Tuesday, November 27, 2012

WAFANYABIASHARA WA DAR WATIWA MBARONI ZANZIBAR WAKIWA NA MADAWA YA KULEVYA KIBAO

Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi Zanzibar
 
Wafanyabiashara wawili wa Jijini Dar es Salaam, wametiwa mbaroni Visiwani Zanzibar baada ya kupatikana wakiingiza madawa ya kulevya kwa njia ya majini.

Naibu Mkurugenzi wa makosa ya Jinai Zanzibar ACP Yusuf Ilembo, amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Othuman Chande Othmani (22) mkazi wa Kinondoni na Abubakari Muharami Bakari(33) mkazi wa Temeke.

Kamanda Ilembo amesem,a kuwa watuhumiwa hao wote wamekamatwa katika Bandari ya Zanzibar walipokuwa wakiwasili kwa boti kutoka Dar es Salaam wakiwa na madawa hayo ya kulevya aina ya Heroine.

Amesema kuwa Mtuhumiwa Abubakari alikamatwa juzi saa 3.00 asubuhi akiwa na kifurushi kimoja likichokuwa na madawa hayo ambapo mwenzake Othman yeye ametiwa nguvuni leo saa 3.00 asubuhi akiwa na vifurushi viwili vya madawa hayo aina ya Heroine.

Kamanda Ilembo amesema kukamatwa kwa watuhumiwa  hao kunatokana na kuimarishwa kwa ulinzi na upekuzi wa hali ya juu uliopo katika maeneo ya viwanja vya ndege na bandari ya Zanzibar.

Amesema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zao za kupatikana na madawa ya kulevywa visiwani hapa.

Amewataka wananchi wakiwemo wasafiri wa ndege na boti wanaoingia na kutoka katika visiwa vya Unguja na Pemba kuacha kulalama na kuona kuwa wanapopekuliwa wanabughudhiwa.

Ammesema maeneo yote ya Viwanja vya Ndege na Bandarini Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Maafisa wengine wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama vimeimarisha ulinzi ili kuhakikisha kuwa hakuna kitu cha hatari kinachoingizwa Visiwani humo.

Mbali ya Madawa ya kulevya na silaha, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepiga mariufuku uingizwaji wa mifuko ya plastiki ya aina zote na kwamba kwa yeyote atakayepatikana na mfuko wa plastiki atakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Kwa siku za hivi karibuni baadhi ya wasafiri wamekuwa wakilalamikia hali ya upekuzi unaoendeshwa katika maeneo ya Viwanja vya Ndege na Bandari na hali wanayoona kuwa ni usumbufu kwao.

No comments:

Post a Comment