Wednesday, December 12, 2012

Walimu waiomba Serikali itenge bajeti kuboresha elimu za awali


Na Mwandishi wa Thehabari Korogwe Vijijini

BAADHI ya walimu na wazazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe wameiomba Serikali kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya kuboresha elimu ya awali ili madarasa hayo yasiwe mzigo kwa walimu wakuu.



Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi eneo hilo umebaini licha ya Serikali kusisitiza kila shule ya msingi kuwa na darasa la awali, baadhi ya maeneo haitoi fungu lolote kuendesha madarasa hayo.

Akizungumza hivi karibuni ofisini kwake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kwagunda, David Kituja iliyopo Kijiji cha Kwagunda Korogwe, alisema darasa la awali shuleni hapo hutumia bajeti ile ile ya shule ya msingi, jambo ambalo limekuwa mzigo kwa walimu wakuu hivyo kushauri kuongeza fungu kuboresha darasa hilo.

“Madarasa ya awali kweli ni tatizo, maana inasikitisha Serikali inasisitiza yaanzishwe kwa kila shule lakini hakuna bajeti yoyote iliyotengwa kuyahudumia...mwalimu unalazimika kubana upande wa bajeti ya msingi uitumie kwenye darasa la awali sasa hii ni changamoto kweli kweli,” alisema Kituja.

Kwa upande wake, mmoja wa wazazi, Vedastus Mhilu alisema, changamoto ya kipato kwa wazazi wengi vijijini bado ni tatizo kubwa kwa uchangiaji wa madarasa hayo jambo ambalo husababisha elimu hiyo kuendeshwa kwa kubabaisha.

“...Huku wazazi wengi ni wakulima kwa hiyo ile fedha tunayoipata haitoshelezi kuwapeleka watoto wetu kusoma madarasa ya awali au kuchangia ada na hata michango ya chakula, si kwamba hatupendi watoto wetu wapitie elimu hiyo ya awali tatizo ni kipato,” alisema Mhilu.

Aidha Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kwashemshi, Jonathan Mzava alisema kwa upande wao wameweza kuanzisha madarasa ya awali kwa ushirikiano na Serikali lakini kikwazo ni namna ya kupata walimu wa kudumu kuwafundisha watoto hao muda wote.

“Hapa shuleni ninao wanafunzi kama 100 hivi wa elimu ya awali, madarasa haya yanaendeshwa kwa msaada wa Serikali ila mwakani nafikiria kuwashirikisha wazazi ili tuweze kuiboresha zaidi...nitawaomba wachangie kiasi kidogo ili tuweze kupata walimu ambao muda wote watakuwa wanawafundisha watoto tofauti na sasa ambapo natumia walimu wa shule ya msingi,” alisema Mzava.

Akizungumzia kuhusu elimu ya awali, Kaimu Ofisa Elimu Sekondari, Shaban Shemzighwa alisema hakuna walimu wanaoajiriwa maalumu kama walimu wa madarasa ya awali hadi sasa, hivyo shule zenyewe hujitegemea kimgawanyo wa walimu kuendesha elimu hiyo.

*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa kushirikiana na HakiElimu

No comments:

Post a Comment