Nimewahi kuuliza waandishi wa habari wawili, mmoja toka Kenya na
mwingine Mtanzania, swali moja: raia wanaamini yuko kiongozi ambaye si
mwizi? Mkenya alisema Wakenya wote wanaamini kuwa viongozi wao siyo
waaminifu. Mtanzania naye alisema Watanzania wengi zaidi nao wanaamini
kuwa viongozi wetu siyo waaminifu.
Madhumuni ya msingi ya kutoa elimu ni kumwezesha mwanafunzi kusoma,
kuhesabu, na kuandika. Madhumuni mengine ya muhimu ni kumwezesha
mwanafunzi kuwa mdadisi, mchambuzi, mwenye uwezo wa kufikiri, na hata
mwenye uwezo ya kupinga kwa hoja yale ambayo anafundishwa. Pengine hili
la pili lingeweza kuwa muhimu kuliko lile la kwanza kama isingekuwa
haiwezekani kupata uwezo huu wa pili bila kuwa na uwezo wa kusoma,
kuhesabu, na kuandika.
Hali duni ya elimu iliyopo sasa inatoa nafasi ndogo sana kwa
wanafunzi kuvuka ngazi ya kwanza na kuingia ngazi ya pili. Tunao
wanafunzi wa sekondari wasiokuwa na uwezo wa kusoma na kuandika. Tunao
wahitimu wa elimu ya juu ambao hawana uwezo wa kuridhisha kulinganisha
na wenzao waliosoma miaka ya sitini na ya sabini.
Maisha ya baadaye ya hawa watoto yatakosa amani iwapo mfumo wa elimu
hautaboreshwa.Leo hii wanaopta elimu nzuri ni asilimia ndogo sana ya
mamilioni ya Watanzania ambao wanapata elimu hafifu. Kwa sababu hii kila
mwaka ongeko la Watanzania wenye uwezo wa kuchambua, kutafakari,
kudadisi, na kupinga kwa hoja masuala mbabali mbali wanazidi kupunguka
na tena kwa kasi kubwa.
Siasa ya vyama vingi imefanikiwa kifuchua maovu mengi ya siasa za
chama kimoja, lakini pia vyama vingi vimejenga pia imani kwa mwananchi
wa kawaida kuwa kila mtu ni mwizi. Juzu juzi nimetoka kupanda Mlima
Kilimanjaro na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Loreto na
nilimsikia mmoja wao akisema kuwa “kila mtu ni mwizi.”
Hatuwezi kuacha kulaumu mienendo ya baadhi ya viongozi wetu ambayo
inawafanya raia waamini kuwa viongozi wa umma waaminifu hawapo tena.
Elimu hafifu inapunguza uwezo wa raia wa kuchambua masuala mbali
mbali, lakini siasa ya vyama vingi imefanya kazi nzuri ya kumfanya raia
ashuku kila kitu na kila mtu. Kwa taratibu za kisheria za mfumo wa
sheria unaojulikana kama civil law ni wajibu wa yule
anayetuhumiwa kuthibitisha kuwa siyo mwizi, au hafanyi janja janja ya
aina fulani anapokuwa kiongozi au mtumishi wa umma.
Hatari ya hali hii ni kuwa hata pale jambo linapokuwa halina mizengwe
ni vigumu kwa raia kuamini hivyo. Raia wanapokuwa hawana tena imani na
viongozi na mfumo wa utawala, misingi ya amani itaanza kupata nyufa. Na
matukio ya miaka ya hivi karibuni yanaashiria kuwa miaka ijayo haitakuwa
na amani ambayo Watanzania wamekuwa nayo kwa muda mrefu.
—Madaraka via Muhunda blog
No comments:
Post a Comment