Ikiwa Leo ndiyo mazishi ya mwl James Irenge aliyemfundisha hayati Baba wa Taifa Mwl
Julius Kambarage Nyerere na hii ni moja ya Makala ambayo nimewahi kuandika
baada ya kufanya mahojiano na Mwl James Irenge mwezi October mwaka 2010
Mungu aiweke roho ya Mwl Irenge Mahali pema
peponi
Soma alichokisema Mwl
Irenge
VIONGOZI WETU LEO NI KAMA WAKOLONI WEUSI
LEO Oktoba14 mwaka 2010 wananchi wa
Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla wanakumbuka miaka 11 tangu kufariki Baba
wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mtetezi wa wanyonge.
Katika jambo lolote,kitu chochote au
mtu yeyeto ambaye amewahikutenda jambo jemana jamii ikalikubali ni vigumu
kusahaulika na ndio maana leo kama ilivyo kwa watanzania kumsahau mwalimu
Nyerere baada ya kifo chake kwa miaka 11
Katika miaka kumi na moja ya kifo
chake watanzania bado wanasema kuna pengo kubwa ambalo kamwe ni vigumu kuzibika
kwani hajatokea kiongozi ambaye anaweza kufananishwa naye hasa katika kutetea
haki za wananchi wake na bara la Afrika kwa ujumla.
Mmiliki wa blog ya Mwana wa Afrika akifanya mahoniano na Mwl Irenge enzi za uhai wake
Na kama leo tutawaeleza watanzania
nin wangapi ambao wanakumbuka kwa vitendo yale aliyotenda Baba wa Taifa ni
vigumu kumkosa mtu,katika hilo wapo wengi lakini miongoni mwa watanzania hao ni
pamoja na mwalimu James Irenge ambaye alikuwa mwalimu wa Baba wa Taifa Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere katika shule ya msingi Mwisenge ya mjini Musoma mkoani
Mara.
Mwalimu Irenge akifanya mahojiano na
mwandishi wa gazeti hili nyumbani kwake maeneo ya Mwisenge mjini hapa anasema
kuwa alianza kumfahamu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka
1934 wakati alipokwenda kuanza darasa la kwanza katika shule hiyo ambapo yeye
alimfundisha Mwalimu Nyerere mwaka 1935 darasa la tatu mwaka mmoja baada ya
kuvushwa darasa la tatu kutokana na uelewa wake kuw mkubwa darasani.
Katika shule hiyo ya Mwisenge
Mwalimu Irenge alimfundisha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere darasa la Tatu somo
la Kiswahili,Hisabati na siasa ambapo anasema ingawa Mwalimu
Nyerere alikuwa anayamudu vyema masomo yote lakini somo la siasa ndilo somo
ambalo mwalimu alikuwa akipenda sana kusoma na kumudu vizuri darasani.
Anaongeza kuwa katika nyakati hizo
za ukoloni ilimlazimu kumfundisha mwalimu somo hilo nyakati za usiku kutokana
na wakoloni kutopenda wanafunzi wa Tanganyika(Tanzania) kufundishwa masomo
hayo.
Pamoja na kumfundisha masomo ya
siasa Mwalimu Irenge ambaye kwa sasa ana miaka (120) ambapo imekuwa vigumu hata
kukaa na muda wote kushinda amelala anasema kuwa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere
alikuwa na tabia moja ambayo ilimtofautisha na wanafunzi wenzake shuleni hapo
kitu ambacho kilipelekea hata kuwa kiongozi mwenye kujali watu anaowaongoza.
Marehemu Mwl James Irenge
Mwalimu Irenge anaongeza kuwa
Mwalimu Nyerere hakuwa na tabia ya kujisifu wala kujikweza ingawa alikuwa na
uwezo mkubwa darasani mpaka kufikia kuvuka darasa la pili na kwenda darasa la
tatu na pia ni mtu ambaye alikuwa anapenda kushirikiana na wenzake kwa
kila jambo,pamoja na kuwa hivyo alikuwa anchukia watu kuwa wavivu na mtu
asiyependa kumaptia mtu haki yake.
Anasema manyanyaso ya wakoloni ndio
anadhani yalipelekea Mwalimu Nyerere kupenda somo la siasa ili siku moja
akomboe Taifa lake ambalo wazee wake walikuwa wakinyanyaswa na wakoloni
‘Kambarage alikuwa anachukia
sana unyanyasaji nadhani hicho ndicho kilipelekea kupenda sana somo la siasa
ili siku moja awakomboe watanzania,hatukujua kama atakuwa rais lakini dhamira
yake ilikuwa ikionyesha kuwa ni mtu anayependa haki” alisema mwalimu Irenge
Pamoja na kuwepo watu mbalimbali
ambao wanatoa historia,Mwalimu Irenge anasema kuwa kumekuwepo na upotofu wa
historia ya mwalimu Nyerere kuwa katika maisha yake ya shule alikuwa akitembea
kutoka Butiama mpaka Mwisenge kitu ambacho si kweli,anaongeza kuwa kuwa
Kambarage alikuwa ni mtoto wa chifu na shule ya Mwisenge ilikuwa maalum kwa
watoto wa machifu ambapo Kambarage alikuwa ni mmoja wa watoto wa Chifu.
Katika hilo Mwalimu Irenge anaongeza
kuwa katika maisha yake yote ya shule Baba wa Taifa Mwalimu Julius
Nyerere hakuwa mtu ambaye anapenda michezo kwani muda mwingi kwake
ulikuwa ni kusoma vitabu vya siasa
Anasema ilikuwa ni vigumu nyakati
hizo kumkuta Mwalimu katika masuala ya kimichezo na kama ulikuwa unamhitaji
ilikuwa ni lazima umtafute sehemu ambayo alikuwa anapenda kusomea
'Kuna sehemu pale
Shuleni alikuwa anapenda kusomea na kama ulikuwa unamhitaji lazima utamkuta
pale” aliongeza mwalimu Irenge
Hali ya Mwalimu Irenge kwa sasa si
nzuri kiafya na kiuchumi ambapo anasema kuwa wakati mwalimu akiwa hai alikuwa
anamjali kwani kuna wakati alikuwa anakwenda Butiama na kukaa huko huku
wakiongea kuhusu masuala ya nchi na Mwalimu wakati mwingine alikuwa anakwenda
kwake kumjulia hali na ambapo kwa sasa imekuwa vigumu kwa viongozi kufika
katika mjini .
Mwalimu Irenge anasema kitendo hicho
kinamuumiza kwasasa kwani viongozi wa sasa wamekuwa tofauti na alivyokuwa
mwalimu Nyerere kwani kiongozi anayefika kumsalimia mara moja moja nyumbani
kwake ni mbunge wa jimbo la Musoma Vijijini Nimrod Mkono ambaye amekuwa mtu wa
karibu tangu kufariki kwa Mwalimu Nyerere.
Maisha ya mzee huyo anasema kuwa
alifurahi sana siku ambayo mwalimu alikuwa akikabidhiwa hati ya kuonyesha kuwa
nchi yetu imekuwa huru kwani aliona amewashinda wakoloni kupitia kwa Baba wa
Taifa Mwalimu Nyerere kwa kuwa harakati zilianzia shule za Mwisenge alipokuwa
akimfundisha somo la siasa.
‘Wakoloni walitunyanyasa sana
nyakati za ukoloni lakini siku anapokea hati ya kuonyesha kuwa nchi yetu
imekuwa huru nilifurahi sana maana niliona Kambarage Shujaa” anasema Mwalimu
Irenge.
Mwalimu James Irenge kwa sasa ni mtu
wa kushinda nyumbani na alistaafu kazi ya ualimu mwaka 1970 ambapo mpaka sasa
watoto 12 na wajukuu 27,Mwalimu huyo anaishi katika maisha ya mateso baada ya
serikali kushindwa kumlipa kiinua mgongo wakati alipostaafu anaongeza kuwa
tangu amestaafu amekuwa akilipwa pensheni ya shilingi mia mbili mpaka mwaka
2005 ndipo ikapandishiwa na kufikia shilingi 20,000 na mwaka 2010 ndipo
pensheni hiyo ikapanda mpaka kufikia kiasi cha shilingi 50,000.
Akiongea kwa tabu huku akisaidiwa na
kijana wake Mwalimu Irenge anasema aliishaandika barua sehemu mbalimbali
kuanzia kwenye ofisi ya Rais,haki za binadamu,wizara ya fedha na wizara ya kazi
ambapo barua ya wizara hiyo ilikabidhiwa kwa waziri wa wizara hiyo Profesa
Athuman Kapuya alipokuja Musoma kwenye sikukuu ya wafanyakazi mwaka 2009.
Pamoja na kunyimwa haki yake
mwalimu huyo anasema kuwa kwa sasa serikali imewabagua sana wazee kwani hata
yeye alialikwa mwaka jana tu kwenye sherehe ya wafanyakazi mjini hapa na kupewa
zawadi la Blanketi lakini malalamiko yake wameshindwa kuyasikiliza mpaka sasam
kitu kinazidi kumsononesha
Amesema mpaka leo hata mkuu wa Mkoa
wa Mara hajawahi kwenda kumtazama wakati anaishi jirani kitu inachoonyesha kuwa
viongozi wa siku hizi hawana upendo kwa wazee na hiyo ndiyo tofauti kubwa kati
ya viongozi kama Mwalimu Nyerere na wa leo
Akiongelea kifo cha Baba wa Taifa
Mwalimu Nyerere mwaka 1999,Mwalimu Irenge anasema kuwa Mwalimu hakupenda kufia
nje ya nchi yake ingawa kuna watu ambao walimlazimisha kwa kuwa walikuwa na
lengo lao katika nchi hii
Anasema kuwa wakati Mwalimu anaenda
Uingereza alilia wakati akiongea naye kwani alisema kuwa hawezi kurudi mzima na
anawaacha watu wake,anasema kuwa kwasasa nchi imepoteza uelekeo kwani baada ya
kufa Mwalimu Nyerere nchi imekuwa ya kila mtu kufanya anavyotaka huku rushwa na
ufisadi ukizidi kuwaumiza watanzania walio wengi.
Akiongelea wizi uliotokea hivi
karibuni benki kuu na mikataba mibovu inayofanywa na serikali ni kipimo tosha
kuwa serikali haiko makini katika masuala makubwa ya nchi na hivyo kuacha
watanzania wakiishi katika umaskini mkubwa huku viongozi wachache wakiendelea
kuwalaghai wananchi.
Anasema leo viongozi wetu wamekuwa
kama wakoloni maana wakoloni ndio walikuwa wanatudanganya sana,kitu ambacho leo
tena kimerudi kwa viongozi wetu.
“Hawa viongozi wetu leo
wamekuwa kama wakoloni maana wamekuwa wakiwalaghai wananchi kwa vitu vidogo
huku wao wakiendelea kuwa matajiri” aliongeza Mwalimu Irenge
Pamoja na Mwalimu huyo kuwa mwasisis
wa TANU lakini anasema Chama Cha Mapinduzi kimepoteza mwelekeo kwani lengo lake
lilikuwa ni kuwasaidia wakulima na wafanyakazi katika kuendeleza Taifa lao
lakini kwa sasa chama hicho kimekuwa cha wafanyabiashara kitu ambacho Mwalimu
hakupenda kwani aliona madhara yake
Mbali na Mwalimu Irenge kumfundisha
Mwalimu Nyerere katika shule ya Mwisenge mjini hapa lakini mwalimu huyo anasema
pia kuna viongozi ambao aliwafundisha katika shule hiyo.
Akiwataja kwa tabu kabla ya kupata
ukweli wa majina hayo katika ofisi ya shule hiyo viongozi hao ni pamoja na
Seleman Kitundu mwasisi wa Tanu na Oswald Marwa ambao wamewahi kuwa wakuu wa
mikoa, huku Joseph Warioba alikuwa wazari mkuu wa Tanzania,Bhoke Munanka ambaye
amewahi kuwa waziri ofisi ya Rais, Pius Ng’wandu,Richard Wambura ambaye amewahi
kuwa balozi wakiwakilisha Tanzania,Mtaragara Chilangi ambaye amewahi kuwa
katibu wa Elimu,Joseph Butiku ambaye amewahi kuwa Ka tibu wa Rais na mkuu wa
Mkoa.
Baada ya kustaafu maisha ya Mwalimu
Irenge kwasasa si mazuri kama anavyosema yeye ambapo kibaya zaidi anasema
atajisikia vibaya kama ataondoka duniani pasipo kulipwa haki yake ambayo
anaidai Serikali,mbali na hilo pia Mwalimu Irenge anasema kuwa uchaguzi wa
Mwaka huu watanzania wapige kura kwa amani kwani hilo litakuwa jambo jema
katika miaka kumi na moja ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Mwalimu Irenge alimalizia kwa kusema
kuwa viongozi wabadilike na wawathamini wananchi kwani leo wananchi wanaishi
kama vile si watanzania na pia hawathaminiwi na kuwafanya wachukie nchi yao.
“Mimi naomba viongozi
wawajali watanzania ili wawe na upendo kwa nchi yao maana kama hawatawathamini
watakuwa wanaichukia nchi yao” alimalizia Mwalimu Irenge
No comments:
Post a Comment