Thursday, November 1, 2012

IGP MWEMA AAGIZA WALIOSHIRIKI VURUGU ZANZIBAR WASAKWE KWA UDI NA UVUMBA

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali Saidi Mwema, ameagiza kukamatwa kwa wale wote walioshiriki katika vurugu zilizopelekea uporaji na uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu ya barabara za mjini wa Zanzibar, wasakwe na kukamatwa ili wafikishwe mahakamani.
Kwa mujibu wa Afisa Habari Mkuu wa Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina, IGP Mwema ametoa agizo hilo mjini Zanzibar wakati akizungumza kwenye baraza la Askari lililohudhuriwa pia na Makamanda wa Polisi wa mikoa mitatu ya Unjuja  kuhusiana na vurugu zilizotokea mwezi uliopita na kupelekea kifo cha Askari Koplo Saidi Abdarahamani Juma.
Akizungumzia kuuawa kwa Askari Koplo Saidi, IGP Mwema amesema mtu yeyote aliyeshiriki katika vitendo hivyo ambavyo vimepelekea taathira kubwa ya uvunjifu wa amani katika mji wa Zanzibar na viunga vyake, ni lazima apelelezwe na popote alipo akamatwe ili sheria ichukue mkondo wake.
Amesema kumuua Askari mmoja ni sawa na kuathiri huduma za kiusalama kwa watu zaidi ya 1,300 na kwa nafasi ya askari mwenye cheo cha Koplo kama Marehemu Saidi, mwenye uwezo wa kuongoza Askari wenzake wanane hadi kumi, atakuwa amewanyima haki watu wengine zaidi ya watu 13,000 kutokana na vitendo vya uhalifu.
IGP Mwema amepongeza ushirikiano uliopo baina ya Askari Polisi na Askari na maafisa wa Vyombo vingine vya ulinzi na usalama na kusema kuwa ushirikiano huo ndio ulioleta mafanikio ya kuwakamata washiriki wa makosa na hatimaye kuleta ushwari katika kisiwa cha Zanzibar.
Amesema nia ya Serikali ya kusajili vikundi mbalimbali vikiwemo vya kidini, ni kutaka kuleta maendeleo ya kiuchumi, ustawi wa Jamii na maendeleo ya kiusalama na kudumisha amani na utulivu wa taifa letu na kwamba hakuna Serikali yoyote Duniani inayoweza kuruhusu vikundi kama hivyo vigeuke kuwa vyenye kuleta vurugu na machafuko ya taifa husika.
Amesema amefurahishwa na kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein, za kuwatia moyo askari na kukemea vikali vitendo vya vurugu za kidini zilizopelekea machafuko visiwani zanzibar na Dar es Salaam.
Awali Kamishna wa Polisi Zanzibar CP. Mussa Ali Mussa, amesema kuwa Jeshi la Polisi visiwani hapa linafanya operesheni ya kisayansi ya kuwasaka na kuwanasa wale wote waliohusika katika vurugu za hivi karibuni na zile zilizopita kwa kutumia picha za kawaida na za video ili kumbaini kila mtu aliyeshiriki katika matukio hayo.
Kamishna Mussa amesema hadi sasa watuhumiwa 98 wamekamatwa na 35 kati yao wamefikishwa Mahakamani na wengine wanaendelea kuhojiwa na watakaothibitika kushiriki katika matukio hayo watafikishwa mahakamani kuunganishwa na wenzao.
Amesema tayari Makachero wa Jeshi Polisi wamepata picha 72 pamoja na CD na DVD zenye kuonyesha sura za washiriki wa vurugu katika maeneo mbalimbali ya mji wa Zanzibar na shughuli ya uchambuzi na utambuzi wa kuwabaini na maeneo wanaoishi inaendelea na kila atakayebainika atakamatwa na kufikishwa mahakamani.
Amesema picha hizo zimesambazwa katika vituo mbalimbali vya Polisi na ofisi za Vikosi vya usalama Zanzibar pamoja na vyombo vya Habari ili kuwafuatilia na kuwakamata wahusika hao kwa hatua zaidi.

No comments:

Post a Comment