Saturday, July 21, 2012

WANANCHI WA VIJIJI V3 VYA  BUHEMBA KUISHTAKI SERIKALI UMOJA WA MATAIFA
   Hizi ni baadhi ya picha zaidi ya 30 kutoka Mgodi wa Buhemba ambao umeacha kilio kwa wananchi wa eneo hilo

         Diwani wa kata ya Buhemba Boniphace Masero akifafanua jambo kwa waandishi wa habari
      Pasto wa Kanisa la Anglikana Samweli Nyakarungu akifafanua jambo
       Mama huyu alisema kuwa tatizo la Maji limekuwa kubwa baada ya kufika kwa wawekezaji hao


Augustine Mgendi

BUHEMBA

WANANCHI vijiji Vitatu wanaozungukwa na Mgodi wa Buhemba  wilaya ya Butiama mkoani Mara wamesema kuwa wanakusudia kuishitaki Serikali ya Tanzania katika Taasisi za Umoja wa Mataifa zinazohusika na haki za binadamu  ikiwa ni shinikizo la kulipwa fidia ya shilingi Bilioni 30.

Mbali na kusudio hilo la kuelekea umoja wa Mataifa lakini pia wananchi hao wamesema kuwa wanakusudia kumuona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete kumueleza madhara yaliyosababishwa na Mgodi huo ambao ulidaiwa kumilikiwa na Serikali kupitia Kampuni ya Meremeta. 

Wananchi hao kutoka vijiji vya Tarani,Biatika na Magunga huku wakiomba Wabunge kuungana na kutoipitisha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini had hapo Serikali itakapo wafidia.   

Akiongea na waandishi habari katika eneo hilo la Buhemba,Diwani wa kata ya Buhemba Boniphace Masero amesema kuwa Mgodi huo umeachia athari kubwa kutokana na machimbo yaliyoachwa kuleta athari kubwa huku Ardhi yao ikiwa haina rutuba kutokana na Kemikali zilizomwagwa katika eneo hilo

Amesema athari zingine zilizoletwa na Mgodi huo ni pamoja na Shule iliyokuwa katika eneo hilo kubomolewa lakini walishindwa kuijenga kama walivyokuwa wameahidi wahuska hao wa mgodi huku miundombinu ya barabara nao ikiwa haifai kutumika.

“Huu Mgodi umetuachia madhara makubwa sana maana Mashimo hayakufukiwa,Milima inaleta uchafuzi wa Mazingira,shule iliyokuwa imejengwa hapa ilibomolewa,Nyumba zikabomoka kutokana na Baruti za mgodi,katika hili sisi tunakusudia kumuona Rais ili tumueleze haya Manyanyaso tunayoyapata” alisema diwani huyo

Diwani Masero ameongeza kuwa athari nyingine ni pamoja na baadhi nyumba za wakazi wa eneo hilo kubomoka kutokana na baruti zilizokuwa zikipigwa katika Mgodi huo lakini mpaka sasa hawajalipwa fidia na hivyo wanawaomba Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoipitisha Bajeti ya wizara ya Nishati na Madini mpaka walipwe fidia yao

Aidha Pasta wa Kanisa la Anglikana Samweli Nyakarungu alisema kuwa mgodi huo wa Buhemba ulikuwa ni Mgodi wa kitapeli ambapo wahusika hao wamechuma raslimali za Taifa na kushindwa kufanya shughuli za Maendeleo katika Jamii. 

Pasta Nyakarungu alisema kuwa mbali na wawekezaji hao wa Kitapeli kuiba mali ya Watanzania lakini pia wamesababisha madhara makubwa kwa jamii ya Buhemba kwa kushindwa kujenga miundombinu ya barabara,kujenga shule kama inavyotakiwa.

Kutoka na adha hiyo Pasta huyo alisema kuwa Serikali imeshindwa kuwajali wananchi wake na hivyo wanawaomba Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kutoipitisha Wizara ya nishati na Madini mpaka hapo wananchi wa eneo hilo watakapopata fidia yao. 

  “Hawa wawekezaji mimi naona hawakuja hapa kwa lengo la kumsaidia mtu wa Buhemba huu Mgodi naona ulikuwa wa Kitapeli kabisa,wamechuma raslimali za Taifa na kushindwa kumsaidia mtu anayezungukwa na mgodi na hata kurekebisha miundombinu huska na hii inaonyesha jinsi Serikali isivyojali wananchi wake” alisema Pasta Nyakarungu

Naye Mwalimu mstaafu Sita Nyamhanga na bi Hadja Yasini walisema kuwa mgodi huo umewaachia matatizo makubwa ikilinganishwa walivyokuwa wameahidiwa wakati wanaanza uchimbaji katika mgodi huo.

  “Tunavyojua ni kwamba wawekezaji wanapowekeza eneo lolote lazima watu wanaozungukwa na Mgodi ule wanufaike lakini hapa Buhemba sisi wananchi ndiyo tumepat tabu kabisa kwani mpaka sasa hatuna shule,barabara inayopitika muda wote,eneo letu limebaki Jangwa huku wakina mama wanapata tabu kutafuta maji kutokana na vyanzo vingi vya maji kuchafuliwa na mgodi” alisema Mwalimu mstaafu huyo.

Kwa upande wake Bi Hadja Yasini alisema kuwa wanapata tabu hata kutafuta kuni kutokana na eneo kubwa la Buhemba kubaki Jangwa tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Kulingana na adha hiyo Bi Hadja alisema kuwa ni vyema Waziri mwenye dhama huska akawasaidia watu wa Buhemba ili waweze kupata fidia zao kutokana na madhara waliyoyapata kutokana na mgodi huo.

Mgodi wa Buhemba ambao ulianza kuchimbwa mwaka 2002 ni moja ya mgodi ambao ulikuwa ni mkubwa hapa nchini ukielezwa kumilikiwa na Serikali na kufungwa mwaka 2006 huku ukiacha eneo hilo la Buhemba kupoteza rutuba yake na hivyo wananchi kushindwa kuendesha shughuli za Kilimo.

No comments:

Post a Comment