Wednesday, April 25, 2012

WATUPA MPANGO WAKE WA MAENDELEO, PIA WAJIPANGA KUKWAMISHA BAJETI, CHADEMA WAANDAA MAANDAMANO

 Daniel Mjema, Dodoma na Editha Majura, Dar

KITENDO cha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kushindwa kuzungumzia shinikizo la baadhi ya wabunge kutaka mawaziri wanane wajiuzulu, kimeonekana kuwakera wawakilishi hao ambao sasa wameamua kuibana Serikali huku wakiapa kukwamisha bajeti za mawaziri hao katika Bunge lijalo la Bajeti.


Jana walianza kuonyesha makali baada ya kukataa mapendekezo ya Mfumo wa Mpango wa Mabadiliko wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2012/2013 wakisema hauna jipya na umetayarishwa kwa mfumo uleule kwa miaka 15 mfululizo.

Juzi, Pinda aliahirisha Bunge bila kugusia shinikizo la wabunge hao kutaka Serikali iwawajibishe Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo; Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja; Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu; Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami; Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe; Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), George Mkuchika.


Wakizungumza na kwa nyakati tofauti jana, wabunge hao, wengi wao wakiwa ni wa CCM, walisema silaha pekee waliyobaki nayo ni kukwamisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2012/2013 katika kikao kijacho cha Bunge.
 
Wabunge hao pia wameonya kwamba kutojiuzulu kwa mawaziri hao kutaiweka CCM njia panda katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwani hoja ya ufisadi ndiyo iliyowafanya wenzao wengi wasirudi bungeni.
 
“Silaha kubwa tuliyobaki nayo sasa ni kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu na nakuambia kama ile karatasi ingerudi upya leo idadi ya wabunge wa CCM ambao wangetia saini ingetikisa nchi,” alisema James Lembeli wa Kahama (CCM).
 
Lembeli alisema anashangaa kuona mawaziri waliotakiwa kujipima wenyewe na kuandika barua za kujiuzulu wakigoma kufanya hivyo na Serikali kupuuza hoja hiyo akisema, hatashangaa kuona Watanzania wakiingia mitaani.
 
“Kitendo cha Waziri Mkuu kutosema chochote kuhusu kujiuzulu kwa mawaziri hao wakati akihitimisha Bunge ni kuiingiza nchi kwenye mgogoro mkubwa. Serikali ifahamu kuwa, ipo madarakani kwa ridhaa ya wananchi,” alisema.
 
Lembeli alisema wananchi walipokea kwa shangwe taarifa ya mawaziri hao kutakiwa kujiuzulu lakini, kitendo cha Waziri Mkuu kuwaacha na kuikwepa hoja hiyo alipokuwa akiahirisha Mkutano wa Bunge juzi, kitaongeza chuki ya wananchi dhidi ya Serikali yao kwa kuwa wataamini inawakumbatia mafisadi.
 
 
“Inakuwaje hawa mawaziri wanane tu watake kuitumbukiza nchi kwenye machafuko? Uwaziri ni dhamana aangalie huko kwenye vijiwe na mitaani watu walivyoshangilia kusikia wametakiwa kujiuzulu leo wanagoma, unamgomea nani?” alihoji Lembeli.
 
Lembeli alisema anaamini Rais atafanya uamuzi mgumu na wa haraka kabla ya Bunge la Bajeti vinginevyo Waziri Mkulo na mawaziri wengine watakuwa na wakati mgumu ambao haujawahi kuonekana katika kupitisha bajeti za wizara zao.
Mbunge mmoja wa Viti Maalumu kwa tiketi ya CCM kutoka Kanda ya Ziwa, alisema ukimya wa Rais Kikwete na kiburi cha mawaziri wake wenye tuhuma za kweli kugoma kujiuzulu, kumezidi kukifanya chama hicho tawala kuporomoka umaarufu.

Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), alisema Rais Kikwete anapaswa kuheshimu maoni na maelekezo ya wabunge na kusema hata kutaka mawaziri wajiuzulu ni utaratibu tu wa kistaarabu.

“Sisi Wabunge 76 tuliosaini hoja ya kutaka Waziri Mkuu ang’oke tumejitoa sadaka kwa maslahi ya nchi lakini naamini wakati wa kumpigia kura Waziri Mkuu, wengi zaidi watatuunga mkono kwa jinsi walivyokerwa na jambo hili,” alisema.
 
“Bunge safari hii limeisha kimyakimya, Spika alipowahoji wanaoafiki hoja ya Waziri Mkuu ya kuliahirisha Bunge waliosema siyo ndiyo waliokuwa wengi na kama ulifuatilia Bunge lilikuwa kimya si kawaida… Rais anatakiwa alione hilo,” alisema.
 
Mbunge wa Kinondoni, Iddi Azzan (CCM), alisema amesikitishwa na hatua ya mawaziri hao kugoma kujiuzulu na kwamba kwa hali ilivyo, busara ya kawaida inataka mawaziri hao wajiuzulu.
 
“Kwa busara ya kawaida wote wanaotuhumiwa kwa wizara zao kufanya madudu wangeacha uroho wa madaraka na kujiuzulu ili kuitikia kilio cha wabunge na Watanzania kwa sababu upepo huko nje sio mzuri hata kidogo,” alisema Azzan.
 
Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM) alisema taifa limeghafilika kwa sababu wananchi wengi nchi nzima walikaa kwenye luninga na kusikiliza redio juzi jioni wakitarajia Waziri Mkuu angetamka moja kwa moja kuwang’oa mawaziri hao.
 
“Jana kwenye baa na vijiwe ilikuwa kama vile kuna mechi ya kukata na shoka... kwa jinsi idadi kubwa ya wananchi walivyofuatilia hotuba ya Waziri Mkuu lakini mwisho wa siku akawaacha solemba,” alisema.
Nape, Mukama

Baadhi ya wabunge wa CCM waliosaini barua ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu wamedai kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho Wilson Mukama amewatisha.

Kanji Lugola wa Mwibara alidai jana kwamba usiku wa kuamkia Jumapili, siku moja baada ya kusaini hati hiyo alipokea simu kutoka kwa Mukama akimtolea maneno makali kutokana na hatua yake hiyo.

“Alizungumza maneno mengi ya vitisho kwa mfululizo bila hata kunipa nafasi ya kujieleza, akasema, ‘nakuja huko wewe na huyo mwenzako mliosaini mtanitambua,’ kuona hivyo tukaondoka Dodoma usiku huohuo,” Lugola alieleza.

Alisema walisafiri hadi Dar es Salaam na kwamba walihudhuria kikao cha Bunge cha Jumatatu iliyopita wakitokea mafichoni.Alipotakiwa kuthibitisha madai hayo Mukama alisema: “Siwezi kutoa habari kwa simu.”

Alipopigiwa tena na kuombwa afuatwe ofisini alisema, “Kwa leo haitawezekana maana niko njiani natokea Dodoma sasa hivi nimefika Gairo, kama unaweza njoo kesho.”

Lugola alidai wakati akipokea vitisho hivyo kutoka kwa Mukama waliokuwa wamesaini kwa upande wa CCM walikuwa yeye na Filikunjombe, baadaye alifuatia na Nimrod Mkono.

No comments:

Post a Comment