Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Lugola alisema
sababu ya kibano alichopata ndani ya CCM ni kutokana na kauli aliyotoa
hivi karibuni mkoani Iringa ya kumuunga mkono Waziri Mkuu aliyejiuzulu,
Edward Lowassa.
“Wabunge wa CCM tunaoikosoa serikali na kuzigomea bajeti tuko wengi,
kwanini ndani ya kikao wametubana mimi na Deo tu? Mimi nadhani ile ziara
tuliyoifanya hivi karibuni kumsindikiza Lowassa mkoani Iringa ndiyo
imeleta shida yote hii,” alisema.
Mbunge huyo machachari bungeni, alisema pamoja na maneno na vitisho
alivyotolewa ndani ya kikao hicho na baadhi ya mawaziri na wabunge
wenzake wa CCM, kamwe hawezi kuogopa.
Alisema hatua ya kutaka kunyamazishana, hakubaliani nayo bali
anaendelea na kasi yake ya kuibana serikali pale anapoona dhahiri kwamba
inakosea.
“Mimi siogopi maneno, hata kifo chenyewe pia sikiogopi. Nitasimamia
ukweli, CCM ni chama changu na serikali ni yangu na naitakia mema ndiyo
maana nipo tayari kufa kwa kusimamia ukweli huo,” alisema.
Hivi karibuni Lowassa aliambatana na wabunge hao mkoani Iringa
ambako alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuchangisha fedha kwa ajili
ya ujenzi wa kanisa na kituo cha redio cha Overcomers Power Centre (OPC)
mjini Iringa.
Katika hafla hiyo alitunukiwa tuzo maalumu kutokana na jitihada zake za kuitumikia na kuisaida jamii nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo, Lugola aliwashangaa watu wanaowalaumu
wanasiasa kwa kuingia makanisani na kusema kuwa kazi wanazozifanya
hazina tofauti na za viongozi wa dini.
Lugola alifananisha matukio yaliyomkuta Lowassa sawa na matatizo yaliyomkuta Bwaba Yesu wakati alipokuwa anahubiri duniani.
Alimmwagia sifa Lowassa kuwa licha ya maneno mengi yanayosemwa juu
yake, lakini bado ameendelea kuitumikia jamii kupitia siasa na shughuli
za kidini.
Alisema kuwa kama ilivyokuwa kwa Yesu ambaye alipigwa na kunyanyaswa
na kuyaacha yote kwa Mungu, Lowassa naye aliandamwa na waliomzushia kesi
kiasi cha kuamua kujiuzulu uwaziri mkuu.
“Mnakumbuka kuwa waliomchukia Yesu walimfungulia mashtaka ya uongo
wakamfikisha mbele ya pilato. Walipoambiwa watoe ushahidi wakashindwa,
lakini wakapiga kelele asulubiwe. Yesu alipigwa, akatemewa mate, lakini
yeye akasema ‘ikiwezekana kikombe hiki kiniepuke lakini si kama
nitakavyo mimi bali mapenzi ya Mungu yatimizwe’.
“Vivyo hivyo Edward, aliposakamwa sana aliamua kujiuzulu uwaziri
mkuu...lakini tunajua kuwa Yesu, baada ya kuuawa, alifufuka na
kuinuliwa. Naomba kanisa liendelee kumuombea Lowassa ili naye ainuliwe
juu katika nchi yetu ya Tanzania,” alisema Lugola.
Filikunjombe naye alimwaga sifa kwa Lowassa akimtaka kutokatishwa
tamaa na maneno yanayosemwa, na kuongeza kuwa siku zote mti wenye
matunda ndio unaopigwa mawe.
Wiki iliyopita katika kikao cha Kamati ya Wabunge wa CCM, Lugola na
Filikunjombe walisutwa kutokana na mwenendo wa kuikosoa serikali na
kuwashambulia mawaziri.
Mbunge aliyewawashia moto wabunge hao ni Said Nkumba wa Sikonge ambaye alihoji mwenendo wao.
Mbele ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Mkumba alisema kuwa wabunge hao
wanatumika na CHADEMA na kuwataka waamue kama wanabaki CCM au la.
Hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge wengi, huku mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde akitolea mfano wake.
Naibu Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Adam Malima naye alimbana
Lugola ataje majina ya mawaziri alioliambia Bunge kwamba wanauza unga.
Tanzania Daima
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment