Wednesday, April 25, 2012

                       JOHN MNYIKA ATEMA CHECHE KWA PINDA. 

Katibu Mwenezi wa Chama cha Demakrasia na Maendeleo Mh. John Mnyika  amesema leo mjini Dodoma kuwa  Waziri Mkuu Mizengo Pinda anapaswa kuagiza timu ya wataalamu aliyoiunda kufuatia mkutano wake wadau wa viwanda vya nguo kufanya uchunguzi maalum kuhusu kiwanda cha nguo cha Urafiki.
Mnyika amesema kuwa ukaguzi huo wa Timu ya Wataalamu kwa maagizo ya Waziri Mkuu Pinda utachangia katika kunusuru Kiwanda cha Nguo cha Urafiki dhidi ya udhaifu wa kiutendaji, ufisadi dhidi ya mali za kampuni, kulinda maslahi ya wafanyakazi na kushughulikia kasoro katika mchakato wa ubinafsishaji.
Katika hotuba yake ya kuahirisha bunge tarehe 23 Aprili 2012 Waziri Mkuu Pinda alieleza taifa kuwa kufuatia mkutano wake na wadau wa tarehe 23 Machi 2012 ameunda kamati ya wataalamu ya kuangalia changamoto zinazokabili viwanda vya nguo nchini ili kuviwezesha kuchangia kwenye mapato ya nchi na katika kuongeza ajira.
Hatahivyo Mnyika amesema ni muhimu Waziri Mkuu Pinda na timu ya wataalamu hao wakazingatia kuwa matatizo ya kiwanda cha urafiki ni zaidi ya changamoto za kawaida kwa kuwa ni matokeo ya kasoro katika mchakato mzima wa ubinafsishaji, udhaifu wa kiutendaji wa miaka mingi pamoja na ufisadi uliokithiri unaohitaji uchunguzi maalum.
Kutokana na hali hiyo Mnyika ametoa wito kwa Serikali kuingilia kati kupitia Wizara ya Fedha hususani Ofisi ya Msajili wa Hazina na Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) na Wizara ya Viwanda na Biashara kuchukua hatua zinazostahili juu ya kiwanda cha Urafiki.
Aidha, kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara kuchukua hatua za kuisimamia serikali ili kuharakisha hatua za kunusuru kiwanda hiki ili kuonyesha pia mfano wa hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuhusu viwanda vingine. Hata hivyo mpaka sasa hakuna hatua kamili zilizochukuliwa na Wizara na Mamlaka husika hivyo Waziri Mkuu Pinda anapaswa kuingilia kati kusukuma hatua kuchukuliwa baadala ya kutoa kauli za ujumla kwamba serikali inalinda viwanda vya ndani.

No comments:

Post a Comment