WAKUU WA MAJESHI YA POLISI KUTOKA NCHI ZA SADC KUKUTANA ZANZIBAR KUWEKA MIKAKATI YA KUKABILI UHALIFU WA KIMATAIFA
Mratibu
wa maandalizi ya mkutano huo ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha
Shirikisho la Polisi wa Kimataifa Duniani (INTERPOL) nchini Tanzania,
Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Gustavus Babile, amesema kuwa mkutano
huo wa siku tatu ambao utafanyika mwanzoni mwa mwezi ujao, utatanguliwa
na mikutano mingine midogo midogo ya kamati tendaji (Technical Organs)
kutoka nchi wanachama.
Kamanda
Babile amesema maandalizi ya mkutano huo utakaoanza Septemba 3 hadi 5,
mwaka huu, yapo katika hatua za mwisho na kwamba tayari Wakuu wa Majeshi
ya Polisi kutoka nchi 11 kati ya 14 wanachama wa Shirikisho hilo la
Wakuu wa Majeshi ya Polisi kwa nchi za Kusini mwa Afrika. Yaani Southern
African Region Police Chiefs Co-Opereratio Organization (SARPCCO) wamethibitisha kushiriki.
Amesema Wakuu wa Majeshi ya Polisi waliothibisha kushiriki katika mkutano huo ni kutoka Afrika ya Kusini, Botswana, Namibia, Swaziland, Lesotho, Malawi, Msumbiji, Congo DRC, Zambia, Zimbabwe na wenyeji Tanzania.
Amesema
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Angola Kamishna Jenerali Ferire Do
Santos Ambrosio De Lemos, atatuma mwakilishi kwenye mkutano huo kutokana
na nchi hiyo kukabiliwa na uchaguzi mkuu wa vyama vingi ambao
utafanyika katika siku za hivi karibuni.
Kamanda Babile amesema ofisi yake bado inaendelea kuwasiliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Mauritius, Kamishna
Jenerali Rampersad Dhun ili kuthibitisha ushiriki wake yeye pamoja na
wajumbe wengine wanaopaswa kuwepo kwenye mkutano huo.
Mbali
ya Wakuu hao wa Majeshi ya Polisi kutoka nchi za SADC, pia Kamanda
Babile amewataja Wajumbe wengine wanaopaswa kuwepo kwenye mkutano huo
kuwa ni pamoja na Wakurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai kutoka
nchi wanachama ambao nao watawaongoza Wataalamu Viongozi katika Vitengo
mbalimbali vya Majeshi hayo ya Polisi kutoka katika nchi shiriki.
Wataalamu
hao ni pamoja na Wakuu wa Vitengo vya Sheria, Wakuu wa Mafunzo, Wakuu
wa Mitandao ya Wanawake, Wakuu wa Maabara ya Uchunguzi wa Vielelezo,
Wakuu wa Udhibiti wa Silaha ndogondogo na za rashasha, Wakuu wa Vikosi
vya Afya na Utabibu, Wakuu wa Mifumo ya Kompyuta pamoja na Wakuu wa
Vitengo vya Interpol kutoka kila nchi wanachama.
Amesema,
pamoja na mambo mengine, wajumbe wa mkutano huo pia watajadili,
kubadilishana uzoefu wa kiutendaji na hatimaye mbinu na mikakati ya
pamoja itakayosaidia kukabiliana na makosa yenye athali kwa maisha ya
binadamu na yale yanayodhoofisha nguvu za kiuchumi kwa nchi za Kiafrika
na duniani kwa ujumla.
Ameyataja
makosa hayo kuwa ni pamoja na Ugaidi, Uharamia, Usafirishaji haramu wa
binadamu, Biashara haramu ya Madawa ya kulevya, makosa ambayo amesema
yana athali za moja kwa moja kwa binadamu.
Ameyataja
baadhi ya Makosa yanayothoofisha nguvu za kiuchumi Duniani ambayo pia
yatajadiliwa kwenye mkutano huo kuwa ni ya hujuma na wizi wa fedha
kutoka kwenye mabenki na taasisi nyingine za kifedha unaofanywa kwa
kutumia mifumo huru ya kompyuta.
Makosa
mengine ni ya wizi na usafirishaji wa magari na mifugo kutoka nchi moja
kwenda nyingine kwa magendo pamoja na uwekezaji wa miradi mikubwa ya
kiuchumi itokanayo na fedha za biashara haramu.
Hata
hivyo, Kamnda Babile ameyataja mambo mengine yatakayofanyika wakati wa
mkutano huo kuwa ni pamoja na uchaguzi wa Mwenyekiti mpya wa Shirikisho
hilo la SARPCCO ambapo Mkuu wa Jeshi la Polisi hapa nchini Inspekta
Jenerali Saidi Ali Mwema, anapewa nafasi kubwa ya kushika wadhifa huo
baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Afrika ya Kusini Kamishna
Jenerali Bi. Mangwashi Phiyega, kumaliza muda wake katika nafasi hiyo.
Kamanda
babile amesema. Endapo IGP Mwema, atachaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa
Shirikisho hilo la SARPCCO, itakuwa ni mara ya pili kwa Jeshi la Polisi
nchini Tanzania kushikilia tena nafasi hiyo kubwa ya Mashirikisho ya
Kimataifa Duniani.
Kwa
mara ya kwanza Tanzania ilipata nafasi hiyo mwaka 2004 na 2005 kupitia
kwa aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi hapa nchini Inspekta Jenerali
Mstaafu Omari Iddi Mahita.
IGP
Mstaafu Mahita, aliweka historia ya kuwa Mkuu wa kwanza wa Jeshi la
Polisi hapa nchini kuwaongoza Wakuu wa Majeshi ya Polisi kwa nchi za
Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika kupitia Shirikisho hilo kubwa
la (SARPCCO) tangu lilipoanzishwa mnamo mwaka 1995, katika mji wa
Swakompumg nchini Namibia.
“Ingawa
mkutano huo utazungumzia zaidi masuala ya kiusalama, lakini pia ni
fursa pekee kwa Visiwa vya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kutangaza na
kukuza vivutio vyake vya kitalii kutokana na ujio wa wageni wengi kutoka
mataifa mbalimbali duniani”. Alisema Kamanda Babile.
Amesema
huo ni wakati wa wafanya biashara kufanya biashara zaidi na hata kupata
nafasi ya masoko nje ya nchi kutokana na bidhaa zinazozaliswa ama
kutengenezwa hapa nchini.
Amesema,
hata baada ya kumalizika kwa mkutano huo, kuna uhakika kuwa baadhi ya
washiriki hasa wale wa Mashirika ya Kimataifa, watapenda kuendelea
kubaki Zanzibar kutembelea fukwe za Bahari na kuona maeneo ya
mbalimbali ambayo ni vivutio kwa wageni yakiwemo yale ya mji Mkongwe
yenye historia ya muda mrefu Ulimwenguni.
Zaidi
ya wajumbe 250 kutoka nchi za SADC pamoja na wa Mashirika mbalimbali ya
Kimataifa duniani, wanatarajiwa kushiriki katika mkutano huo.
No comments:
Post a Comment