kupigania usawa wa rasilimali za taifa, hivyo kupitia mshahara wake wa
ubunge atatoa mchango wa kumlipia ada mwanafunzi bora wa chuo hicho
mwakani.
Mbunge huyo aliupongeza uongozi wa GTI kwa mafanikio waliofikia ya
kuanzisha chuo kinachotoa mafunzo ya jinsia kwa jamii na kushauri
uongozi kujipanga na kuwasilisha ombi la kuomba fungu la fedha kutoka
Mfuko wa Mbunge wa Maendeleo wa Jimbo ili kukiwezesha chuo hicho kufanya
shughuli zake kiufanisi.
Awali akizungumza katika mahafali hayo, Mkuu wa Chuo cha GTI, Dk.
Diana-Bupe Mwiru alisema mahafali hayo ni ya kihistoria kutokana na
kwamba yanafanyika kipindi ambacho Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP)
ambao ni wamiliki wa chuo hicho wakisherehekea miaka 20 tangu kuanzishwa
kwa taasisi hiyo.
"TGNP inasherehekea miaka 20 ya harakati za ukombozi wa mwanamke
kimapinduzi dai kuu likiwa rasilimali za nchi kunufaisha watu wote na
hasa wale walioko pembezoni. Mwanamke wa kitanzania amekuwa miongoni mwa
makundi yaliyoko pembezoni kutokana na mila na sheria kandamizi ambazo
zilishindwa kutambua mchango wa mwanamke katika jamii na majukumu
makubwa ambayo ameyabeba ili kuhakikisha kuwa jamii inaendelea kuwepo,"
alisema Dk. Mwiru.
Aliongeza kuwa GTI tangu kuanzishwa kwake imekuwa ikitoa mafunzo kwa
umahiri mkubwa katika soko la ndani na nchi za jirani, huku kikiwa
kimefundisha washiriki zaidi ya 6000 kutoka nchi za Msumbiji, Nigeria,
Malawi, zambia, Kenya, rwanda, Uganda, Ethiopia, Norway pamoja na
Tanzania yenyewe.
"Kutokana na umahiri wake katika kutoa mafunzo GTI imeweza
kutambuliwa kimataifa kama chuo kilichotukuka katika kutoa maarifa na
stadi katika nyanja ya jinsia na maendeleo kwa Afrika Mashariki na Kati.
Kwa GTI hii ni hatua ya mafanikio ambayo tuna kila sababu ya
kujivunia," alisema Mkuu wa Chuo hicho.
Aidha Dk. Mwiru alitoa shukrani kwa mashirika mfadhili wa GTI ambayo
ni 'Foundation for Civil Society, UN Women, UNFPA, Deloitte, Action Aid
na SIDA kupitia TGNP na RATN ambayo yamekuwa sehemu ya mafanikio ya
chuo hicho. Ikiwa ni pamoja na kuiomba Serikali pamoja na taasisi zake
nayo kuanza kukitumia chuo hicho.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Bodi ya
GTI, Profesa Saida Othman aliiomba Serikali kushughulikia changamoto ya
ubora wa elimu kiujumla kwani matokeo yanavyokuwa mabaya hata vyuo
vinavyotegemea wanafunzi hukosa wanafunzi wenye sifa kujiunga na vyuo
hivyo.
Jumla ya wahitimu wa 11 walifanikiwa kutunukiwa vyeti vya mafunzo ya jinsia katika mahafali hayo ya kwanza.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com.
No comments:
Post a Comment